Tafuta

Jumuiya ya Heri za Mlimani, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, Jumatatu tarehe 17 Aprili 2023 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Jumuiya ya Heri za Mlimani, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, Jumatatu tarehe 17 Aprili 2023 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.  (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Heri za Mlimani: Ushuhuda wa Imani Katika Matendo

Jumuiya ya Heri za Mlimani, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, Jumatatu tarehe 17 Aprili 2023 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Amewapongeza kwa kukita maisha yao katika: Sala na Liturujia ya Kanisa, Muziki Mtakatifu na maisha ya udugu wa kibinadamu, kielelezo cha uwepo angavu wa Ufalme wa Mungu kati yao. Ni Jumuiya inayokazia: Sakramenti, Udugu, Upendo, Ukarimu na Huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Heri za Mlimani, “Comunità delle Beatitudini” muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Kristo Yesu inayosimika maisha na utume wake katika ari na mwamko wa kimisionari, ilianzishwa nchini Ufaransa kunako mwaka 1973, kama sehemu ya matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kielelezo cha ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na juhudi za Wakarisimatiki Wakatoliki. Jumuiya hii ilianzishwa na wanandoa wawili: Gerard Croissant (Ephraïm) na mke wake Jo, pamoja na Jean-Marc na Mireille Hammel ambao waliishi mang’amuzi ya Roho Mtakatifu, urafiki na ujirani wa Mwenyezi Mungu katika maisha na utume wao kama zilivyokuwa Jumuiya za kwanza za Wakristo zinazosimuliwa na Mwinjili Luka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. “Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.” Mdo 2: 46-47. Kardinali Robert Coffy, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Albi, aliitambua kama “Muungano wa Wachamungu.” Kunako Mwaka 2002 Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha likaitambua Jumuiya hii. Tarehe 29 Juni 2011 Askofu mkuu Robert Le Gall wa Jimbo kuu la Toulouse, aliipatia Jumuiya hii hadhi ya Kijimbo na hivyo kuwa chini ya Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume (CIVCSVA) na hatimaye, tarehe 8 Desemba 2020 ikapewa hadhi ya Kipapa. Takwimu za mwaka 2019 zinaonesha kwamba, kulikuwa na jumla ya wanachama 760 waliokuwa wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika nchi 51 huko Ulaya, Afrika, Asia, Marekani, Oceania na Mashariki ya Kati.

Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Heri za Mlimani
Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Heri za Mlimani

Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Baadhi ya wanajumuiya hawa wanatekeleza dhamana na wajibu wao kwenye Madhabahu yaliyoko nchini Ufaransa, Hungaria, Italia pamoja na Pwani ya Pembe. Mapadre wao wanahudumia katika Parokia mbalimbali ushuhuda angavu katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Hii ni Jumuiya ambayo imeanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi zinazoendelea hasa kwa huduma miongoni mwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto walemavu; familia maskini, maendeleo ya wanawake na ustawi wa jamii; chakula kwa maskini bila kusahau huduma ya afya kwa maskini na wale wasiojiweza, lengo ni kupambana na umaskini unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Jumuiya inasimikwa katika sala, sakramenti, liturujia na huduma
Jumuiya inasimikwa katika sala, sakramenti, liturujia na huduma

Jumuiya ya Heri za Mlimani, “Comunità delle Beatitudini” kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, Jumatatu tarehe 17 Aprili 2023 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Amewapongeza kwa kukita maisha yao katika: Sala na Liturujia ya Kanisa, Muziki Mtakatifu na maisha ya udugu wa kibinadamu, kielelezo cha uwepo angavu wa Ufalme wa Mungu kati yao. Mang’amuzi haya ya Kipentekoste yanawawezesha kujibidiisha daima kutafuta uwepo wa Mungu kati yao kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Maisha ya Sala kadiri ya tasaufi ya Wakarmeli na ile ya Makanisa ya Mashariki. Maisha haya ya sala ni chemchemi ya udugu wa kibinadamu unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na hivyo kutoa fursa ya kuendelea kustawi, kwa kila mmoja wao kadiri ya wito wake. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwawajali na kuwasikiliza watu wenye shida na changamoto za maisha, kielelezo cha wema na ukarimu hata kwa watalii na mahujaji wakati wa likizo ya kiangazi, majiundo ya sala, maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni nyenzo msingi katika majiundo ya watu wa Mungu huduma inayotolewa mjini Lourdes na Lisieux na sehemu mbalimbali za dunia. Huduma kwa mahujaji, wageni na watalii Nchi Takatifu na maeneo mengine ya sala; ni ushuhuda angavu wa mahusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu.

Umoja katika tofauti msingi msingi udugu wa kibinadamu
Umoja katika tofauti msingi msingi udugu wa kibinadamu

Hii ni huduma ya maisha ya wakfu inayosimikwa katika taamuli, sala na utume; mambo muhimu sana katika kukuza na kuendeleza majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni; kama sehemu ya mchakato wa kutafuta, kukuza na kudumisha amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu, mfano bora wa kuigwa na wengi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, maisha ya kijumuiya ni sehemu muhimu sana ya kumwilisha mshikamano na udugu wa kibinadamu; huu ni utambulisho muhimu sana wa Wakristo wanaohimizwa kutembea bega kwa bega, huku wakisaidiana na kupendana. Hii ndiyo nguvu ya maisha ya kitawa, kwa kushirikiana na kushikamana kidugu, katika sala na huduma makini kwa maskini. Huu ni mwaliko wa kusonga mbele katika maisha na utume wao kwa ari, moyo na nguvu mpya, daima wakiwa chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kutangaza na kushuhudia imani katika hali ya furaha na matumaini, daima wakijiaminisha chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa maisha na mchakato wa Uinjilishaji. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewachangamotisha wanachama hawa kuvalia njuga malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya; majadiliano ya kidini husasani na waamini wa dini ya Kiislam. Amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili daima waendelee kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya kuwa ni wanafunzi.

Jumuiya ya Heri
17 April 2023, 16:47