Papa Francisko: Mahubiri Sherehe ya Pentekoste Kwa Mwaka 2023
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kanuni ya Imani: Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Hii ni sehemu ya Kanuni ya Imani. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima ni kipengele kinachofafanua asili ya Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anayetenda kazi zake kwa njia ya: Imani, Neno, Sakramenti na Sala za Kanisa. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini uzima unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Na anatenda kazi zake katika kazi ya uumbaji, ndani ya Kanisa na katika nyoyo za waamini. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa na Siku ya Waamini Walei wanapoitwa kwa namna ya pekee kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao, Dominika tarehe 28 Mei 2023 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kuhusu kazi za Roho Mtakatifu: Roho Mtakatifu ni Muumbaji; Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani ya Kanisa, kwa kuwashukia Mitume na hivyo kuwagawia karama na mapaji yake yanayopaswa kutumika katika utulivu, ili ndani ya Kanisa, karama na mapaji haya yaweze kutumika vizuri zaidi. Roho Mtakatifu ni zawadi maalum kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, ni zawadi ya upatanisho, amani na utulivu wa ndani kwa wale wote waliovunjika na kupondeka moyo.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Roho Mtakatifu ndiye anayeratibisha mambo yote na kuyaweka katika mpangilio wake, yaani kutoka katika vurugu na kuyarejeshea amani na utulivu wake wa asili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Roho wa Mungu ambaye, kwa maongozi ya ajabu, huongoza mwenendo wa nyakati na kutengeneza upya uso wa dunia, anasimamia maendeleo hayo. Rej. GS, 26. Roho Mtakatifu anapyaisha uso wa dunia bila kubadili ukweli wa mambo, kwani anaukirimia utulivu kwa sababu Roho Mtakatifu ni chemchemi ya utulivu: Ipse harmonia est! Leo hii kuna vurugu na migawanyiko, hali ya kutoelewana pamoja na kukandamizwa na upweke hasi. Kuna vita, kinzani na migogoro mbalimbali, kazi ya Shetani, Ibilisi, baba wa kinzani na mipasuko ya kijamii, ndiye audanganyae ulimwengu wote, anafurahia ukosefu wa haki, kumbe nguvu za binadamu hazifai kitu ili kurejesha amani na utulivu. Ni katika muktadha huu, baada ya Sherehe ya Pasaka, Kristo Yesu anamtuma Roho Mtakatifu, Roho wa umoja na amani, mwaliko kwa waamini ni kuendelea kumwomba kila siku ya maisha. Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani ya Kanisa, kwa kuwashukia Mitume na hivyo kuwagawia karama na mapaji yake yanayopaswa kutumika katika utulivu, ili ndani ya Kanisa, karama na mapaji haya yaweze kutumika vizuri zaidi. Roho Mtakatifu anapowashukia Mitume wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka: Roho Mtakatifu hafuti zile tofauti wala tamaduni zao, bali anawajalia wote kujazwa na Roho Mtakatifu, mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika fadhila ya upendo. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yule yule anasema Mtakatifu Paulo, kwa maana Wakristo wote wamebatizwa katika Roho mmoja na hivyo kuwa ni mwili mmoja. Rej. 1Kor 12:4.13. Roho Mtakatifu anawaongoza waamini kutambuana kuwa ni ndugu wamoja na hii pia ndiyo njia anayowaonesha kuifuata!
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume”, hii ni safari ya maisha ya kiroho kadiri ya Roho Mtakatifu, fursa makini ya kujenga utamaduni wa kumsikiliza Roho Mtakatifu, kwani katika shida na magumu ya historia ya Kanisa, Roho Mtakatifu ndiye nguzo na moyo wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, chachu makini ya uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji. Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa ndiye anayetoa maana ya imani, maadili na shughuli za kitume, vinginevyo mambo yote haya yangekuwa ni mafundisho yasiokuwa na msingi, wajibu na shughuli za kichungaji zingekuwa ni kazi kama zilivyo kazi nyinginezo. Ni katika Roho Mtakatifu imani inakuwa ni sehemu ya maisha, upendo wa Mungu unatawala na matumaini yanazaliwa upya. Roho Mtakatifu awe ni kiini cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, na anao umuhimu wa pekee katika ulimwengu mamboleo, kumbe waamini wanapaswa kumwita kila siku wakisema, “Njoo Roho Mtakatifu.” Huu ni mwaliko kwa waamini kutembea katika mshikamanano, kwani Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa Siku ile ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja, ndiyo njia pekee ya kuadhimisha Sinodi na kuendelea kulipyaisha Kanisa, huku Roho Mtakatifu akipewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa kanisa kwa ajili ya ujenzi wa amani na utulivu ndani ya Kanisa.
Roho Mtakatifu ni zawadi maalum kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, ni zawadi ya upatanisho, amani na utulivu wa ndani kwa wale wote waliovunjika na kupondeka moyo; wanaoelemewa na mzigo wa dhambi na ubaya wa moyo; Roho Mtakatifu anawakirimia utulivu wa ndani wale wote wanaojitahidi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa na Mwenyezi Mungu. Kumbe, huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini kumwita Roho Mtakatifu, kuanza siku kwa kumwomba, ili hatimaye, waamini waweze kuwa ni wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana ni chemchemi ya amani na utulivu wa ndani, Kanisa linapenda kuwaaminisha walimwengu nchini ya ulinzi wa Roho Mtakatifu pamoja na kuliweka wakfu Kanisa na nyoyo za waamini. Uje Roho Mtakatifu uzienee nyoyo za waamini wako, washa moto wa mapendo yako, peleka Roho wako, vitaumbwa upya na sura ya ulimwengu itageuka. Njoo zawadi ya zawadi, amani na utulivu wa Kanisa, ulijalie Kanisa lako umoja katika Roho Mtakatifu. Njoo Roho Mtakatifu chemchemi ya msamaha, amani na utulivu wa moyo, wageuze waja wako kwa njia ya Bikira Maria.