Michezo ya Olimpiki 2024 Jijini Paris Ni Wakati wa Ushuhuda wa Kikristo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbali mbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu, furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbalimbali ni jukwaa la kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa walimwengu. Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa iliuchagua mji mkuu wa Ufaransa, Paris, kuwa mwenyeji wa michuano ya Olimpiki mwaka 2024, na kuutunuku mji wa Los Angeles nchini Marekani kuwa mwenyeji wa michuano hiyo kwa mwaka 2028.
Ni katika muktadha wa mashindano ya Olimpiki Jijini Paris, Ufaransa, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu nchini Ufaransa, kuonesha moyo wa ukarimu, upendo na wajibu mkuu kwa kuwakaribisha wanamichezo kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Ufaransa kutumia fursa hii kuwa ni tukio la kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kutoka katika tamaduni na dini mbalimbali. Hii ni changamoto ya kujenga moyo wazi na wakujitolea, tayari kutumia: Makanisa, Shule na Nyumba zao kama kielelezo cha upendo, ukarimu na ushuhuda wa tunu msingi za Kikristo, chemchemi ya furaha ya kweli. Iwe ni fursa ya kujenga mshikamano na maskini, walemavu na wale wote wanaobaguliwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Michezo ya Olimpiki iwe ni fursa ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaohitajiwa sana katika nyakati hizi. Tangu wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa baraka zake za Kitume kwa waandaaji na watu wote wa kujitolea bila kuwasahau wote watakaoshiriki katika mashindano haya kwa mwaka 2024. Ikumbukwe kwamba, michezo ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, kimekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.