Tafuta

, Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa Kuu tarehe 7 Aprili 2023 ni shuhuda zilizotolewa kwa Baba Mtakatifu wakati wa hija zake za kitume sehemu mbalimbali za dunia. , Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa Kuu tarehe 7 Aprili 2023 ni shuhuda zilizotolewa kwa Baba Mtakatifu wakati wa hija zake za kitume sehemu mbalimbali za dunia.  (AFP or licensors)

Njia ya Msalaba 2023 Sauti ya Amani Katika Ulimwengu Uliogubikwa na Vita!

Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa Kuu tarehe 7 Aprili 2023 ni shuhuda zilizotolewa kwa Baba Mtakatifu wakati wa hija zake za kitume sehemu mbalimbali za dunia, ambazo zimehaririwa na Sekretarieti kuu ya Vatican kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume: “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani.” Hizi ni sauti za amani katika ulimwengu uliogubikwa na vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane XXIII tarehe 11 Aprili 1963 yaani miaka 60 iliyopita alichapisha Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani.” Hii ni amani duniani, ambayo watu wa nyakati zote waliitamani kwa hamu kubwa sana, na kamwe haiwezi kujengwa wala kuimarishwa isipokuwa kwa kulinda kitakatifu utaratibu uliowekwa na Mungu. Kwa njia ya maendeleo ya sayansi mbalimbali na vumbuzi za teknolojia mpya, mwanadamu amefahamu zaidi kwamba utaratibu wa ajabu unafanya kazi katika viumbe na katika nguvu za asili, na kwamba mtu ana cheo maalum, kiasi cha kuweza kutambua utaratibu huo na kutengeneza nyenzo ili kutawala nguvu hizi na kuzigeuza ziwe kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha na haki za tunu za kimaadili na kiutamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, mashindano ya utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha, zikiwemo silaha za nyuklia yanaendelea kukomba rasilimali za dunia ambazo zingeweza kutumika vyema zaidi kwa ajili ya kunogesha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Kunahitajika mkakati wa Kimataifa ili kusitisha hatari inayoweza kusababishwa na mashindano ya silaha kwani madhara yake ni makubwa kama inavyojionesha huko nchini Ukraine. Kuna Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa sehemu mbalimbali za dunia na madhara yake ni makubwa kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na kuchechemea kwa hali ya maisha; kukosekana kwa uhakika na usalama wa chakula duniani hasa Barani Afrika na Mashariki ya Kati.

Sauti ya amani katika ulimwengu uliogubikwa kwa vita
Sauti ya amani katika ulimwengu uliogubikwa kwa vita

Vita imeendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato kama inavyojionesha nchini Siria na sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, kuna haja ya kukazia majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kukuza na kudumisha amani, utulivu na maridhiano kati ya watu; hali inayopaswa kusimikwa katika majadiliano. Ni katika muktadha huu, Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa Kuu tarehe 7 Aprili 2023 ni shuhuda zilizotolewa kwa Baba Mtakatifu wakati wa hija zake za kitume sehemu mbalimbali za dunia, ambazo zimehaririwa na Sekretarieti kuu ya Vatican kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume: “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani.” Hizi ni sauti za watu kutoka katika maeneo ya vita, dhuluma na nyanyaso, ambazo zinatangaza kilio cha amani duniani, kama ilivyokuwa wakati wa kuzaliwa Kristo Yesu mjini Bethlehemu na kama alivyofanya alipokuwa ametundikwa juu ya Msalaba, akawasamehe watesi wake, leo hii awasamehe binadamu kutokana na mapungufu yao; agange na kuponya nyoyo za ona hatimaye, awakirimie amani ya kudumu. Kutokana na changamoto za kiafya, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa kuu tarehe 7 Aprili 2023 amelazimika kufuatilia Njia ya Msalaba akiwa kwenye Makazi yake ya Hosteli ya Mtakatifu Martha mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, amani ya kweli inapata chimbuko lake katika akili na nyoyo za watu wenye mapenzi mema, wanaoweza kuthubutu kunyamazisha mlio wa bunduki na kuanza kujielekeza zaidi kwenye mchakato wa ujenzi wa misingi ya majadiliano, haki, msamaha na upatanisho unaowatambua watu wote kuwa ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Watu wanuie hata wokovu kwa ajili ya jirani zao. Kuna watu wanalazimika kuzikimbia nchi zao kiasi hata chakuhatarisha maisha yao jangwani na hata kuzama kwenye vilindi vya Bahari. Watu wajenge na kuimarisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kuwasaidia na kuwapatia hifadhi wale wote wanaoteseka kama wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maaulum.

