Papa Francisko atatoa tuzo ya kimataifa ya Paul VI kwa Rais Mattarella
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Jumatatu tarehe 29 Mei 2023, katika siku ambayo inaadhimishwa miaka 60 ya kuchaguliwa kwa Papa Paulo VI (Giovanni Battista Montini), Rais wa Jamhuri ya Italia Bwana Sergio Mattarella atapokea Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI kutoka mikononi mwa Baba Mtakatifu Francisko. Utoaji wa utambuzi huo utafanyika katika Ukumbi wa Clementina wa Jumba la Kitume Vatican. Tuzo hiyo ilianzishwa kwa mpango wa Taasisi ya Paulo VI ili kuweza kumulika na kuwatunuku watu mashuhuri ambao wamejitofautisha katika nyanja mbali mbali za kiutamaduni na katika kukuza kuishi kwa haki kwa wanadamu na, kwa njia tofauti, kushuhudia uhai wa ulimwengu, na urithi wa kiroho wa Papa Montini.
Kamati ya Kisayansi
Kamati ya Kisayansi na Kamati Tendaji imeamua kumtunuku kwa hiyo Rais Mattarella kwa kujitolea kwake kwa manufaa ya wote katika dhamira ya kisiasa inayochochewa na maadili ya Kikristo na wakati huo huo, kwa bidii katika utumishi wa taasisi za kiraia. Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika Taasisi ya Paulo VI inasomeka kuwa “Kwa Rais Sergio Mattarella inawezekana kutambua urithi wa utamaduni mkubwa wa wanasiasa wa Kikatoliki, ambao walifikiri na kuchangia kuunda Umoja wa Ulaya kama nafasi ya kuishi kwa amani na kidemokrasia kati ya watu.
Historia ya tuzo
Taasisi ya Paulo VI ilianzishwa siku moja baada ya kifo cha Papa Montini kwa mpango wa Kazi kwa ajili ya Elimu ya Kikristo ya Brescia Jimbo ambalo papa wa 262 alizaliwa na kuhitimu masomo yake ya kwanza, kama Kituo cha mafunzo na kumbukumbu juu ya Kanisa kuhusu sura, takwimu, kazi na mafundisho ya Giovanni Battista Montini yaani Papa Paulo VI. Kati ya malengo yake ni pamoja na kuunda maktaba maalum, kumbukumbu, uhamadishaji wa mikutano ya mafunzo na machapisho ya mada. Hii ni Tuzo la Kimataifa la Paulo VI, kwa heshima ya kumbukumbu ya Baba Mtakatifu Montini aliyehisi kwa undani mahangaiko na matumaini ya binadamu wa kisasa, akijitahidi kujua na kuelewa mang’amuzi yao ili kuwarejesha katika makabiliano yenye mwanga na suluhu ya ujumbe wa Kikristo, kwa kuunganisha mwelekeo wa kidini na kiutamaduni wa utu wa papa.
Tangu kuanza kwa toleo la tuzo
Kwa hiyo Tuzo hiyo ilitolewa kwa mara ya kwanza mnamo 1984 kwa Hans Urs von Balthasar kwa masomo yake ya kitaalimungu na ilitunukiwa na Papa Mtakatifu Yohane Paulo II. Kisha alitunukiwa mnamo mwaka wa 1988, Olivier Messiaen kwa muziki, mwaka wa 1993 Oscar Cullmann kwa uekumeni, mwaka wa 2003 Paul Ricoeur kwa falsafa na mwaka wa 2009 mfululizo wa ‘Sources Chrétiennes” yaani “Vyanzo Ukristo kwa ajili ya elimu.
Mahali pa kuzaliwa kwa Papa Montini
Makao makuu ya Taasisi ya Paul oVI iko huko Concesio, karibu na mahali pa kuzaliwa kwa Giovanni Battista Montini, ambayo imekuwa mahali pa hija. Inatunza na watawa wa Shirika la Mabinti wa Maria Msaada wa Wakristo, wanaoishi karibu na nyumba, ambayo pia inashirikiana katika shughuli za Taasisi. Ni watawa wa Kisalesia ambao huwakaribisha wageni na kuwaongoza. Tangu 2014, ratiba imeandaliwa kwa ajili ya kutembelea nyumba hiyo ambayo inafikiwa na mahujaji 10,000 kwa mwaka. Taasisi huandaa mipango mbalimbali kwa mapadre, waseminari, wanafunzi, kwa ajili ya shule na kukaribisha mikutano ya makundi mbalimbali ya kikanisa.