Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Lisbon, Ureno 2023: Matumaini Kwa Vijana!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023, ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu. Awe ni mfano bora wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu katika maisha! Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika huduma ya upendo! Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa kawaida pale ambapo kijana anaanguka, utu wake pia unaanguka; anapoinuka, anauinua pia utu wa watu wengine ulimwenguni kote. Hii ni nguvu maridhawa ambayo iko mikononi mwa vijana. Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anapenda kuwaambia vijana “Inuka” ujumbe mahususi ambao utawasaidia vijana kujiandaa kwa nyakati na kuwa tayari kuandika kurasa mpya katika historia ya mwanadamu, jambo ambalo linahitaji: nguvu, hamasa na ari kubwa, ili kuinuka, tayari kuwa shuhuda wa mambo hayo aliyoyaona. Mtume Paulo ambaye alilitesa na kulidhulumu Kanisa anashuhudia kuhusu nuru angavu kutoka mbinguni na sauti ya Kristo Yesu aliyemwita kwa jina lake.
Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuzama zaidi katika tukio hili la kuitwa kwa Saulo mara mbili kama alivyofanya Musa na Samuel. Paulo Mtume alishuhudia ufunuo na nguvu ya Mungu, kuonesha kwamba, Kristo Yesu alimfahamu vizuri sana kama mtu aliyekuwa na chuki dhidi ya Wakristo kutokana na ujinga wake. Kristo Yesu alitaka kumwonjesha, huruma na upendo wake wa daima. Hii ni neema, kielelezo cha upendo usiokuwa na kifani na mwanga mpya utakaomletea wongofu. Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 22 Aprili 2023 mara baada ya kukutana na kuzungumza na Carlos Moedas Mstahiki Meya wa Jiji la Lisbon, nchini Ureno mintarafu maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2023 amewatumia watu wa Mungu nchini Ureno ujumbe wa matumaini kwa wale wote wanaojibidiisha usiku na mchana kuandaa hija yake ya kitume nchini Ureno. Anafurahishwa sana na maandalizi na anawaomba msamaha kutokana na vurugu zinazoweza kujitokeza kati yao, lakini anawashukuru sana kwa makaribisho yao, matumaini na uwazi wa moyo! Anawatakia kile la kheri na Mwenyezi Mungu apende kuwabariki na kuwapatia nguvu ya kusonga mbele kwa ari na mwamko mkubwa.
Paulo Mtume alikuwa hajapata nafasi ya kukutana mubashara na Kristo Yesu, bali alibahatika kuonana na Wakristo aliowadhulumu na kwa hakika, alikuwa amekutana na Kristo Yesu kati ya watu aliowadhulumu. Kumfahamu Kristo Yesu na Kanisa lake ni kama chanda na pete. Wakristo wanaweza kupata mang’amuzi haya, ikiwa kama wamejenga umoja wa Kikanisa. Kristo Yesu anataka vijana nao kutubu na kumwongokea, tayari kusikiliza na kujibu wito na mwaliko wake! Jambo la msingi ni vijana kujibidiisha kukutana na Kristo Yesu katika: Sala, Neno, Sakramenti na matendo ya huruma ili kuonja neema na msamaha wake, na hatimaye, waweze kumpenda kwa moyo na akili zao zote, tayari kukumbatia na kuambata mtindo mpya wa maisha na kupokea utume kama ilivyokuwa kwa Sauli. Watakatifu wengi walipenda kusema na kushuhudia ukweli wa mambo, leo hii mambo yamebadilika sana, watu wengi hawataki kutangaza na kushuhudia ukweli, ili wapendwe kama walivyo! Toba na wongofu wa Mtakatifu Paulo ulimwezesha kuendelea na safari kuelekea Dameski, huku akiwa ni mtu mpya kabisa. Wongofu wa ndani ni hija ya maisha ya kila siku, jambo la msingi ni kumtii Kristo Yesu, na kumwachia nafasi ili aweze kufanya mabadiliko katika nia na malengo yao, ili waweze kuwa ni Mitume, mashuhuda na watangazaji wa Injili. Ni fursa ya kuimarisha fadhila ya ukimya na sala kama Paulo alivyokirimiwa na Kristo Yesu. Hii ni changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanamfuasa Kristo, ili kupata mwanga halisi wa maisha.
Baba Mtakatifu anaonya kwamba, vijana ndio waathirika wa kwanza pamoja na wale wanaowazunguka, kwa kukumbatia itikadi zinazobomoa utu na heshima ya binadamu. Kwa kuwa na misimamo mikali ya kidini na kiimani inayopelekea vurugu na uvunjifu wa amani. Kwa baadhi ya vijana, mitandao ya kijamii imekuwa ni silaha za mapambano dhidi ya wengine, kiasi hata cha kuthubutu kutumia habari za kughushi kama silaha ya kuwachafulia wengine sifa njema na hatimaye, kusambaza sumu. Baba Mtakatifu anawaomba vijana wamwachie Kristo Yesu nafasi ili kuwasaidia kuibua na kukuza karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kwa toba na wongofu wa ndani, Mtakatifu Paulo, akabahatika kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa ya watu aliowanyanyasa na kuwadhulumu. Hata leo hii, Kristo Yesu anawaamini sana vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo. Wakristo wanaitwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, ili kutangaza na kushuhudia hayo walioyaona, kwa kuzingatia uzoefu na mang’amuzi yao ya maisha. Vijana wasisahau kwamba: “kwa kweli, kila mmoja ambaye ameuonja kiukweli upendo wa Mungu unaookoa haitaji muda mrefu wala mafunzo marefu ili aweze kwenda nje kutangaza na kushuhudia huo upendo. Kila Mkristo ni mmisionari kwa kiwango ambacho amekwisha kutana na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu.” Evangelii gaudium, 120. Baba Mtakatifu Francisko anaonesha matumaini kwamba, hatua zote hizi zitawawezesha waamini kuwa ni mahujaji wa kweli, daima wakiendelea kujiweka wazi kwa mshangao wa Mungu katika mapito ya maisha yao. Wawe tayari kusikiliza na kujibu sauti ya Mungu kwa njia ya sauti ya ndugu zao. Kwa njia hii wataweza kusaidiana kuinuka katika nyakati za taabu na mahangaiko makubwa katika historia; watakuwa ni mashuhuda wa matumaini mapya kwa ajili ya siku za usoni!