Tafuta

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amekazia kuhusu: Dhamana na wajibu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amekazia kuhusu: Dhamana na wajibu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Hotuba ya Baba Mtakatifu Kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa: Udugu na Amani

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amekazia kuhusu: Dhamana na wajibu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; Utandawazi unaokumbana na ukame wa udugu wa kibinadamu; ndoto kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu ni amani inayojengwa katika sadaka, majadiliano na diplomasia na kumwilishwa katika udugu wa kibinadamu na kamwe amani haiwezi kuelea kwenye ombwe! Udugu wa kibinadamu na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, “The Security Council of the United Nations” tarehe 14 Juni 2023 limejadili pamoja na mambo mengine hoja kutoka katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuhusu: "Maadili ya Udugu wa Kibinadamu Katika Kukuza na Kudumisha Amani" chini ya "Matengenezo ya ajenda ya kimataifa ya amani na usalama”. Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE Noura bint Mohammed Al Kaabi ameongoza mkutano huo. Wengine walioshiriki ni pamoja na: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres; Sheikh Ahmed Muhammed Ahmed Aṭ-Ṭayyeb, Imamu Mkuu wa Al-Azhar; pamoja na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amesoma hotuba iliyoandaliwa na Baba Mtakatifu. Katika hotuba hii, Baba Mtakatifu amekazia mambo yafuatayo: Dhamana na wajibu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; Utandawazi unaokumbana na ukame wa udugu wa kibinadamu; ndoto kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu ni amani inayojengwa katika sadaka, majadiliano na diplomasia na kumwilishwa katika udugu wa kibinadamu na kamwe amani haiwezi kuelea kwenye ombwe! Dhamana na wajibu mkuu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kulinda usalama na kudumisha amani kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Katiba ya Umoja wa Mataifa italindwa na kuheshimiwa kwa kuzingatia msingi wa ukweli na uwazi katika utekelezaji wa maamuzi yake ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka.

Jumuiya ya Kimataifa ina kiu ya haki na udugu wa kibinadamu
Jumuiya ya Kimataifa ina kiu ya haki na udugu wa kibinadamu

Utandawazi umeiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuwa karibu sana, lakini inateseka kutokana na ukosefu wa udugu wa kibinadamu unaoathirika kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa haki na usawa, umaskini pamoja na ukosefu wa utamaduni wa mshikamano. Na matokeo yake ni kuibuka kwa mifumo mipya ya kiitikadi inayosambaza, uchoyo na ubinafsi; ulaji wa kupindukia unaodhohofisha mafungamano ya kijamii. Na kibaya zaidi ni ukame wa udugu wa kibinadamu unaodhohofishwa na kinzani, mipasuko ya kijamii na vita inayoendelea kupamba moto sehemu mbalimbali za dunia, kiasi cha kudhani kwamba, binadamu hajajifunza vyema kuhusiana na madhara ya Vita Kuu ya Dunia na matokeo yake ni kuibuka kwa kasi dhana ya utaifa isiyokuwa na mashiko inayochochea kinzani na migogoro ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ndoto kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu ni amani, lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, binadamu anapendelea zaidi vita kuliko amani kwani vita inawanufaisha watu wachache ndani ya jamii kwa gharama ya familia kubwa ya binadamu. Fedha inayotokana na biashara haramu ya silaha duniani inanuka damu ya watu wasiokuwa na hatia na inachochea mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha. Inachukua muda na ujasiri kujenga mazingira ya watu kukutana na kujadiliana, kwa ajili ya kujenga na kudumisha amani.

Ndoto kubwa ya Mungu ni amani duniani.
Ndoto kubwa ya Mungu ni amani duniani.

Hii ni changamoto ya kuondokana na “dhana ya vita ya haki” ambayo imepitwa na wakati kwa sababu madhara ya vita ni makubwa, kumbe huu ni wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kukataa kishawishi cha kuingia vitani na hivyo kujizatiti katika ujenzi wa amani inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, sadaka, majadiliano na diplomasia pamoja na ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza kilio cha watu wanaoteseka kutokana na vita, hususan watoto wadogo kwani machozi yao yanatoa hukumu na kwamba, kesho yao inayoandaliwa sasa inatokana na maamuzi yanayotekelezwa kwa wakati huu. Amani ni jambo linalowezekana ikiwa kama, binadamu atatia nia ya kuitafuta kwa njia ya kufikiri na wala si katika vionjo; amani itafutwe katika mapana yake na wala si katika uchoyo na ubinafsi na kwamba, amani ni tendo endelevu linalosimikwa katika haki; na kwamba, amani thabiti inasimikwa katika sababu za kimaadili na utu wema kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, bado kuna fursa ya kuandika ukurasa mpya wa amani inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu ambao kamwe hauwezi kubaki unaelea katika ombwe, kwa sababu udugu huu ni muhimu kwa binadamu kwa sababu binadamu kimsingi ni kiumbe jamii na hivyo inawezekana kabisa kujenga jamii inayosimikwa katika haki na amani ya kudumu. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya Kanisa Katoliki anapenda kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika kutafuta na kudumisha amani duniani, ili kweli Jumuiya ya Kimataifa iweze kujikita katika huduma kwa ajili ya amani ili kuragibisha udugu wa kibinadamu na amani duniani kwani ni “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt 5:9.

Baraza la Usalama

 

15 June 2023, 15:27