Kumbukizi ya Miaka 60 ya Waraka wa Pacem in terris
Kumbukizi ya Miaka 60 ya Waraka wa Pacem in terris

Ni katika hali na mazingira kama haya watu wanajikuta wakiwa wameteleza, kuanguka na hatimaye kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuvuruga misingi ya amani duniani. Kumbe, kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kusaidiana kwa hali na mali. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika Njia ya Msalaba, hata leo hii kuna akina mama wanaoshuhudia watoto wao wakipoteza maisha kutokana na ajali mbalimbali, vita na mabomu ya kutegwa ardhini ambayo bado yanasababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na chuki, uhasama na tabia ya kutaka kulipiza kisasi. Ni katika hali na mazingira kama haya, watu wa Mungu wanaweza kujenga mazingira bora yatakayosaidia kutoa hifadhi kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Wawaone kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wenye haki na nyajibu wanazoweza kutekeleza katika jamii. Hawa ni watu wanaowahitaji wasamaria wema na akina Simoni wa Kirene waliomsaidia Kristo Yesu kubeba Msalaba wake! Kuna watu wanatekwa nyara na wengine wanapotea katika hali na mazingira ya kutatanisha kiasi hata cha kudhalilishwa na kutweza; kuna watu wameathirika sana kutokana na vitendo vya kigaidi na hujuma za kiuchumi. Yote haya yanafanywa na watu wachache ndani ya jamii ili kujipatia utajiri wa haraka haraka na hivyo kusahau utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kumbukizi ya Miaka 60 ya Waraka wa Pacem in terris
Kumbukizi ya Miaka 60 ya Waraka wa Pacem in terris

Ulimwengu unawahitaji sana mashuhuda wa haki, amani na maridhiano ya kijamii. Vijana wengi, wangetamani kubaki nyumbani mwao, kuendelea na masomo na kujipatia ajira, lakini baadhi yao wanajikuta wakiwa mstari wa mbele vitani. Vijana walioshiriki katika Njia ya Msalaba wanasema, wamechoka na vita, wanataka amani na usalama ili warejee tena makwao! Watu wanaotoka kwenye maeneo ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii wanasema, hii ni Misalaba ambayo imekuwa ni sababu ya watu kupekenywa na baa la njaa, magonjwa na umaskini na hata kuyakimbia makazi yao ili kutafuta usalama na maisha bora zaidi. Kuna haja kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Katika shida na mahangaiko ya mazito ya ndani, unafika wakati hata mwamini anashindwa kuonja uwepo angavu wa Mungu katika maisha yake kuona na kuwapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na vita. Lakini, mashuhuda wanasema, wamepata nguvu ya kusonga mbele, licha ya matatizo na magumu yanayowaandama kutoka katika Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na udugu wa kibinadamu. Watoto na vijana wafundwe kuheshimu na kuthamini tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu kwa kujikita katika misingi ya ukweli, uwazi, uaminifu na uadilifu, ili kweli amani iweze kushika mkondo wake katika maisha ya watu mbalimbali. Mashuhuda katika Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, wanasema, kuna watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa kutokana na vita, ndiyo maana, kuna watoto wamemwandikia Kristo Yesu barua wakimwomba asaidie kukomesha vita sehemu mbalimbali za dunia, ili amani iweze kutawala katika akili na nyoyo za watu, ili watu wote licha ya tofauti zao msingi waweze kujisikia kuwa ni ndugu wamoja, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Vita ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya binadamu
Vita ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya binadamu

Kwa hakika, vita ni sumu ya matumaini, ustawi na maendeleo ya wengi. Leo hii, watu wanaoishi katika mazingira ya vita na mipasuko ya kijamii, hawana amani wala matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kuna watu wanateseka kutokana na majanga asilia kwa sababu ya uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, kiasi kwamba wanajikuta wakiwa wametundikwa Msalabani kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kwenye Njia ya Msalaba. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha usalama, maisha, mafungamano ya kijamii pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu ya umma. Vitendo vya kigaidi ni kinyume kabisa na uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Hivi ni vitendo ambavyo vinapaswa kulaaniwa na kushutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa bila “kupepesa pepesa macho! Imani thabiti, utu wema, haki na amani, visaidie kujenga jamii inayosimikwa katika umoja, udugu na mshikamano wa kibinadamu, ili kushuhudia upendo wa Mungu kwa watu wote! Huu ni upendo ambao unaangazwa na misingi ya imani ya kweli, amani na upatanisho, ili Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka, aweze kuwakirimia waja wake, amani ya kudumu inayopata chimbuko lake katika dhamiri nyofu na moyo uliotulia, usiotaka wala kutamani makuu! Baada ya mateso makali ya Njia ya Msalaba, Kristo Yesu alizikwa kaburini. Waamini kwa njia ya Ubatizo, wanakufa na kufufuka na Kristo Yesu; wanazika utu wao wa kale na kujivika utu mpya unaowawezesha kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Kristo Mfufuka awe ni chemchemi ya haki, amani na maridhiano.
Kristo Mfufuka awe ni chemchemi ya haki, amani na maridhiano.

Ni wakati wa kuweka silaha chini na kuanza mchakato wa haki, msamaha na upatanisho mambo msingi katika ujenzi wa amani ya kudumu. Mwishoni mwa Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, watu wa Mungu wamemshukuru Kristo Yesu kwa ujasiri wake uliomwezesha kuubeba Msalaba; Madonda yake Matakatifu ni chemchemi ya Sakramenti za Kanisa kwa ajili ya kuganga na kuponya udhaifu wa mwanadamu. Wanamshukuru Bikira Maria, aliyemfuata katika Njia ya Msalaba, akawa ni kielelezo cha imani, upendo na matumaini ya kweli. Msamaha na huruma ya Kristo Yesu, isaidie kuganga na kuponya madhaifu ya binadamu. Msalaba uwe ni alama ya maisha mapya na msamaha wa kweli, silaha makini dhidi ya dhambi na mauti, tayari kuanza kujielekeza katika mchakato wa upatanisho, haki na amani duniani!

Njia ya Msalaba 2023
08 April 2023, 16:41