Papa amemkabidhi Maria viongozi wa mataifa!
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, kabla ya sala ya Malkia wa Mbingu, katika Dominika ya tano ya Pasaka, kwenye uwanja wa Kossuth Lajos, jijini Budapest tarehe 30 Aprile 2023, amemshukuru kwanza Kardinali Erdő, Askofu Mkuu wa Budapest kwa maneno yake. Amemsalimia Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na Viongozi waliokuwapo katika Misa hiyo Takatifu. Baba Mtakatifu ameemeleza jinsi ambavyo anakaribia kurudi Roma lakini kabla ya kufanya hivyo, alitoa shukrani zake kwao, kuanzia na ndugu zake Maaskofu, mapadre, watawa wa kike na kiume na watu wote wapendwa wa Hungaria kwa makaribisho na upendo waliompatia katika siku hizi.
Baba Mtakatifu ametoa shukrani zake kwa wale ambao wamefika hapo kutoka mbali na wale ambao wamefanya kazi kwa bidii na vizuri kufanikisha ziara hiyo. Kwa kila mtu amesema köszönöm, Isten fizesse! yaani asante, Mungu atawalipa! Baba Mtakatifu amependa kuwa na kumbukumbu maalum kwa wagonjwa na wazee, kwa wale ambao hawakuweza kuwa pale , kwa wale wanaojisikia peke yao na kwa wale ambao wamepoteza imani kwa Mungu na matumaini ya maisha. Kwa wote hao amesema “Niko karibu na ninyi, ninawaombea na ninawabariki”.
Baba Mtakatifu katika salamu zake amewasalimu wanadiplomasia na kaka na dada wa madhehebu mengine ya Kikristo. Shukrani kwa uwepo wao na shukrani kwa sababu katika nchi hiyo madhehebu ya dini tofauti hukutana na kusaidiana. Kardinali Erdő Askofu Mkuu wa Budapest alisema kwamba watu wameishi hapo “kwenye mpaka wa mashariki wa Ukristo wa Magharibi kwa miaka elfu”.
Kwa hiyo ni vizuri kwamba mipaka haiwakilishi mipaka inayojitenga, lakini ni maeneo ya mawasiliano; na kwamba waaminio katika Kristo wamekuwa wakiweka mahali pa kwanza upendo unaounganisha na si tofauti za kihistoria, kiutamaduni na kidini zinazogawanya. Injili inatuunganisha na ni katika kurudi kwayo, kwenye chemchemi, safari kati ya Wakristo itaendelea sawasawa na mapenzi ya Yesu, Mchungaji Mwema anayetaka tuwe na umoja katika zizi moja."
Baba Mtakatifu baadaye ilikuwa ni wakati wa kumgeukia Mama Yetu Maria. Ambapo amesema:“kwake, Magna Domina Hungarorum, ambaye wanamwita kama Malkia na Mlinzi, amewakabidhi Wahungaria wote. “Na kutoka katika jiji hili kubwa na nchi hii adhimu, ningependa kuweka moyoni mwako imani na mustakabali wa bara zima la Ulaya, ambalo nimekuwa nikifikiria juu yake katika siku za hivi karibuni, na kwa njia fulani sababu ya amani”.
Bikira Mtakatifu, angalia watu wanaoteseka zaidi. Zaidi ya yote, angalia watu wa karibu wa Kiukraine waliouawa shahidi na watu wa Urussi, waliowekwa wakfu kwako. Wewe ni Malkia wa amani, tia ndani ya mioyo ya wanadamu na viongozi wa mataifa hamu ya kujenga amani, kuwapa vizazi mustakabali wa matumaini, na si wa vita; siku zijazo zilizojaa utoto, sio makaburi; na ulimwengu wa udugu, na sio wa kuta. Na tunakutazama wewe, Mama Mtakatifu wa Mungu: baada ya ufufuko wa Yesu ulisindikiza hatua za kwanza za jumuiya ya Kikristo, na kuifanya kudumu na kwa umoja katika sala (Mdo 1:14). Hivyo umewaweka waamini pamoja, ukidumisha umoja kwa unyenyekevu na kielelezo chako cha kusaidia. Tunakuomba kwa ajili ya Kanisa la Ulaya, ili liweze kugundua tena nguvu ya sala, ili liweze kugundua tena ndani yako unyenyekevu na utii, bidii ya ushuhuda na uzuri wa kutangaza. Na tunakabidhi Kanisa hili na nchi hii kwako. Wewe, uliyemfurahia Mwanao mfufuka, ujaze mioyo yetu na furaha yake.
Kwa kuhitimisha, Papa Mtakatifu amewatakia hilo, ili kueneza furaha ya Kristo: Isten éltessen! [Hongera!]. Ninashukuru kwa siku hizi, na ninawabeba moyoni mwangu na kuwaomba mniombee. Isten ald meg magyart! [Mungu abariki Wahungaria!", amehitimisha Papa.