Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika kipindi hiki cha Pasaka, Mama Kanisa anamshangilia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika kipindi hiki cha Pasaka, Mama Kanisa anamshangilia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko Afafanua Maana ya Fumbo la Pasaka na Amani Duniani

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Jarida la “L’Espresso” linalochapishwa nchini Italia, anapembua kwa kina na mapana maana ya Sherehe ya Pasaka na Amani Duniani, wakati huu ambapo walimwengu wanaonekana kupoteza matumaini kutokana na vita na jeuri ya baadhi ya viongozi wanaoendelea kujimwambafai nchini Ukraine, bila kusahau maeneo mengine ya dunia, ambako Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inaendelea kupiganwa vipande vipande! Hatari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo ambao waamini wa Kanisa la Mwanzo waliusadiki, wakauuishi na kuutangaza kama kiini cha ukweli; waliuendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; wakauthibitisha kwa njia ya Maandiko Matakatifu ya Agano Jipya na wakauhubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko kwa wafu na kwa njia ya kifo chake, ameshinda mauti na wafu amewapatia uzima. Hili ni tukio halisi linaloweza kuthibitishwa kihistoria. Kaburi tupu limekuwa ni alama muhimu kwa watu wote, hatua ya kwanza kutambua tukio la ufufuko, kama ilivyokuwa kwa wale wanawake watakatifu pamoja na Mitume wa Yesu. Wanawake watakatifu ni mashuhuda wa kwanza wa Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Mitume na wanafunzi wa Yesu walipata taabu sana katika mchakato wa kukabiliana na ukweli kuhusu Ufufuko wa Kristo Yesu, kiasi kwamba, baadhi yao waliona shaka! Imani ya Mitume katika Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu imezaliwa kwa tendo la neema ya Kimungu, yaani kutokana na mang’amuzi yao ya moja kwa moja ya ukweli wa Kristo Mfufuka. Mwili wa Kristo Yesu katika ufufuko umejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kiasi kwamba, Mtakatifu Paulo anaweza kukiri kwamba Kristo Yesu ni Mtu wa mbinguni. Licha ya ufufuko wa Kristo Yesu kuwa ni wa kihistoria, lakini linabaki kuwa ni Fumbo la Imani, ndiyo maana wafuasi wa Kristo Yesu wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Rej. KKK 638-658.

Fumbo la Pasaka ni muhtasari wa imani, matumaini na mapendo
Fumbo la Pasaka ni muhtasari wa imani, matumaini na mapendo

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Jarida la “L’Espresso” linalochapishwa nchini Italia, anapembua kwa kina na mapana maana ya Sherehe ya Pasaka na Amani Duniani, wakati huu ambapo walimwengu wanaonekana kupoteza matumaini kutokana na vita na jeuri ya baadhi ya viongozi wanaoendelea kujimwambafai nchini Ukraine, bila kusahau maeneo mengine ya dunia, ambako Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inaendelea kupiganwa vipande vipande. Baba Mtakatifu anasema, katika kipindi hiki cha Pasaka, Mama Kanisa anamshangilia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Yn 20:19-23. “Amani kwenu” ni zawadi ya kwanza ya Kristo Mfufuka kwa wafuasi wake waliokuwa wamejifungia chumba cha juu kutokana na uwoga, baada ya kuona mateso na kifo chake cha Msalaba. Amani ni kati ya matamanio halali ya binadamu anasema, Papa Francisko kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu kupinga vita, vurugu na mipasuko ya kijamii. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, binadamu anajitahidi kung’oa na kutokomeza kutoka ndani mwake mizizi ya vita, vurugu na mipasuko ya kijamii; inayopata chimbuko lake katika: “Chuki, wivu, uhasama, choyo na tabia ya kupenda kulipiza kisasi.”

Vita inapaswa kutibiwa kutoka katika undani wa moyo wa mtu!
Vita inapaswa kutibiwa kutoka katika undani wa moyo wa mtu!

Baba Mtakatifu anawashukuru wamiliki wa Jarida la “L’Espresso” kwa kutoa nafasi kwa mashuhuda, wajumbe na wapenda amani, ili kutoa maoni yao. Huu ni mwaliko wa kuondoa sumu ya chuki, vita na uhasama kutoka katika sakafu ya nyoyo za watu, ili kutoa nafasi kwa mbegu ya amani, haki na upatanisho ziweze kuchanua na kuzaa matunda yanayokusudiwa. Mtakatifu Yohane XXIII tarehe 11 Aprili 1963 yaani miaka 60 iliyopita alichapisha Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani.” Hii ni amani duniani, ambayo watu wa nyakati zote waliitamani kwa hamu kubwa sana, na kamwe haiwezi kujengwa wala kuimarishwa isipokuwa kwa kulinda kitakatifu utaratibu uliowekwa na Mungu. Kwa njia ya maendeleo ya sayansi mbalimbali na vumbuzi za teknolojia mpya, mwanadamu amefahamu zaidi kwamba utaratibu wa ajabu unafanya kazi katika viumbe na katika nguvu za asili, na kwamba mtu ana cheo maalum, kiasi cha kuweza kutambua utaratibu huo na kutengeneza nyenzo ili kutawala nguvu hizi na kuzigeuza ziwe kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha na haki za tunu za kimaadili na kiutamaduni. Huu ni wakati wa kukataa katu katu: utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita kwani ni kinyume cha maadili na utu wema.

Amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani.
Amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani.

Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unalenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Amani ya kweli inajengwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa watengenezaji na wafanyabiashara biashara ya silaha duniani, hii kauli kamwe haitaweza kuwafurahisha, lakini huu ndio ukweli wa mambo na wala si wazo la kufikirika tu, linaloelea kwenye ombwe! Ni wakati muafaka wa kuondokana na mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha na badala yake, kutimia rasilimali hii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu, kwa kupambana na baa la njaa, ujinga, maradhi na umaskini; mambao yanayopenyekenyua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimiza mahojiano haya maalum, kwa kuwatakia watu wote amani na utulvu!

Papa: Maana ya Pasaka

 

11 April 2023, 14:11