Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hospitali ni mahali pa mateso na mahangaiko yua binadamu, lakini pia ni mahali pa matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hospitali ni mahali pa mateso na mahangaiko yua binadamu, lakini pia ni mahali pa matumaini.   (ANSA)

Papa Francisko Asema Hospitali ni Mahali Pa Mateso na Matumaini

Baba Mtakatifu anasema, hospitali ni mahali pa mateso na mahangaiko yua binadamu, lakini pia ni mahali pa matumaini. Akiwa hospitalini Gemelli ameonja mazingira ya kifamilia, udugu na ukarimu; mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya yake na hatimaye, kuruhusiwa kurejea tena kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha kuendelea na maisha pamoja na shughuli zake za kila siku. Hii ni sehemu ya barua ya shukrani kwa uongozi wa Hospitali ya Gemelli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Falsafa ya neno asante ni kuomba tena! Waswahili husema, “Moyo usio na shukrani hukausha mema yote.” Baba Mtakatifu Francisko baada ya kulazwa tarehe 7 Juni 2023 na kufanyiwa operesheni kubwa kwenye utumbo mpana; aliendelea kupata matibabu hadi aliporuhusiwa tarehe 16 Juni 2023, akawashukuru wale wote waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao. Siku hiyo hiyo alikwenda moja kwa moja kumshukuru Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Popoli Romani” kwa sala, maombezi na tunza yake ya kimama wakati wote alipokuwa amelazwa Hospitali ya Gemelli. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 19 Juni 2023 amemwandikia barua Professa Marco Elefanti, Rais wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli IRCCS “Fondazione Policlinico Universitario Agostino Gemelli IRCCS” kumshukuru kwa niaba ya Familia kubwa ya watu wa Mungu Hospitali ya Gemelli, Roma, kwa ukarimu na udugu wao wa kibinadamu, ambao ameuonja wakati wote alipokuwa amelazwa hospitalini hapo, kiasi cha kumfanya ajisikie kuwa yuko nyumbani!

Hospitali ni mahali pa mateso na matumaini ya wagonjwa
Hospitali ni mahali pa mateso na matumaini ya wagonjwa

Baba Mtakatifu anasema, hospitali ni mahali pa mateso na mahangaiko ya binadamu, lakini pia ni mahali pa matumaini. Akiwa hospitalini hapo ameonja mazingira ya kifamilia, udugu na ukarimu; mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya yake na hatimaye, kuruhusiwa kurejea tena kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha kuendelea na maisha pamoja na shughuli zake za kila siku. Anawashukuru na kuwapongeza kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma ya afya, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Huduma hii imenogeshwa kwa weledi wa kisayansi. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ndani ya moyo wake, anabeba nyuso, historia na mahangaiko ya watu mbalimbali.

Hospitalini Papa anasema ameonja upendo, ukarimu na mshikamano
Hospitalini Papa anasema ameonja upendo, ukarimu na mshikamano

Wakati huo huo, Professa Marco Elefanti, Rais wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli IRCCS “Fondazione Policlinico Universitario Agostino Gemelli IRCCS” baada ya kupata barua kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko akiwashukuru kwa huduma makini waliyompatia, ameamua kuwashirikisha furaha, wafanyakazi wote wa hospitalini hapo. Hospitali ya Gemelli ni sawa na mji mdogo ndani ya Jiji kuu la Roma. Hapa ni mahali ambapo kila siku kuna maelfu ya watu wanaofika wakiwa na matumaini pamoja na wasiwasi mbalimbali kutokana na mahangaiko yao. Hospitalini hapo, licha ya kutoa huduma ya tiba, wagonjwa wanapata pia huduma ya kiroho na hivyo Hospitali inamhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; daima utu na heshima yake vikipewa msukumo wa pekee. Huduma hii anasema Baba Mtakatifu inakuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini wakati wa mateso na majaribu katika maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kazi nyeti na ngumu wanayoitekeleza Hospitalini hapo!

Papa anawashukuru wote waliomhudumia.
Papa anawashukuru wote waliomhudumia.

Hii ni huduma ya huruma ambayo kwa njia ya wagonjwa, wahudumu hao wanaweza kukutana na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua kwamba, ameona kwa macho yake mwenyewe na akatunza hicho alichokiona na atakiwakilisha mbele ya Mwenyezi Mungu kama ushuhuda wa matendo ya huruma mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kumshukuru tena Professa Marco Elefanti, Rais wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli IRCCS, wafanyakazi na wale wote wanaounda familia kubwa ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Wote hawa amewapatia baraka zake za kitume na kuwaomba kuendelea kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa Afya Gemelli
26 Juni 2023, 16:30