Tafuta

“Akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.” “Akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.”   (Vatican Media)

Papa Francisko: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Nendeni Ulimwenguni Kote Mkatangaze Injili

Mama Kanisa, tarehe 18 Mei 2023 linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ingawa kutokana na sababu za kichungaji, Sherehe hii itaadhimishwa rasmi, Jumapili tarehe 21 Mei 2023 sanjari na Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni ambayo kwa Mwaka 2023 inayonogeshwa na kauli mbiu “Kuongea Kutoka Moyoni, “Kadiri ya Ukweli na Upendo” Efe 4:14. Akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa katika Kanuni ya Imani anasadiki na kufundisha kwamba, “Akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 17 Mei 2023, amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa, tarehe 18 Mei 2023 linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ingawa kutokana na sababu za kichungaji, Sherehe hii itaadhimishwa rasmi, Jumapili tarehe 21 Mei 2023 sanjari na Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni ambayo kwa Mwaka 2023 inayonogeshwa na kauli mbiu “Kuongea Kutoka Moyoni, “Kadiri ya Ukweli na Upendo” Efe 4:14. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa mawasiliano ya moyo kwa moyo, ili kuzungumza vyema na kupenda vyema; umuhimu wa kuzungumza kwa moyo kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi sanjari na kuondoa chuki na uhasama ili kuragibisha lugha ya amani. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa sala ifuatayo: Bwana Yesu, Neno safi lililomiminwa kutoka moyoni mwa Baba wa milele, atusaidie kufanya mawasiliano yetu kuwa wazi, bayana zaidi na ya kutoka moyoni. Bwana Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, atusaidie kusikiliza mapigo ya mioyo, tujitambue tena kama ndugu wamoja, na hivyo kuondoa uhasama na chuki inayowagawa wanadamu. Huu ni wakati muafaka kwa waamini kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho haya na kwamba, anawaombea amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu Mfufuka. Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia mambo ya juu na kamwe wasiridhike na mambo ya dunia, kwani haya yanapita kama “upepo wa kisulisuli”.

Tangazeni na kushuhudia Injili ya Kristo katika maisha yenu
Tangazeni na kushuhudia Injili ya Kristo katika maisha yenu

Roho wa Kristo Mfufuka awasaidie waamini kung’amua na hatimaye, kusoma alama za nyakati, ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili kwa uaminifu na kwa furaha katika medani mbalimbali za maisha, daima wakijitahidi kuwa ni wajenzi wa udugu wa kibinadamu. Ni wakati muafaka wa kuangalia matukio muhimu kabla ya Kristo Yesu kupaa mbinguni, kwani, anawaachia wafuasi wake wosia akisema “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt 28:19-20. Huu ni ujumbe makini kwa vijana kujizatiti katika utume wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mataifa. Wazee na wagonjwa hata katika mahangaiko yao, watambue kwamba, wanayo nafasi muhimu sana katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu ulimwenguni. Na kwa wanandoa wapya watengeneze mazingira katika familia zao, ili ziwe ni mahali pa kujifunza kumpenda Mwenyezi Mungu, daima wakijitahidi kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili. Waamini wapokee na kujitahidi kumwilisha wito wa umisionari unaofumbatwa katika ushuhuda, kwa kuendelea kuungana na Kristo Yesu katika maisha ya: Sala, Sakramenti na Huduma ya huruma na upendo kwa jirani. Kwa namna ya pekee, amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Ukraine, wanaoendelea kuteseka kutokana na vita.

Kupaa Bwana Mbinguni
18 May 2023, 17:31