Tume ya Kipapa ya Biblia: Magonjwa na Mateso Katika Biblia!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Biblia, Alhamisi tarehe 20 Aprili 2023 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, huku mazungumzo yao yakinogeshwa na kauli mbiu “Magonjwa na Mateso Katika Biblia.” Mwanadamu kwa asili amejeruhiwa na dhambi inayobeba ukweli wa mapungufu, udhaifu na kifo kilicho andikwa ndani ya nyoyo za binadamu. Ugonjwa na ukomo wa maisha ya mwanadamu katika mawazo ya kisasa ni jambo linaloonekana kuwa ni hasara, kero na jambo la lisilokuwa na thamani, kumbe linapaswa kupunguzwa, kupingwa na hata kufutwa kwa gharama yoyote ile. Mwanadamu anaogopa kuhoji maana ya magonjwa kwa sababu anaogopa athari zake kimaadili. Lakini magonjwa ni ukweli ambao unapaswa kufahamika na kwamba, hata mwaminifu wakati mwingine anadhohofu anapokutana na Fumbo la mateso na kifo katika safari ya maisha yake hapa duniani, anashtuka na wakati mwingine imani yake inaweza kutikiswa na hata kuwekwa rehani. Mwanadamu anaweza pia kuruhusu mateso kuingia moyoni mwake, kiasi hata cha kupelekea mwamini kukata tamaa na kuanza kuingia katika hali ya uasi. Kwa upande mwingine, mwanadamu anaweza kuyapokea mateso kama fursa ya kukua na hivyo, kutambua mambo msingi katika maisha hadi pale mwamini atakapokutana na Mwenyezi Mungu mubashara! Kuhusu magonjwa na hatimaye kifo ni dhana ambayo inafafanuliwa vyema zaidi katika Maandiko Matakatifu. Mgonjwa mara nyingi aliweza kujiaminisha mbele ya Mungu kwa machozi, huku akiomba uponyaji; wakati wa majaribu, misuko suko ya maisha na hivyo kuleta msukumo wa ndani yaani toba na wongofu wa ndani.
Katika Agano Jipya, Kristo Yesu anafunua: huruma, upendo, msamaha na jitihada zake za kumtafuta mwenye dhambi ili aweze kutubu na kumwongokea Mungu. Ni kutokana na muktadha huu Kristo Yesu katika maisha na utume wake alipenda kujenga mahusiano ya pekee na wagonjwa na wale wote waliokuwa wamevunjika na kupondeka moyo kama ilivyokuwa kwa wagonjwa wenye ukoma au wale waliokuwa wamepooza, Mama mkwe wake Simon bila kumsahau yule mtumishi wa Akida. Kristo Yesu aliwaweka huru wale wote waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu pamoja na kuwaponya wale wote waliojikabidhi kwake. Huruma iliyofunuliwa na Kristo Yesu ilikuwa ni ishara kwamba, Mwenyezi Mungu alikuwa anawatembelea watu wake, ikawa ni fursa ya kujitambulisha kwao, kwa kuwafunulia Umungu wake pamoja na utume wake wa Kimasiha, kiasi hata cha kufikia hatua ya kijifananisha nao akisema “Nalikuwa mgonjwa nanyi mkanijia.” Kilele cha utambulisho wa Kristo Yesu ni: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu na hivyo kuwapatia wafuasi wake agizo la kuendeleza utume wake kwa wagonjwa kwa kuwawekea mikono na kuwabariki kwa jina lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maandiko Matakatifu hayatoi majibu mepesi mepesi kuhusu suala la magonjwa na kifo! Badala yake, mwamini anaitwa na kualikwa kuchukua mateso na mahangaiko yake kama mahali muafaka pa kukutana na Mwenyezi Mungu, kama kielelezo cha ukaribu na uwepo wake, ili hatimaye waweze kuonja wema na huruma yake isiyokuwa na kikomo huwasimamia viumbe wake waliojeruhiwa ili kuwaponya, kuwahuisha na hatimaye, kuwaokoa.
Hivyo basi, kwa Mkristo mateso yanageuzwa kuwa ni chemchemi ya tumaini la ufufuo na wokovu na kwamba, hata udhaifu unakuwa ni zawadi kubwa ya ushirika ambayo Mwenyezi Mungu humfanya kushiriki katika utimilifu wake wa wema kwa usahihi kupitia uzoefu wa udhaifu na mahangaiko yake ya kibinadamu. Kumbe matukio ya mateso na mahangaiko katika maisha yanapaswa kutazamwa katika mwanga wa upendo, tayari kukubali udhaifu na mapungufu ya kibinadamu kama fursa ya ukuaji na ukombozi, kwani njia ya mateso ni mwanzo wa kuelekea kwenye kushiriki upendo mkuu wa Kristo Yesu. Uzoefu na mang’amuzi ya magonjwa na kifo ni mwaliko kwa waamini kuishi katika mshikamano wa kibinadamu na wa kikristo kulingana na mtindo wa Mungu ambao unasimikwa katika: Ukaribu, upendo na huruma. Mfano wa Msamaria mwema unawaalika waamini kujitoa sadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zake na kwamba, hili ni jambo la msingi katika ujenzi wa jamii inayojumuisha na yenye mwelekeo mzuri zaidi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wajumbe kwa kazi nzuri wanayoitekeleza katika huduma ya Neno la Mungu kwa njia ya tafiti makini na mafundisho adhimu, sehemu muhimu sana ya utume na maisha ya Kanisa. Uzuri wa kazi na utume huu, unategemea pia jinsi ambavyo mwamini mwenyewe anakuwa tayari kulipokea Fumbo la Umwilisho katika maisha yake ya imani.