Tafuta

Mtakatifu Paulo VI hapo tarehe 25 Julai 1968 takribani miaka 55 iliyopita alichapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae”  yaani "Maisha ya Binadamu." Mtakatifu Paulo VI hapo tarehe 25 Julai 1968 takribani miaka 55 iliyopita alichapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani "Maisha ya Binadamu." 

Waraka wa Mtakatifu Paulo VI: Humanae Vitae! Maisha ya Binadamu: Unabii!

Ni Waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Papa Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI hapo tarehe 25 Julai 1968 takribani miaka 55 iliyopita alichapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu.” Ni Waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Papa Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ni kati ya mafundisho mazito ya Papa Paulo VI aliyetangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 14 Oktoba 2018. Anakita mawazo yake katika dhamana na wajibu wa uumbaji, malezi, makuzi na elimu ya watoto. Wanandoa wanapaswa kufikiri, kujiandaa kikamilifu, kusindikizana na hatimaye, kupokea mtoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, dhamana inayowawajibisha! Hizi ni changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, zinazotaka waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, sadaka na majitoleo binafsi. Nchi zilizoendelea ziliona kwamba, ongezeko la watu duniani, lilikuwa ni tishio kwa ustawi na maendeleo yao. Kutokana na mantiki hii, wachumi wakawatangazia watu raha, starehe na anasa kwa kufumbata utamaduni wa kifo na matokeo yake, leo hii kuna nchi ambazo zinalia na kuomboleza kutokana na kuwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa kila mwaka pamoja na kuendelea na kuwa na idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa.

Miaka 55 ya Waraka wa Kitume Humanae vitae
Miaka 55 ya Waraka wa Kitume Humanae vitae

Mtakatifu Paulo VI katika Waraka huu wa kitume, alipembua kanuni maadili na Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Akakazia kwa namna ya pekee, wajibu wa wazazi katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha, kwa kuheshimu mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kwa mwelekeo huu, wanandoa wanaweza kuwa kweli waaminifu katika tendo la ndoa na mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kukataa kishawishi cha kukumbatia utamaduni wa kifo, unaofumbatwa katika vitendo vya utoaji na uzuiaji mimba, vinavyowekwa mbele ya macho ya watu wengi kama njia muafaka ya kufurahia maisha na kusahau kwamba, majuto ni mjukuu na baada ya kisa ni mkasa! Ikolojia ya binadamu inapaswa kulindwa na kudumishwa kwa kujikita katika kanuni maadili, utu wema na haki msingi za binadamu! Kanisa linakazia umuhimu wa waamini kuambata kanuni maadili na utu wema; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani tendaji. Kanisa linapenda kuwaona waamini wake wakiwa makini kushuhudia Injili Familia inayoambata Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waraka wa “Maisha ya binadamu” unapaswa sasa kusomwa pia kwa mwanga wa “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Injili ndani ya familia” ambao umechapishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko anayekazia umuhimu wa: Injili ya Familia, Injili ya Uhai, Utu na heshima ya binadamu. Papa Francisko anapembua kuhusu wito wa familia; umuhimu wa upendo ndani ya familia; upendo unaozaa upendo kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana; kwa kuenzi na kudumisha udugu wa kibinadamu na mshikamano. Anakazia umuhimu wa malezi na majiundo makini kwa watoto, bila kusahau changamoto zinazowakabili wanandoa.

Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu
Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu

Huu ni mwono muhimu wa ufahamu wa binadamu unaosimikwa katika upendo na jinsia ya kibinadamu, unaoeleweka kulingana na mpango wa Mungu, ambao miaka 55 baada ya kuchapishwa kwake unaendelea kupendekeza ukweli wa hali ya juu uliokanushwa na miongo kadhaa ya watu waliojikita katika utamaduni wa kifo. Hii ndiyo thamani ya Waraka wa “Humanae vitae, wa Mtakatifu Paulo VI, ukichambuliwa na Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, 19 Mei 2023, katika Agostino, katika ufunguzi wa utafiti wa siku mbili unaohusu waraka huo, ulioandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Maadili ya Kibiolojia ya Jérôme Lejeune. Kwa upande wake, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha, amekazia juu ya kipengele muhimu sana cha mapenzi ya dhati kati ya mume na mke, ili kuendeleza uzazi. Mtakatifu Paulo VI anakazia "sifa" nne za kimsingi za upendo wa ndoa: Upendo kamili wa kibinadamu, Upendo kibinafsi na urafiki", "upendo mwaminifu na wa kipekee hadi kifo", "upendo wenye matunda." Kumbe, kuna haja ya kuendelea kutafakari uhusiano uliopo kati ya tendo la ndoa, upendo ndani ya ndoa na uzazi. Kwa hakika Papa Francisko amerudia kwa usahihi kuhusiana na mada ya vidhibiti mimba, akisema kwamba, wajibu wa wanataalimungu ni kufanya utafiti na kutafakari kitaalimungu, bila ya kujiwekea vikwazo, kwani ni wajibu wa Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kutoa msimamo wa Mama Kanisa.

Paulo Vi Humanae vitae
20 May 2023, 16:15