Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu akisaidiana na Kardinali Leonardo Sandri, Makamu wa Dekano wa Makardinali. Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu akisaidiana na Kardinali Leonardo Sandri, Makamu wa Dekano wa Makardinali.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko: Mateso ya Yesu Ni Chemchemi ya Wokovu, Imani na Matumaini

Katika Maadhimisho ya Dominika ya Matawi, tarehe 2 Aprili 2023, Papa Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu akisaidiana na Kardinali Leonardo Sandri, Makamu wa Dekano wa Makardinali. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu: Fumbo la mateso ya Kristo Yesu: Kiroho na Kimwili: Kiini cha ukombozi kutoka katika lindi la dhambi na mauti; na chemchemi ya matumaini, kwa wale wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu, ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi wakiwa wamebeba matawi ya mitende mikononi mwao kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Matawi yaliyobarikiwa yanatunzwa na waamini kama visakramenti majumbani mwao, kuwakumbusha ushindi wa Kristo Yesu waliouadhimisha kwa kuandamana, huku wakiwa wamebeba matawi ya mitende mikononi mwao. Katika Maadhimisho ya Dominika ya Matawi, tarehe 2 Aprili 2023, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu akisaidiana na Kardinali Leonardo Sandri, Makamu wa Dekano wa Makardinali. Katika mahubiri yake, ametafakari kwa kina kuhusu: Historia ya Mateso ya Kristo Yesu, kama yalivyoandikwa na Mathayo 26:14-27:66. Baba Mtakatifu katika tafakari yake amekazia kwa namna ya pekee: Fumbo la mateso ya Kristo Yesu: Kiroho na Kimwili: Kiini cha ukombozi kutoka katika lindi la dhambi na mauti; na chemchemi ya matumaini, kwa wale wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. “Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha?” Mama Kanisa katika Liturujia ya Neno la Mungu, amewawezesha waamini kusikiliza tena Zaburi ya 22: 2 inayohusu mateso na matumaini ya mwadilifu kama kiini cha Fumbo la Mateso ya Kristo Yesu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.

Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme na Masiha wa Bwana
Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme na Masiha wa Bwana

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu aliteseka kimwili, alipigwa mijeledi, akatemewa mate, akavikwa taji ya miiba kichwani na hatimaye akatundikwa juu ya Msalaba. Aliteseka kiroho kwa kusalitiwa na mwanafunzi wake, Yuda Iskariote kwa vipande thelathini vya fedha; Mtume Petro akamkana mara tatu kabla ya jogoo kuwika, akahukumiwa kufa, kifo cha aibu, akashambuliwa na kudhihakiwa na askari pamoja na wapita njia. Katika mateso yote haya, Kristo Yesu alitambua kwamba, Yeye pamoja na Baba yake wa mbinguni ni wamoja na anatenda kazi pamoja naye. Rej. Yn 10: 30; 14:10. Lakini kabla ya kufa Msalabani, Kristo Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, “Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Mt 27:46. Hiki ni kielelezo cha mateso yaliyogusa na kutikisa maisha na utume wa Kristo, kiasi cha kuonesha ile sadaka yake ya hali ya juu kabisa, tukio ambalo limeandikwa na Mwinjili Mathayo pamoja na Marko. Rej. Mk 15:34. Kristo Yesu akaonja uchungu wa maisha, kwa kujiuliza kutoka katika undani wake, yote haya ni kwa ajili ya nini? Neno “Kuachwa” lina beba maana nzito katika Maandiko Matakatifu, kwani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mateso, cha “upendo ulioingia mchanga”, upendo uliokataliwa; upendo uliosalitiwa. Hiki ni kielelezo cha watoto waliokataliwa na wazazi wao, kiasi hata cha kutolewa mimba kabla ya kuzaliwa; ni kielelezo cha upweke hasi unaoweza kumtumbukiza mtu katika ugonjwa wa sonona; ni upweke kama ule wa mwanamke mjane au mwanaume mgane aliyempoteza mwenzi wake wake ndoa, “asali wa maisha yake.”

Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini
Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini

Huu ni ushuhda wa machungu katika maisha ya ndoa na familia; mahusiano tenge ya kijamii; dhuluma na nyanyaso; ukosefu wa haki na hatimaye, ni upweke hasi kutokana na magonjwa. Yote haya, Kristo Yesu aliyabeba na kutundikwa nayo juu ya Msalaba, katika hali isiyokuwa ya kawaida, akaonja umbali wa Baba yake wa mbinguni. Kristo Yesu aliteseka, akafa Msalabani na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Alipenda kumwonjesha mwanadamu upendo wake wa dhati, uliokuwa unabubujika kutoka katika “sakafu ya moyo wake”, changamoto na mwaliko kwa waamini, kuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini kwa jirani zao kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waonje uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu katika maisha yao, kiasi hata cha kuweza kushangazwa, ni kwa nini Kristo Yesu anawapenda kiasi hiki? Maswali tete kuhusu Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu ni huruma na upendo wake usiokuwa na mwisho, unaomkirimia mwamini matumaini, kwa kujiaminisha mikononi mwa Baba yake wa mbinguni. Kristo Yesu hata katika mateso makali, bado anaendelea kuwapenda, kuwaombea na hata kuwasamehe watesi wake. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ukatili wa binadamu unamezwa na huruma na upendo wa Kristo Yesu; utengano unageuzwa kuwa ni ujenzi wa ushirika, ukaribu na giza linageuzwa kuwa ni nuru ya ajabu. Kristo Yesu ni ufunuo wa Mwenyezi Mungu anayewapenda waja wake, kwa sababu binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu ni kiumbe chenye thamani kubwa!

Dominika ya Matawi, Mwanzo wa Maadhimisho ya Juma kuu
Dominika ya Matawi, Mwanzo wa Maadhimisho ya Juma kuu

Huu ndio upendo unaoweza kuleta mageuzi katika akili na nyoyo za watu kiasi hata cha kugeuza nyoyo za mawe kuwa nyoyo za nyama, kiasi hata cha kuwa ni chemchemi ya huruma, upole na upendo kamili. Kristo Yesu anaendelea kujitaabisha kuwatafuta wale waliopotea, ili kuwaokoa na kuendelea kuwaonjesha upendo wake usiokuwa na kifani! Kristo Yesu anataka pia wafuasi wake na watu wote wenye mapenzi mema, kumwonesha pia upendo wao, kwani aliwapenda upeo, kiasi hata cha kuzama katika maisha ya mwanadamu, akawa sawa na wanadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni katika muktadha huu, Upendo wa Kristo Yesu, unawawajibisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwatendea wema, ukarimu na upendo, wale wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kwani hao ndio kielelezo cha Kristo Yesu anayeendelea kuteseka katika hali ya maskini; wale wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa utu, heshima na haki zao msingi. Kuna maskini wa hali na kipato, wanaoishi huko barabarani na mitaani, lakini watu wanawapita na kuwageuzia kisogo. Kuna wakimbizi na wahamiaji, wanaopaswa kuangaliwa usoni kama binadamu wenye haki, utu na heshima yao na wala si kuangalia tu idadi yao. Kuna wafungwa na maabusu wanaoteseka magerezani na kukataliwa na jamii. Kuna makundi makubwa ya watu, wanaotambulishwa kuwa ni hatari kwa jamii kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu. Kuna watoto wanaotolewa mimba hata kabla ya kuzaliwa; wazee wanaotelekezwa kwenye nyumba za kutunzia wazee wakati wanao ndugu na jamaa zao ambao wangeweza kuwalinda na kuwatunza, lakini watu wanapendelea “kuponda mali ati kufa kwaja.”

Papa Francisko amewashukuru wote walioshiriki katika Ibada hii.
Papa Francisko amewashukuru wote walioshiriki katika Ibada hii.

Kuna wagonjwa ambao wamelazwa majumbani na hospitalini, wala hakuna mtu anayewajali kwa kuwatembelea na kuwasaidia katika mahangaiko yao; walemavu ambao wametelekezwa kama “daladala iliyokatika usukani.” Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna vijana wa kizazi kipya wanaojisikia watupu na wala hakuna watu wakusikiliza na kujibu kilio cha mateso na mahangaiko yao. Maadhimisho ya Juma kuu iwe ni fursa ya kuamsha tena dhamiri nyofu, ili kufumbua macho na masikio, tayari kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kwani watu kama hawa ni mfano hai wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Kristo Yesu kwa upendo wake wa dhati na kwa kujisadaka bila ya kujibakiza amemwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi n amauti. Huu ni mwaliko kwa waamini kuomba neema ya kupenda kama alivyopenda Kristo Yesu wale wote waliokuwa wametengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii! Akawaona, akawathamini na kuwarejeshea tena utu wao, heshima na haki zao msingi. Mwishoni mwa mahubiri yake, Dominika ya Matawi, Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio chao kwa matendo na kamwe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasizibe masikio na kuwageuzia kisogo. Ni wakati wa kumwilisha kwa matendo adili na matakatifu Injili ya huruma na upendo na kwa njia hii watakuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja na unyenyekevu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu “bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu.” Flp 2:7.

Mateso

 

02 April 2023, 15:18