Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni Ni Chemchemi ya Imani na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023, ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa jirani zao kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu. Awe ni mfano bora wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu katika maisha! Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika huduma ya upendo! Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kujenga matumaini, lakini wanapaswa kujiandaa vyema, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya chemchemi ya matumaini kwa vijana wengi. Iwe ni fursa ya kuzungumza na wazee, ili waweze kuwashirikisha mang’amuzi yao. Hii ni sehemu ya ujumbekwa njia ya video kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya vijana wanaojiandaa kwenda nchini Ureno ili kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2023.
Video hii imeandaliwa na Askofu msaidizi Amèrico Manuel Alves Aguiar wa Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno, baada ya mazungumzo yake na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Aprili 2023. Baba Mtakatifu anayaangalia Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa imani na matumaini makubwa, licha ya changamoto za maandalizi sanjari na majukumu yao ya kila siku. Ushiriki mkamilifu wa vijana katika maadhimisho haya ni jambo jema sana, mwaliko kwa vijana kujiandaa kushiriki tukio hili la furaha katika maisha yao; jambo la msingi ni kuzamisha matumaini yao katika maadhimisho haya, kwani hapa ni mahali panapowawezesha vijana kukua na kukomaa! Ni siku ambazo matukio mbalimbali yanaacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za vijana; kwa kujenga mahusiano na mafungamano na vijana kutoka katika nchi mbalimbali duniani; lakini cha msingi zaidi ni kuona na kushuhudia nguvu ya vijana wa kizazi kipya. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu vijana ni nguvu ya Kanisa, changamoto na mwaliko kwa vijana kutoka kimasomaso. Ili kuweza kujiandaa barabara katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kuangalia mizizi ya maisha yao, wajitahidi kukutana na kuzungumza na wazee, wawaombe ushauri jinsi ya kuweza kuishi kikamilifu siku hizi za ujana wao! Wazee kwa hakika watawapatia ushauri mfuaka na wao watasonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kuwakumbushia vijana kwamba, Kanisa linawasubiri kwa hamu kubwa mjini Lisbon, nchini Ureno kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni.