Tafuta

Papa katika Uwanja wa Kossuth Lajos:Hungaria iangazwe maisha mapya!

Yesu ndiye mlango unaotupeleka nje ulimwenguni.Anatusukuma kwenda kukutana na kaka na dada zetu.Kila mtu,bila ubaguzi,ameitwa kwa hilo,kuondoka katika la faraja na kuwa na ujasiri wa kufikia kila pembe inayohitaji mwanga wa Injili.Ni mahubiri ya Papa Aprili 30.

Na Angella Rwezaula;- Vatican.

Dominika ya tano ya Pasaka, imemkuta Baba Mtakatifu  Francisko jijini Budapest katika hija ya 41 ya kitume, ambapo amekuwa katika Uwanja wa Kossuth Lajos tarehe 30 Aprili 2023, katika siku ambayo Mama Kanisa anadhimisha Mchungaji Mwema, sanjari na maadhimisho ya  Siku ya 60 ya Kuombea Miito duniani, iliyoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI mnamo 1964. Uwanja ulijaa waamini kuanzia maaskofu, mapadre, mashemasi, watawa, waseminari na watu wote wa Mungu, hata viongozi wa serikali, madhehebu mengine na wanadiplomasia. Baba Mtakatifu Francisko akianza mahubiri yake mara baada ya masomo, amesema: “Maneno ya mwisho ambayo Yesu anatamka katika Injili ambayo tumesikia yanatoa muhtasari wa maana ya utume wake: “Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yn 10:10). Hivi ndivyo mchungaji mwema afanyavyo: hutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Hivyo Yesu, kama mchungaji anayekwenda kulitafuta kundi lake, alikuja kututafuta tulipokuwa tumepotea; kama mchungaji, alikuja kutunyakua kutoka katika kifo; kama mchungaji anayewajua kondoo wake mmoja baada ya mwingine na kuwapenda kwa huruma isiyo na kikomo, ametuachia tuingie katika zizi la Baba, na kutufanya kuwa watoto wake”.

Misa Takatifu katika uwanja wa Kossuth Lajos
Misa Takatifu katika uwanja wa Kossuth Lajos

Kwa hiyo, Baba Mtakatifu amependa kutafakari sura ya Mchungaji Mwema, kwa kuzingatia matendo mawili ambayo, kwa mujibu wa  Injili, anawatunza kondoo wake: Kwanza  kabisa “anawaita, kondoo wake” kisha anaongoza nje. Kwa hiyo mwanzoni mwa historia yetu ya wokovu, hatuko pale na sifa zetu, uwezo wetu, miundo yetu; katika asili kuna mwito wa Mungu, shauku yake ya kutufikia, hangaiko lake kwa kila mmoja wetu, wingi wa huruma yake inayotaka kutuokoa kutoka katika dhambi na kifo, ili kutupatia uzima kwa wingi na furaha isiyo na mwisho. Yesu alikuja kama Mchungaji Mwema wa wanadamu ili kutuita na kutupeleka nyumbani. Kwa hiyo nasi tukikumbuka kwa shukrani, tunaweza kukumbuka upendo wake kwetu sisi ambao tulikuwa mbali naye.” Ndiyo, wakati “sisi sote tulikuwa tumepotea kama kundi” na “kila mmoja wetu akaenda zake mwenyewe” alisema(Is 53:6). Alichukua maovu yetu na kuchukua dhambi zetu, na kuturudisha kwenye moyo wa Baba. Ndivyo lilisikika somo la Mtume Petro katika somo la pili: “Mlikuwa mkitanga-tanga kama kondoo, lakini sasa mmerudishwa kwa Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu” (1 Pt 2:25). Na bado leo hii, katika kila hali ya maisha, katika kile tulichobeba mioyoni mwetu, katika mshangao wetu, katika hofu zetu, kwa maana ya kushindwa ambayo wakati mwingine hutushambulia, katika gereza la huzuni linalotishia kutufunga, anatuita.  Anakuja kama Mchungaji mwema na anatuita kwa jina, ili atuambie jinsi tulivyo wa thamani machoni pake, kutuponya majeraha yetu na kubeba juu yake udhaifu wetu, kutukusanya katika umoja katika zizi lake na kutufahamisha na Baba, na kila mmoja.

