Kumbukizi ya Miaka 50 Kwa Makumbusho ya Kisasa na Jumba la Makumbusho ya Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Makumbusho ya Kisasa pamoja na Jumba la Makumbusho ya Vatican, Ijumaa tarehe 23 Juni 2023, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na wasanii zaidi ya 200 kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watu mashuhuri kama: Wachoraji, wachongaji, wasanifu majengo, waandishi, washairi, wanamuziki na waigizaji. Hadhira hii imekusanyika kwenye Kikanisa cha Sistine, kama sehemu ya mfululizo wa mikutano ya Baba Mtakatifu pamoja na wasanii. Tukio kama hili liliadhimishwa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1964, kwa kuhusisha uhusiano wa karibu uliopo kati ya Kanisa na Wasanii wenyewe. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kusherehekea kazi na maisha ya wasanii kwa kuangalia mchango wao katika ujenzi wa hisia ya utu wa mwanadamu sanjari na kukuza kanuni maadili ya pamoja. Hii ni sehemu ya mpango mkakati wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu linalopania kujenga na kukuza mahusiano kati ya Vatican na ulimwengu wa utamaduni; kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi kama chombo muhimu kwa ajili ya kukutana katika ukweli, mwingiliano wa pamoja unaopania pamoja na mambo mengine kuimarisha sanaa, fasihi na utamaduni, ili wasanii wahisi zaidi kwamba wanatambuliwa na kuthaminiwa na Kanisa katika mchakato wa kutafuta na kudumisha ukweli, wema na uzuri. Kardinali José Tolentino de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu anasema, Kanisa linapaswa kuzindua na kupyaisha uzoefu na mang’amuzi ya Kanisa kama rafiki wa wasanii wanaojitahidi kujibu maswali ambayo walimwengu wanauliza katika zama hizi, tayari kukuza mchakato wa majadiliano, ukuaji na maelewano.
Tukio hili limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu, Gavana wa Mji wa Vatican, Makumbusho ya Vatican pamoja na Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wasanii hawa amekazia mahusiano ya asili na maalum kati ya Kanisa na wasanii; kipaji na ubunifu wa msanii; wasanii wanao uwezo wa kuota ndoto na kuleta upya katika historia ya maisha ya mwanadamu; wao ni kielelezo cha utu wa binadamu; sanaa inafumbatwa katika uzuri ambacho ni kipaji tendaji na kamwe wasiwasahau maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, msanii ni mtu anayezama sana katika maisha na ulimwengu katika ujumla wake na kwamba, binadamu anatembea katika roho na kwamba, mahusiano na mafungamano kati ya Kanisa na wasanii ni mambo ya kawaida lakini pia ni mambo maalum, hazina na amana kwa wote. Walimwengu wanahitaji kuona matunda ya usikivu, uhuru na heshima. Kazi za kisanii zinamwezesha mwanadamu kupenya katika undani ili hatimaye kuzama katika ukweli wa mambo na kwamba, binadamu ameumbwa kwa ajili ya kufurahia maisha na wala si kifo. Kazi ya ubunifu wa msanii inashiriki katika kazi ya uumbaji iliyofanywa na Mwenyezi Mungu na hivyo wasanii wanakuwa ni jicho linayotazama na kuota ndoto; waangalie kile wanachokiona na kuota kile wanachokiona, tayari kuleta mambo mapya katika historia ya mwanadamu.
Wasanii ni kama manabii wanaoangalia uzuri wa mambo ya mbeleni, huku wakitoa changamoto, kwa kushutumu na kulaani hotuba nyepesi nyepesi, uchu wa mali na madaraka. Kejeli na unabii; usheshi na kejeli ni mambo yanayopaswa kukuzwa na kudumishwa Biblia imejaa nyakati za kejeli, ambamo dhana ya kujitosheleza, kujizuia, ukosefu wa haki, unyama hufanyiwa mzaha wakati wamevikwa mamlaka na wakati mwingine hata kwa utakatifu kwa ajili ya kukosoa. Wasanii ni watu ambao wanapaswa kujipambanua katika utetezi wa maisha ya binadamu, haki jamii pamoja na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja. Moja ya vitu vinavyoleta sanaa karibu na imani ni ukweli kwamba inasumbua kidogo. Sanaa na imani haziwezi kuacha mambo kama yalivyo: kwani yanabadilishwa, yanageuzwa na yanasonga mbele. Sanaa huwapata watu amani na kuwafanya wawe macho na kwamba, wasanii hawana budi kuwa ni vyombo vya kutoa mwanga wa matumaini katika giza la ubinafsi na hali ya kutojali, kwa kuzamisha nuru na uzuri unaookoa. Wengi wanatumaini kwamba, sanaa itarejea katika uzuri wake, lakini kuna uzuri usio na maana, uzuri wa juu juu na wa bandia hata kuna uzuri wa udanganyifu, ule uzuri wa kujipodoa, lakini uzuri wa kweli unajikita katika maelewano. Baba Mtakatifu Francisko anazidi kusema kwamba, wanataalimungu wanawezea Ubaba wa Mwenyezi Mungu; Ushiriki wa Kristo Yesu na Maelewano ni kazi ya Roho Mtakatifu na mwelekeo wa kibinadamu ni wa kiroho zaidi na kwamba, uzuri wa kweli kimsingi ni onesho la maelewano.
Roho wa Mungu ndiye mpatanishi mkuu wa ulimwengu na ndiye anayetenda na kuleta umoja hata katika tofauti, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anayeunganisha tofauti na hivyo kujenga umoja ambao si usawa.Upatanifu hufanya miujiza hii, kama ilivyojitokeza wakati wa Sherehe ya Pentekoste ile ya kwanza. Huu ni ujumbe unaogusa uhasia wa mambo duniani. Hiki ni kipindi kinachotawaliwa na ukoloni wa kitikadi wa vyombo vya mawasiliano ya kijamii; vita, kinzani na migogoro inavyozidi kupamba moto sehemu mbalimbali za dunia sanjari na utandawazi unaochanganya watu, kiasi kwamba, hata Kanisa pia linaweza kuathirika kwa mambo haya. Wasanii wanaweza kusaidia kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili kuunda maelewano. Kabla ya kuhitimisha hotuba yake, Baba Mtakatifu amewataka wasanii kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kuwakumbuka na kuwaenzi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hata katika zama hizi, maskini nao wanahitaji sanaa na uzuri sanjari na kuonja tena uzuri wa maisha: Wasanii wawe ni kipaza sauti cha maskini kwa kutafsiri kilio chao katika hali ya ukimya. Baba Mtakatifu anawataka wasanii wamtukuze Mungu Mwenyezi, Baba wa wote ambaye kila mtu anamtafuta hata kupitia katika sanaa.