Papa Francisko Akutana na Vijana Wanaojiandaa Kupokea Kipaimara
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuieneza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu Mfufuka. Sakramenti ya Kipaimara inathibitisha na kuimarisha neema ya Ubatizo. Waamini waliozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu, wakaokolewa kutoka katika dhambi ya mauti, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wanakirimiwa mapaji ya Roho Mtakatifu. Mama Kanisa anawaombea watoto wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili awakirimie Roho Mtakatifu Mfariji. Awape Roho wa hekima na akili; Roho wa ushauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada. Mama Kanisa anawaombea kwa Mwenyezi Mungu ili awajaze Roho wa uchaji kwa njia ya Kristo Yesu!
Matunda ya Sakramenti ya Kipaimara ni kuzamishwa zaidi katika kufanywa waana wapendwa wa Mungu na hivyo kuunganishwa kwa nguvu zaidi na Kristo Yesu. Ni Sakramenti inayoongeza ndani ya waamini vipaji na karama za Roho Mtakatifu na hivyo waamini kukamilishwa zaidi kiungo cha waamini na Kanisa la Kristo Yesu. Waamini wanapata nguvu na ari ya kueneza na kutetea kwa maneno na matendo kama mashuhuda aminifu na wa kweli wa Kristo Yesu, tayari hata kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakristo walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara daima wanakumbushwa na Mama Kanisa kwamba, wamepokea mhuri wa kiroho. Yaani, Roho wa hekima na akili, shauri na nguvu; elimu, ibada na uchaji mtakatifu. Ni dhamana na jukumu la waamini kulinda amana na utajiri huu. Mwenyezi anawatia alama na amewajaza amana yake, Roho Mtakatifu nyoyoni mwao. Rej. KKK 1285-1321.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 20 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na watoto na vijana kutoka Jimbo kuu la Genova, Italia wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara. Amewatakia matembezi mema kwenye Bustani za Vatican, kwani huko kuna mambo mazuri ya kuangalia. Amewaomba wasigombane kati yao kwani hii ni kazi ya Shetani, Ibilisi. Badala yake wajenge mahusiano na mafungamano mema, ili kukuza na kudumisha utu na heshima ya kila mtu. Wajitahidi kuwaheshimu jirani zao kwa kuwatunzia heshima. Wachunge sana ndimi zao. Mwishoni, amewaalika wote kwa pamoja kusali salam Maria na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.