Papa Francisko: Pyaisheni Ibada kwa Bikira Maria! Salini Rozari
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 3 Mei 2023 amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupyaisha Ibada ya Rozari Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria. Wajitahidi kupenya katika undani wa mafumbo ya maisha ya Bikira Maria, ili hatimaye, waweze kumpokea kama Mama yao wa Maisha ya kiroho, kielelezo na mfano wa uaminifu kwa Kristo Yesu. Waamini wamkimbilie kumwomba, ili aweze kuwaombea udumifu katika imani, umoja, ushirikiano na amani na hatimaye, aweze kuwakinga na hatari zote za roho na za mwili, tayari kushiriki katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu na heshima kwa kazi ya uumbaji. Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya ufunuo wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu na ukombozi kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Mwezi Mei ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, silaha za pambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo ni: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti ya Upatanisho pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Anawataka waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Baba Mtakatifu katika sala yake anasema, Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia wa Rozari Takatifu, amebarikiwa kuliko wanawake wote, ni sura ya Kanisa iliyovishwa mwanga wa Pasaka; Yeye ni heshima ya watu wa Mungu; mshindi dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo!
Bikira Maria ni shuhuda wa unabii wa upendo wa huruma ya Mungu; mwalimu mahiri wa Habari Njema ya Mwana wa Mungu, alama ya moto wa Roho Mtakatifu. Huku bondeni kwenye furaha na machozi, Bikira Maria awafundishe watoto wake ukweli wa milele ambao Baba wa milele, anapenda kuwafunulia wadogo. Bikira Maria awaoneshe ulinzi na tunza ya mkono wenye nguvu! Moyo wake usiokuwa na doa uwe ni kimbilio la wadhambi, njia inayowaelekeza kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na ndugu zake wote katika imani, matumaini na mapendo, wanajiaminisha kwa Bikira Maria na kujiweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu, ili kumtolea Mungu sifa na utukufu, milele yote! Baba Mtakatifu anapenda kuwakabidhi watu wote kwa Kristo Yesu, lakini zaidi wale wenye shida na mahangaiko makubwa. Bikira Maria Mama wa faraja awaombee baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu wale: wasiopendwa; waliotengwa na kusukumiziwa pembezoni mwa jamii; wale wote wanaopokwa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi; yatima na wale wote walionyimwa haki zao msingi! Anawaombea baraka ya Mwenyezi Mungu iliyomwilishwa katika Kristo Yesu, iweze kuwalinda; Mwenyezi Mungu aweze kuwaangazia nuru za uso wake na kuwafadhili; awainulie uso wake na kuwapatia amani. Baba Mtakatifu anasema, baraka hii imepata utimilifu wake ndani ya Bikira Maria aliyebahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; Uso wa huruma ya Baba wa milele ambao waamini wanautafakari katika Matendo ya Rozari Takatifu na kwamba, kwa njia ya Kristo Yesu na Bikira Maria, waamini wanaweza kuendelea kubaki wakiwa ndani ya Mwenyezi Mungu. Ili kuwa Wakristo, kweli, waamini hawana budi kuwa na Ibada kwa Bikira Maria, kwa kutambua mambo msingi yanayounganisha maisha ya Bikira Maria na Kristo Yesu. Kwa kusali Rozari Takatifu, Injili ya Kristo inaendelea kutangazwa na kumwilishwa katika maisha, watu, familia na katika ulimwengu mzima!
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija pamoja na Bikira Maria, Mwalimu mkuu katika maisha ya kiroho, aliyethubutu kumfuasa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba, akabarikiwa kwa kuwa aliamini! Anawaonya waamini kutomkimbilia Bikira Maria kwa kutaka awafanyie miujiza ya “chapuchapu”, kwani Bikira Maria wa Injili anayeheshimiwa na Kanisa ni yule anayeangalia mambo msingi, anayewaombea watoto wake huruma ya Mungu ili hatimaye, kukutana na Hakimu mwenye haki, yaani Mwana kondoo wa Mungu aliyechinjwa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu! Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo anasema Baba Mtakatifu, mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu badala ya kuogopa hukumu yake kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu kamwe haiwezi kuondoa haki! Yesu aliteswa na kufa Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la utumwa wa dhambi na mauti. Kwa njia ya imani inayowaunganisha katika Msalaba wa Kristo, wamekombolea na hivyo kuwekwa huru, kumbe, hakuna sababu ya kuwa na woga, bali kukimbilia na kuambata upendo wake. Bikira Maria ni kielelezo cha mapinduzi ya wema na upendo wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria anaonesha kwamba unyenyekevu na upole si fadhila ya wanyonge bali ni fadhila ya watu wenye nguvu ambao hawana sababu ya kuwatendea wengine ubaya ili kuonekana kuwa ni watu wa maana sana. Mwingiliano wa haki na upole, wa taamuli na kujali mahitaji ya wengine ndiyo inayolifanya Kanisa limtazame Bikira Maria kama mfano bora wa uinjilishaji. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wote kuiga mfano wa Bikira Maria, ili waweze kuwa ni alama na Sakramenti ya huruma ya Mungu anayesamehe yote! Kwa kushikamana na Bikira Maria, wote wanaweza kuimba huruma ya Mungu kwani ni huruma ambayo amewakirimia watakatifu na watu wake waaminifu na kwa njia yao huruma hii imeweza kuwafikia wengine wote. Kwa njia ya kiburi cha binadamu na uchu wa malimwengu, binadamu ameshindwa kutimiza hamu ya moyo wake! Njia pekee ya kuweza kuinuka tena ni kwa njia ya Bikira Maria kumshika mkono na kumfunika kwa joho ili kumweka pembeni wa Moyo wake usiokuwa na doa!