Tafuta

Wawakilishi wa Kongamano la Kimataifa la Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika “Africa Compact on Education” kwa muda wa siku mbili wamekuwa wakijadili kuhusu Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika. Wawakilishi wa Kongamano la Kimataifa la Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika “Africa Compact on Education” kwa muda wa siku mbili wamekuwa wakijadili kuhusu Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika. 

Papa Francisko: Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika: Ushiriki

Papa amemtaja Mtumishi wa Mungu Mwalimu J. K. Nyerere, Muasisi wa Taifa la Tanzania aliyetoa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi ya adui ujinga kwa kukazia elimu kwa wote. Mtumishi wa Mungu Mwalimu Nyerere aliyarutubisha maisha yake kwa Ibada ya Misa Takatifu, na kwake Ekaristi Takatifu, kilikuwa ni chakula safi cha maisha ya kiroho, kilichomwezesha kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake kwa watu wa Mungu nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ubora wa elimu unapimwa kwa kuangalia thamani yake katika maisha na uwezo wa kuanzisha utamaduni mpya unaowashirikisha watu wengi zaidi. Baba Mtakatifu anapenda kutoa wito kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kutoka katika sekta ya utamaduni, sayansi, sanaa na michezo na wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii kushiriki katika Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” kwa njia ya ushuhuda na kazi zao. Wasaidie kuhamasisha tunu msingi za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani; uzuri, wema, ukarimu na udugu wa kibinadamu. Kila mtu ajitahidi kuwajibika, ili kuendeleza mchakato wa mageuzi; ili kuganga na kuponya ulimwengu huu ambao umejeruhiwa vibaya; kila mmoja, akijitahidi kuwa ni Msamaria mwema, anayeguswa na mahangaiko ya wengine, badala ya kuchochea chuki na uhasama kati ya jamii. Huu ni mfumo wa elimu wenye mwono mpana na wenye uwezo wa kuwashirikisha wote ili kutoa majibu yatakayosaidia kujenga mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ulimwengu mamboleo unawahitaji watu watakaojenga na kudumisha amani na utulivu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila mtu binafsi, anawajibika kutoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa mfumo mpya wa elimu: utu na heshima ya binadamu, ili hatimaye, kila mtu aweze kuonesha: uzuri na upekee wake; uwezo wa kuhusiana na kufungamana na wengine katika hali na mazingira yanayowazunguka, ili kuondokana na utamaduni wa chuki na uhasama ambao kimsingi umepitwa na wakati. Huu ni muda wa kusikiliza na kujibu kilio cha watoto na vijana wanaorithishwa tunu msingi, uelewa na ufahamu, ili kwa pamoja waweze kujenga leo na kesho inayosimikwa katika haki, amani na maisha bora zaidi.

Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa
Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa

Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wengi zaidi wanashiriki katika mchakato wa elimu bora. Katika hali na mazingira kama haya, familia zinapaswa kuwa ni sehemu ya wadau wakuu katika sekta ya elimu. Watu wajifunze na kuwafunza wengine ukarimu, kwa kutoa msaada zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawakilishi wa Kongamano la Kimataifa la Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika “Africa Compact on Education” kwa muda wa siku mbili wamekuwa wakijadili kuhusu Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika na Alhamisi, tarehe 1 Juni 2023 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekazia kuhusu ujenzi wa mtandao wa mfumo wa elimu Barani Afrika; Umuhimu wa elimu bora kwa vijana wa kizazi kipya Barani Afrika na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ina matumaini makubwa na Bara la Afrika. Mkutano huu ni mwendelezo wa Kongamano la Kimataifa la Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika “Africa Compact on Education” lililofanyika huko Kinshasa, kwa udhamini wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC na kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kinshasa. Baba Mtakatifu anasema, Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika unapaswa kumwilishwa katika matendo, kwa ushiriki wa watu wengi katika jamii, kwa kujenga mtandao wa mfumo wa elimu Barani Afrika unaojikita katika ushiriki wa jamii nzima. Mchakato huu unakwenda sanjari na ujenzi wa mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu na hapa huu ni msingi wa imani.

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa
Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa

Baba Mtakatifu amewakumbusha wajumbe wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika kwamba, Bara la Afrika bado ni kijana sana na vijana wengi Barani Afrika wana akili sana, kumbe, huu ni mwaliko wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya kutoka Barani Afrika. Huu ni muda muafaka wa kushirikiana kwa karibu zaidi na serikali mbalimbali kwa ajili ya kuwaandaa waalimu wenye ujuzi na maarifa na pamoja na kuwaundia mazingira bora ya kufundishia, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kitaaluma vyema zaidi. Jumuiya ya Kimataifa inaliangalia Bara la Afrika kwa imani na matumaini makubwa, kutokana na rasilimali, amana na utajiri ulioko Barani Afrika; maendeleo makubwa ya kiuchumi bila kusahau mapokeo ya elimu asilia kutoka Barani Afrika inayojikita katika ukarimu na mshikamano mambo yanayoingia vyema katika Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika na kuboreshwa zaidi na tunu msingi za Kiinjili. Mfumo huu unaweza kuchota amana na utajiri mkubwa kutoka kwa wanafalsafa wa Kiafrika na waalimu na wanasiasa kama Mzee Nelson Mandela katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho na kwamba, elimu ni chombo madhubuti kabisa cha kuleta mabadiliko duniani. Baba Mtakatifu amemtaja Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Muasisi wa Taifa la Tanzania aliyetoa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi ya adui ujinga kwa kukazia elimu kwa wote. Mtumishi wa Mungu Mwalimu Nyerere aliyarutubisha maisha yake kwa kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu, na kwake Ekaristi Takatifu, kilikuwa ni chakula safi cha maisha ya kiroho, kilichomwezesha kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Kwa hakika, Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika ni jambo jipya Barani Afrika linalosimikwa katika mapokeo ya utamaduni wa Kiafrika na Imani ya Kikristo, kumbe, hakuna sababu ya kuogopa. Bikira Maria, Mama wa Afrika awasindikize katika utekelezaji wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika.

Mwalimu J.K. Nyerere alikazia umuhimu wa elimu ya umma.
Mwalimu J.K. Nyerere alikazia umuhimu wa elimu ya umma.

Wakati huo huo, Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, ambaye ni mjumbe wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika katika mahojiano maalum na Radio Vatican amefafanua umuhimu wa elimu kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, wazo kuu linalopewa kipaumbele na Baba Mtakatifu Francisko. Elimu ielekezwe kwa mwanadamu ili iweze kujibu masuala na matamanio yake halali, imwandae mwanadamu kwa ajili ya kutengeneza na kuboresha maisha yake, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, elimu itoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, itoe fursa na mwelekeo mpana zaidi, ili fursa hizi ziweze kufanyiwa kazi; kwa kukazia: usawa na kwamba, watu wote wanapaswa kufaidika na mfumo mpya wa elimu; watu wajisadake kuiendeleza duniani, kuilinda na kuipendezesha na elimu kiwe ni chombo kitakacho tekeleza majukumu yote haya.

Papa Elimu Barani Afrika
01 June 2023, 15:19