Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli: Chombo cha Huruma, Faraja na Upatanisho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika maadhimisho ya Sikukuuu ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda, tarehe 3 Juni 2023, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amemweka wakfu Monsinyo Diego Giovanni Ravelli, kuwa Askofu mkuu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tukio ambalo limehudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amemtaka Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli kuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho, kuwatia shime wanaoteseka na kuhangaika katika maisha; awe kwao ni faraja na hivyo kuwasaidia waamini kukutana na Kristo Mfufuka kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kardinali Parolin ameshirikiana na Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa pamoja na Askofu Guido Marini wa Jimbo Katoliki la Tortona, nchini Italia, wote hawa ni viongozi wa Kanisa ambao Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli amefanya nao utume mjini Vatican. Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli ametakiwa kuwa ni chombo cha neema na baraka, faraja na upatanisho katika ulimwengu mamboleo wenye changamoto nyingi. Licha ya mambo yote haya, bado kila siku kuna jumuiya ya waamini wanaokusanyika kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, huku wakitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mahali ambapo, tangu tarehe 11 Oktoba 2021 pamekuwa ni eneo lake la utume kama Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa na hata baada ya kuwekwa wakfu, ataendelea na utume wake kama Mshereheshaji mkuu wa Liturujia za Kipapa. Kumbe ni wajibu wake kuwasaidia na kuwaongoza waamini ili kuadhimisha vyema Fumbo la Pasaka, ili hatimaye, waweze kukutana na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli ameteuliwa na Mwenyezi Mungu, kielelezo cha upendo wake usiokuwa na mfano, ili aweze kuwa ni sadaka na kwamba, wito huu anapaswa kuuchukulia kama zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayoiishi kwa amani na utulivu wa ndani. Aendelee kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, anatumwa kuendelea kuwa mcheshi katika huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kuendelea kupyaisha imani na udumifu katika maisha na wito wake; kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya Neno, Sakramenti, Matendo ya huruma na Maisha ya sala. Ajitahidi kuwa ni mchungaji mwema, tayari kusadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, awe ni mhudumu kweli kweli atakayewasaidia waamini kwa njia ya utume na maisha yake, kukutana na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.
Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli amechagua maneno ya “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” kuwa ni kauli mbiu yake ya Kiaskofu. Hii ni furaha ya kukutana na Kristo Yesu na hivyo kuwa ni mfuasi wake amini, chombo makini cha faraja na huruma yake isiyokuwa na kipimo. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, furaha hii inaendelea kukua na kukomaa licha ya matatizo, changamoto na fursa mbalimbali anazoweza kukutana nazo katika maisha na utume wake. Kumbe, Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli anaitwa kuiishi Injili inayosimikwa katika ushuhuda na upendo. Na Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli kwa upande wake, amewaomba watu wa Mungu wamsindikize katika maisha na utume wake kwa sala, ili kutunza ndani mwake hii zawadi kubwa ya kuwekwa wakfu kama Askofu mkuu.
Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli alizaliwa tarehe Mosi Novemba 1965 huko Lazzate nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 15 Juni 1991 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na kuhamia Jimbo Katoliki la Velletri-Segni. Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Afisa mwandamizi, Idara ya Mtunza Sadaka ya Kipapa. Baadaye alijiendeleza zaidi katika masomo na hatimaye, kujipatia Shahada ya uzamili katika Mbinu za Ufundishaji kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian, Roma. Waswahili wanasema, elimu ni bahari na wala haina mwisho, Askofu mkuu Diego Giovanni Ravelli alijiendeleza zaidi katika Liturujia ya Kanisa na hatimaye kujipatia Shahada ya Uzamivu kutoka Taasisi ya Kipapa ya Liturujia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmi kilichoko mjini Roma. Tarehe 25 Februari 2006 akateuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa Mshereheshaji Mkuu wa Liturujia za Kipapa. Tarehe 12 Oktoba 2013 akateuliwa kuwa Afisa Mwandamizi Idara ya Mtunza Sadaka ya Kipapa. Tarehe 11 Oktoba 2021, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Mshereheshaji mkuu wa Liturujia za Kipapa na Mratibu mkuu wa Kwaya ya Kipapa (Cappella Musicale Pontificia). Na hatimaye, tarehe 21 Aprili 2023, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu na ataendelea na utume wake kama Mshereheshaji mkuu wa Liturujia za Kipapa na Mratibu mkuu wa Kwaya ya Kipapa (Cappella Musicale Pontificia.)