Wakati wa Misa na matoleo
Wakati wa Misa na matoleo

Baba Mtakatifu alifafanua kuwa, uwepo wao hapo uliwajaza na kusikia furaha ya kuwa watu watakatifu wa Mungu: Wote wamezaliwa kutokana na wito wake; “ndiye aliyetuita na kwa sababu hii sisi tu watu wake, kundi lake, Kanisa lake” . Kwa hiyo amewakusanya hapo ili, hata kama wao ni tofauti na kila mmoja wao  ni wa jamii tofauti, ukuu wa upendo wake umewaleta pale katika kukumbatiana mmoja na mwingne. Inapendeza kujikuta wako pamoja: Maaskofu na mapadre, watawa na waamini walei; na inapendeza kushiriki furaha hii pamoja na wajumbe wa kiekumene, wakuu wa jumuiya ya Wayahudi, wawakilishi wa taasisi za kiraia na mabalozi wa kidiplomasia. Papa ameongeza kusema: “Huu ndio ukatoliki: sisi sote Wakristo, tuitwao kwa majina na Mchungaji Mwema, tunaitwa kukaribisha na kueneza upendo wake, ili kufanya zizi lake liwe shirikishi na kamwe lisiwe la kutengwa.” Kwa hiyo wote wameitwa kukuza uhusiano wa udugu na ushirikiano, bila kujigawa, bila kuzingatia jamii yao kama mazingira yaliyohifadhiwa, bila kushikwa na wasiwasi wa kutetea nafasi ya kila mmoja, lakini kujifungulia kwa upendo wa pande zote.

Baba Mtakatifu wakti wa Misa Takatifu
Baba Mtakatifu wakti wa Misa Takatifu

Baba Mtakafu amesema kuwa baada ya kuwaita kondoo, Mchungaji “anawaongoza nje” (Yh 10:3). Awali ya yote aliwafanya waingie zizini kwa kuwaita, sasa anawasukumia nje. Kitu cha kwanza ni kukusanywa katika familia ya Mungu ili kuwa watu wake, lakini kisha kutumwa kwenda ulimwenguni ili, kwa ujasiri na bila woga, kuweza kuwa watangazaji wa Habari Njema, mashuhuda wa Upendo ambao umefanya kuzaliwa kwa  upya. “Tunaweza kufahamu mwendo huu  kwa kuingia na kutoka katika picha nyingine ambayo Yesu anatumia: ile ya mlango.  Yeye anasema: “Mimi ndimi mlango: mtu akiingia katika mimi, ataokolewa; ataingia na kutoka na kupata malisho” (Yh 10, 9). Papa ameomba kuwa makini juu ya “kuingia na kutoka”. Kwa upande mmoja, Yesu ndiye mlango ambao umefunguka sana kuturuhusu kuingia katika ushirika wa Baba na kuonja huruma yake; lakini, kama kila mtu anajua, mlango wazi hutumiwa sio tu kuingia, lakini kuondoka pia mahali ulipo. Na kisha, baada ya kuturudisha katika kumbatio la Mungu na katika zizi la Kanisa, Yesu ndiye mlango unaotupeleka nje ulimwenguni: Anatusukuma kwenda kukutana na kaka na dada zetu. Na tukumbuke vyema: kila mtu, bila ubaguzi, ameitwa kwa hilo, kuondoka katika eneo letu la faraja na kuwa na ujasiri wa kufikia kila pembe inayohitaji mwanga wa Injili”, (Evangelii gaudium, 20), Papa amesisitiza.

