Mkutano Mkuu wa 34 wa Shirika la Waassumptionist: Kuishi na Kutangaza Matumaini ya Injili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Shirika la Waagustino wa Kupalizwa, au “Waassumptionist”: “Congregatio Augustinianorum ab Assumptione” kwa lugha ya Kifaransa “Religieux de l'Assomption au Assompionnistes” na kwa kifupi A.A. lilianzishwa na Emmanuel d'Alzon kunako mwaka wa 1845 na kutambuliwa rasmi na Vatican kunako mwaka 1864. Hili ni Shirika linalojipambanua kwa ajili elimu ya Kikristo, Malezi na Makuzi kwa vijana wa kizazi kipya; huduma ya shughuli za kichungaji maparokiani, umisionari na jitihada za kukoleza majadiliano ya kiekumene yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shirika hili tangu tarehe 1 Juni hadi tarehe 21 limekuwa likiadhimisha Mkutano mkuu wa 34 ulionogeshwa na kauli mbiu “Ufalme wa Mungu umekaribia: kuishi na kutangaza matumaini ya Injili.”
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 22 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na Wanashirika wa “Assumption”. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu ametafakari kuhusu kauli mbiu ya Mkutano mkuu wa 34: “Ufalme wa Mungu umekaribia: kuishi na kutangaza matumaini ya Injili” mintarafu moyo wa Mtakatifu Augustino “Adveniat Regnum tuum”, Utume kwa mahujaji, amewatia shime kuendeleza utume wao huko Mashariki ya Kati pamoja na kuwekeza katika nchi za Kimisionari pamoja na kukuza upendo ndani mwao: upendo kwa Kristo Yesu, Bikira Maria na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza wajumbe wa mkutano mkuu pamoja na viongozi wote waliochaguliwa kuliongoza Shirika. Kuishi na kutangaza Ufalme wa Mungu na matumaini ya Kiinjili ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, mambo yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Watawa wanapaswa kuwa ni alama ya ukaribu wa Mungu kwa watu wanaowazunguka na kuwahudumia. Ukaribu huu ujioneshe kwa utume unaotekelezwa na Shirika, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Ukaribu wao ujioneshe na kushuhudiwa katika umoja na mshikamano unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Ni kwa njia ya ushuhuda wa Kiinjili watu wataweza kuonja uwepo wa Uaflme wa Mungu. Baba Mtakatifu amewapongeza wanashirika kwa kujizatiti kikamilifu katika huduma kwa mahujaji wanaotembelea Madhabahu ya Lourdes, kiasi hata cha kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Amerika ya Kusini pamoja na sehemu mbalimbali za dunia.
Hii ni huduma inayotolewa hata kwa watu ambao wako nje ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko amewatia shime wamisionari hawa kuendeleza utume wao huko Mashariki ya Kati, ambako Ukristo uko mashakani na kwamba, vita kati ya Urusi na Ukrain inatishia msingi wa amani na maridhiano. Baba Mtakatifu kwa niaba ya Kanisa amewapongeza watawa hawa kwa uwepo wao nchini Bulgaria; kwa kuendelea kujikita katika majadiano ya kiekumene na kidini nchini Bulgaria. Baba Mtakatifu anawataka wamisionari hawa kuendelea kuwa ni vyombo na wajenzi wa umoja, ushirika wa huduma na amani. Amewahakikishia uwepo wake wa sala ili kuwekeza kwa nguvu zaidi katika nchi changa duniani. Amewapongeza kwa kuwekeza zaidi katika malezi na majiundo ya wanashirika wao, hali inayoweka matumaini makubwa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwa maisha na utume wa Shirika. Hii pia ni changamoto kubwa katika mchakato wa kutangaza na kumwilisha karama ya Shirika. Baba Mtakatifu anaungana pamoja nao kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mchakato huu unaopania kupyaisha maisha na utume wa Shirika, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, kwani upya wa maisha ni sehemu ya vinasaba vya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Baba Mtakatifu anawataka wanashirika hawa kukuza na kudumisha upendo kwa Kristo yesu, Bikira Maria na Kanisa. Ni katika muktadha huu, wataendelea kuwa waaminifu kwa karama ya Shirika inayopyaishwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wanaowahudumia. Katika mambo yote haya, waendelee kutumainia sala na imani yake kwao na hatimaye, amewatakia mwisho mwema wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 34 wa Shirika na utume mwema, mahali popote pale ambapo, Kristo Yesu anawatuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.