Tafuta

2023.05.20 Partecipanti al Capitolo Generale della Compagnia di Maria 2023.05.20 Partecipanti al Capitolo Generale della Compagnia di Maria  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko Akutana na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Monfortani: Ushuhuda wa Ukarimu

Kuna changamoto za kichungaji zinazojikita katika uchoyo na ubinafsi, kutopea kwa imani, ulaji wa kupindukia na unyonyaji wa maskini. Ili kuweza kukabiliana na changamoto kama hizi, Mtakatifu Luigi Maria Grignion de Montfort alianzisha programu ya maisha iliyojikita katika kutafuta, kutafakari na kutumia hekima ya moyoni ili kupambana na hekima potofu, kwa msaada na kwa kuiga mfano wa Bikira Maria. Papa amekazia: ukarimu, mwelekeo wa kimataifa na huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa 38 wa Shirika la Wamisionari wa Monfortani, tarehe 23 Mei 2023 wamemchagua Mheshimiwa Padre Yoseph Putra Dwi Darma WATUN, SMM, kuwa mkuu wa 23 wa Shirika la Monfortani. Mkutano mkuu wa 38 unanogeshwa na kauli mbiu “Kuthubutu kuchukua hatari kwa Mungu kwa mwanadamu; Uaminifu wetu wa ubunifu.” Hii ni kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka kwa Mtakatifu Luigi Maria Grignion de Montfort aliyetangazwa hivi karibuni kuwa Mtakatifu na Muasisi wa Shirika. Shirika lilianzishwa wakati ambapo kulikuwa na changamoto pevu ya kiimani, Mtakatifu Luigi Maria Grignion de Montfort akatoa kipaumbele cha kwanza kwa hekima ya Kimungu itawale ndani mwake na kuendelea kujikita katika ubunifu, bila woga huku akihubiri upendo wa Mungu na kukoleza Ibada kwa Bikira Maria, hadi kifo chake, huku akiwa na umri wa miaka arobaini tu! Shirika hili linafanya utume wake katika nchi thelathini na tatu, huku wakishirikiana na Ndugu wa Mtakatifu Gabrieli na Mabinti wa Hekima pamoja na Chama cha Waamini Walei. Leo hii kuna changamoto za kichungaji zinazojikita katika uchoyo na ubinafsi, kutopea kwa imani, ulaji wa kupindukia na unyonyaji wa maskini. Ili kuweza kukabiliana na changamoto kama hizi, Mtakatifu Luigi Maria Grignion de Montfort alianzisha programu ya maisha iliyojikita katika kutafuta, kutafakari na kutumia hekima ya moyoni ili kupambana na hekima potofu, kwa msaada na kwa kuiga mfano wa Bikira Maria.

Papa amekazia: ukarimu. mwelekeo wa kimataifa na huruma
Papa amekazia: ukarimu. mwelekeo wa kimataifa na huruma

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 20 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na washiriki wa mkutano mkuu wa 38 wa wa Shirika la Wamisionari wa Monfortani kwa kukazia ukarimu, mwelekeo wa kimataifa na huruma. Maandiko Matakatifu yanamwonesha Bikira Maria aliyekubali kupokea Hekima ya Mungu kwa ujasiri na hatimaye akabadili mwelekeo wa maisha yake, akawa tayari kupokea na kutoa upendo wa kidugu aliokuwa ameupokea mjini Nazareti, Mlimani Kalvari na pale alipokuwa chumba cha juu katika mwanga wa Pasaka ya Kristo Mfufuka. Bikira Maria ni mfano bora wa ukarimu, changamoto na mwaliko kwa wanashirika kufuata na kuiga mfano wa Bikira Maria unaofumbatwa katika kipaji cha ubunifu, tayari kuwapokea na kuwakirimia watu ambao Mwenyezi Mungu anawawekea mbele ya huduma yao. Hili ni Shirika la Kimataifa anasema Baba Mtakatifu lenye watu kutoka katika mataifa na tamaduni mbalimbali zinazohitaji majadiliano. Mwelekeo huu una changamoto zake zinazoliwezesha Shirika kuwa ni Jumuiya ya Kiinjili, zawadi kwa watu wote. Huu ni mwaliko wa kueneza amana na utajiri huu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Ibada kwa Bikira Maria idumishwe
Ibada kwa Bikira Maria idumishwe

Karama mbalimbali zinakuwa na kukomaa miongoni mwa watu wanaojisikia kupendwa na kuthaminiwa, kama watoto wapendwa wa Bikira Maria, mwaliko wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Bikira Maria awe ni mfano bora wa kuigwa, ili hata wao waweze kutenda kwa ujasiri, ubunifu na moyo wa huruma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Wanapaswa kuwa na moyo wa huruma ili kweli waweze kuwa na huruma, kama Mwenyezi Mungu alivyo, yaani ni mwingi wa huruma, upendo na anapenda kuonesha ukaribu wake kwa waja wake. Haya ni mambo wanayopaswa kuyatumia kuchunguzia dhamiri zao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ndio ushuhuda unaotolewa na Padre Olivier Maire, Mmisionari wa Montfort aliyeuwawa na mtu ambaye alikosea kumkaribisha ili kumkirimia makazi na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi. Ukarimu na ujasiri wake ukamgharimu maisha, awe ni mfano bora wa kuigwa. Bado kuna haja ya kuendelea kujifunza kupenda na kukua katika upendo ili hatimaye kukua na kukomaa katika upendo, huruma na ukarimu.

Wanashirika wametakiwa kukuza mwelekeo wa Kimataifa
Wanashirika wametakiwa kukuza mwelekeo wa Kimataifa

Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa tangu awali sana. Hii ni Ibada inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Watakatifu na waungama imani, wakaiendeleza Ibada hii kwa ari na moyo mkuu zaidi, kiasi hata Mababa wa Kanisa kulivalia njuga na kuitangaza kwa ajili ya Kanisa zima. Mtakatifu Yohane Eudes aliyeishi kati ya Mwaka 1601 hadi mwaka 1680 katika tafakari zake, alipenda kuunganisha Moyo Mtakatifu wa Yesu na Moyo Safi wa Bikira Maria, Mama wa Yesu. Kunako mwaka 1668 Ibada hii ikaanza kuadhimishwa nchini Ufaransa. Tarehe 13 Julai 1917, Bikira Maria aliwatokea Watoto wa Fatima, wakati walimwengu walipokuwa wanateseka kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Bikira Maria akawapatia ujumbe wa matumaini uliokuwa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika: toba, wongofu wa ndani pamoja na sala na kwamba, Mwenyezi Mungu daima anatembea katika historia ya maisha ya waja wake, mwaliko kwa waamini ni kumtumainia Kristo Yesu kwani yeye ameushinda ulimwengu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Baba Mtakatifu Francisko ndiyo maana mwaka 2022 aliwaweka walimwengu wote wakfu kwa Moyo Safi wa Bikira Maria. Shirika la Wamisionari wa Monfortani limepewa dhamana ya kuwaweka walimwengu wote wakfu chini ya ulinzi na tunza Bikira Maria na awasaidie kutafuta ujasiri, huku wakiongozwa na kipaji cha ubunifu katika msamaha, majadiliano na ukarimu kwa ajili ya amani ya ulimwengu na binadamu wote.

mkutano mkuu
20 May 2023, 15:17