Papa Francisko Utengenezaji wa Silaha za Nyuklia ni Kinyume cha Ujenzi wa Haki na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mkutano wa kilele wa Hiroshima kuanzia tarehe 19-21 Mei 2023 ni fursa kwa viongozi wa mataifa saba tajiri duniani, G7 kuonesha azma yao thabiti ya kudumisha utaratibu wa kimataifa unaozingatia utawala wa sheria, na kuimarisha mawasiliano yao na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Masuala makuu ambayo yameshughulikiwa wakati wa vikao vinane vya kazi ni: uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Mengine ni: Ustahimilivu wa Kiuchumi na Usalama wa Kiuchumi, Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unaolenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Hii inatokana na ukweli kwamba, amani ya kweli inajengwa kwa njia ya majadiliano na mshikamano. Maeneo kama vile: Jinsia, Haki za Binadamu, Ulimwengu wa kidigitali, Sayansi na Teknolojia pia yamechambuliwa. Viongozi wa G7, wamethibitisha dhamira yao ya kusimama pamoja dhidi ya vita haramu, visivyo na uhalali vinavyochochewa na Urusi dhidi ya Ukraine. Wamelaani kwa maneno makali, ukiukaji wa wazi wa Urusi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) na athari za vita vya Urusi kwa ulimwengu wote. Miezi 15 ya uchokozi wa Urusi umegharimu maelfu ya maisha, umesababisha mateso makali kwa wananchi wa Ukraine, na hivyo kuhatarisha upatikanaji wa chakula na nishati kwa watu wengi walio hatarini zaidi ulimwenguni. Wanatoa pole zao kamili na rambirambi kwa watu wa Ukrain kwa hasara na mateso yao. Viongozi wa G7 wamewasalimia watu wa Ukraine kwa upinzani wao wa kijasiri. Msaada wao kwa Ukraine hautayumba na wala hawatachoka katika kujitolea ili kupunguza athari za vitendo haramu vya Urusi kwa ulimwengu wote.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019, iliyonogeshwa na kauli mbiu: “Linda Maisha Yote”: Ujumbe unaoitaka familia ya Mungu katika ujumla wake, kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha, anasema, ili kuweza kuwa na amani ya kudumu, kuna haja kwa watu wote kuweka silaha zao chini, lakini zaidi zile silaha ya maangamizi. Hizi silaha za nyuklia zinazoweza kuleta maafa makubwa zaidi kwa miji na nchi mbalimbali duniani. Kwa mara nyingine Baba Mtakatifu anasema bila kupepesapepesa macho kwamba: utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema. Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, unalenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Ni katika muktadha wa Mkutano wa kilele wa Hiroshima kuanzia tarehe 19-21 Mei 2023 wa viongozi wa mataifa saba tajiri duniani, G7, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Askofu Alexis-Mitsuru Shirahama wa Jimbo Katoliki la Hiroshima, kama mwenyeji wa mkutano wa G7, akikumbuka hija yake ya Kitume aliyoifanya nchini Japan Mwezi Novemba 2019.
Baba Mtakatifu anakaza kusema utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema pamoja na ustawi wa mazingira bora nyumba ya wote. Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, vita na migogoro ya kijamii inayoendelea kuibuka sehemu mbalimbali za dunia, bila kusahau vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi. Uzoefu unaonesha kwamba, ni kwa njia ya ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, ulimwengu unaweza kuponya madonda hayo na kujielekeza katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika haki na amani. Katika mapambazuko ya Karne ya Ishirini na moja utafutaji wa amani unahusianishwa na hitaji la usalama na tafakari ya kina, itakayowezesha uwepo wa amani, kwa kuhakikisha kwamba usalama wa Jumuiya ya Kimataifa hauna budi kwenda sanjari na uhakika wa usalama wa chakula na maji safi na salama; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, huduma za afya, utunzaji wa vyanzo vya nishati pamoja na ugawaji bora wa rasilimali za dunia. Usalama wa Jumuiya ya Kimataifa unahitaji mshikamano na mafungamano Kimataifa kati ya serikali na na wadau wengine ili kuwa na mwelekeo unaowajibisha sanjari na ushirikiano wa Kimataifa. Hiroshima kama kielelezo cha kumbukumbu hai, unaonesha jinsi ambavyo silaha za nyuklia zilivyo tishio kwa amani na kwamba, kuna haja ya kuwa na uhakika wa amani Kitaifa na Kimataifa.
Jumuiya ya Kimataifa itazame na kutafakari kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia na matumizi mabaya ya rasimali watu na kiuchumi, kumbe, kinachohitajika ni ile hali ya kuaminiana na majadiliano katika ukweli na uwazi. Jumuiya ya Kimataifa haipaswi kudharau athari za hali ya kuendelea kwa hofu na mashaka na umiliki wao unahatarisha ukuaji wa hali ya kuaminiana na majadiliano. Katika muktadha huu, silaha za nyuklia na silaha zingine za maangamizi makubwa zinawakilisha hatari inayozidisha ambayo inatoa udanganyifu tu wa amani. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko katika kuombea Mkutano wa kilele wa G7 huko Hiroshima ametaka uoneshe maono ya kuona mbali katika kuweka misingi ya amani ya kudumu na usalama thabiti na wa muda mrefu. Anamshukuru Askofu Alexis-Mitsuru Shirahama wa Jimbo Katoliki la Hiroshima, kwa juhudi zake katika huduma ya haki na amani na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume kwa moyo mkunjufu.