Baba Mtakatifu akitoa mahubiri yake
Baba Mtakatifu akitoa mahubiri yake

Baba Mtakatifu kwa ufafanuzi zaidi amkazia kusema kuwa : Katika kutoka ina maana kwa kila mmoja wetu kuwa, kama Yesu, mlango wazi. Inasikitisha na inaumiza kuona milango iliyofungwa: milango iliyofungwa ya ubinafsi wetu kuelekea wale wanaotembea kando yetu kila siku; milango iliyofungwa ya ubinafsi wetu katika jamii ambayo inahatarisha kustahimili upweke; milango iliyofungwa ya kutojali kwetu wale walio katika mateso na umaskini; milango imefungwa kwa wale ambao ni wageni, tofauti, wahamiaji, maskini. Na hata milango iliyofungwa ya jumuiya zetu za kikanisa: imefungwa kati yetu, imefungwa kuelekea ulimwengu, imefungwa kwa wale ambao hawafanani nasi, imefungwa kwa wale wanaotamani msamaha wa Mungu. Kwa kusisitiza hilo Papa amesema: “Tafadhali tufungue milango! Hebu pia tujaribu kuwa kama Yesu, kwa maneno, ishara, shughuli za kila siku na mlango uwe wazi, mlango ambao haujafungwa kwa gadhabu  usoni pa  mtu yeyote, mlango unaoruhusu kila mtu kuingia na kuona uzuri wa upendo na msamaha kutoka kwa Bwana”.

Wakati wa kutoa vipaji
Wakati wa kutoa vipaji

Papa amependa kurudia hilo hasa kwa kujigeukia yeye mwenyewe, maaskofu wenzake, mapadre, kwanza wao kama wachungaji kwamba:  “Kama mchungaji, Yesu sio mhuni au mwizi ( Yh 10:8); yaani, hatumii nafasi yake kwa kujinufaisha, halidhulumu kundi alilokabidhiwa, hatumii nafasi kutoka kwa ndugu walei, na hatumii mamlaka magumu". Kwa hiyo "Tujitie moyo kuwa  na milango iliyo wazi zaidi, ya kuwa wawezeshaji wa neema ya Mungu, wataalamu katika ukaribu, tayari kutoa uzima, kama Yesu Kristo, Bwana wetu na wote, kama anavyotufundisha kwa mikono iliyo wazi kutoka katika msalaba na inatuonesha kila wakati altareni, Mkate wa uzima uliomegwa kwa ajili yetu". Baba Mtakatifu amerudia kusema hayo hayo hata kwa kaka na dada walei, kwa makatekista, wahudumu wa kichungaji, kwa wale wenye majukumu ya kisiasa na kijamii, kwa wale wanaoendelea na maisha yao tu ya kila siku, wakati mwingine kwa shida ili wawe na milango wazi. Papa amesema: “Hebu tumruhusu Bwana wa uzima aingie mioyoni mwetu, Neno lake linalofariji na kuponya, kisha tutoke nje na tuwe wenye milango wazi katika jamii. Kuwa wazi na umoja kwa mtu mwingine, kusaidia Hungaria kukua katika udugu,  na njia ya amani”.

Askofu Mkuu wa Budapest na Papa Francisko
Askofu Mkuu wa Budapest na Papa Francisko

Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu amesema: "Yesu Mchungaji Mwema anatuita kwa jina na hututunza kwa huruma isiyo na kikomo. Yeye ndiye mlango na yeyote anayeingia kupitia yeye ana uzima wa milele: kwa hiyo yeye ni wakati wetu ujao, wakati ujao wa uzima tele” (Yn 10:10). Kwa hiyo, kamwe tusivunjike moyo, tusikubali kamwe kuibiwa furaha na amani ambayo ametupatia, tusijitoe katika matatizo au kutojali. Tujiruhusu kuandamana na Mchungaji wetu: pamoja naye maisha yetu, familia zetu, jumuiya zetu za Kikristo na Hungaria yote yaangaze kwa maisha mapya!” Mara baada ya Misa, Askofu Mkuu wa Budapest alimshukuru Papa kwa hija yake, na maeno aliyowalekeza kuwa Kanisa linalotoka kwenda nje.

Mahubiri Papa 30 Aprili 2023
30 April 2023, 11:08