Kardinali Michael Czerny Mwakilishi wa Papa Kwenye Jubilei ya Miaka 140 ya Uinjilishaji Congo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, kumwakilisha katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 140 ya Uinjilishaji nchini Congo. Kilele cha Maadhimisho haya ni tarehe 4 Juni 2023. Hizi zilikuwa ni juhudi za uinjilishaji zilizotekelezwa na Papa Leo XIII. Kumbe, hili ni tukio la kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuliwezesha Kanisa kutangaza amani na kuendelea kuinjilisha. Katika miaka hii 140 kumekuwepo na wainjilishaji wengi waliosimama kidete kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake kwa bidii, juhudi, maarifa, kwa upendo na bila woga.
Ni katika muktadha huu wa kumbukizi ya Miaka 140 ya Uinjilishaji nchini Congo, Baba Mtakatifu amemteuwa Kardinali Michael Czerny, atakaye ambatana na Askofu mkuu Benvenuti Manamika Bafouakouahou wa Jimbo kuu la Brazzaville na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Congo ambaye analifahamu sana Kanisa la Congo, mahitaji yake msingi na matumaini ya watu wa Mungu Barani Afrika. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime, ari na moyo mkuu watu wa Mungu nchini Congo wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 140 ya Uinjilishaji na anapenda kuwapatia baraka zake za kitume. Bikira Maria, Malkia wa Afrika awaombee matumaini, ulinzi, imani na upendo; ili waweze kushikamana, ili hatimaye, kujenga na kudumisha haki, amani, maridhiano na maendeleo endelevu ya binadamu. Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume, kwa watu wa Mungu watakaokusanyika tarehe 4 Juni 2023 kuadhimisha tukio hili kuu ya imani. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea ili furaha na upendo unaobubujika katika maadhimisho haya uweze kuendelea kufanya kazi wakati wote.