Papa Francisko Asikitishwa na Mauaji ya Watoto wa Shule ya Msingi Belgrade
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mauaji yaliyotokea hivi karibuni katika shule ya Msingi Vladislav Ribnikar na Mladenovac huko Belgrade. Katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Ladislav Német wa Jimbo kuu la Belgrade na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Kimataifa la Watakatifu Cyril na Methodi, Belgrade, anamwomba, amfikishie salam zake za rambirambi kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito.
Baba Mtakatifu anakaza kusema hivi ni vitendo vya ukatili na kwamba, anapenda kuungana na wale wote wanaowaombolezea watoto wao waliouwawa kinyama. Anapenda kuwaweka chini huruma na upendo wa Kristo Yesu Mfufuka. Anawaombea faraja na nguvu ya Roho Mtakatifu, ili waweze kuimarika katika imani, matumaini na mapendo. Mwishoni, amewapatia wote baraka zake za kitume. Kijana mwenye umri wa miaka 21 hivi karibuni amewafyatulia risasi wanafunzi wa shule ya msingi na hivyo kupelekea vifo vya wanafunzi nane wa shule ya msingi na wengine saba kujeruhiwa. Inasadikiwa kwamba, kijana huyu alipanga mauaji haya kwa muda mrefu.