Msalaba ni Kitabu kikuu kinachosimulia huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wa nyakati zote. Msalaba ni Kitabu kikuu kinachosimulia huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wa nyakati zote.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

IJUMAA KUU: Mama Kanisa Anatangaza Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kwa Wafu

Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa katika mahubiri yake wakati wa Liturujia ya Neno la Mungu amesema, Kanisa katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, baada ya mageuzo linatangaza: Kifo na Kuutukuza Ufufuko wa Kristo Yesu mpaka atakapokuja tena.” Papa Francisko anasema Kristo Yesu hata katika hali ya upweke na kimya kikuu, aliendelea kuwapenda, kuwasamehe na kuwaombea watesi wake! Njia ya Msalaba Colosseo hatakuwepo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii maadhimisho ya Ijumaa kuu, tarehe 7 Aprili 2023 anasema, Kristo Yesu akiwa ametundikwa Msalabani, alikataa katukatu kujikatia tamaa, alimwomba na kukikabidhi kwa Baba yake wa mbinguni! Katika hali ya upweke, aliendelea kuwapenda, kuwasamehe na kuwaombea watesi wake, changamoto na mwaliko wa kuwa na moyo wa upendo kwa Wakristo wengi wanaoteseka na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Fumbo la Pasaka la Msalaba na Ufufuko wa Kristo Yesu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu ambayo Mitume na Kanisa wanaendelea kuitangaza na kuishuhudia, kama utimilifu wa Mpango wa wokovu kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao wokovu. Mababa wa Kanisa wanasema, imani inaweza kujaribu kutafuta mazingira ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu yaliyotajwa kiaminifu katika Injili na kutangazwa na kushuhudiwa na chemchemi nyingine za historia kusudi iweze kujua zaidi maana ya ukombozi. Rej. KKK 571-573. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 7 Aprili 2023 ameongoza Ibada ya Ijumaa Kuu kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ambayo imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Kuabudu Msalaba pamoja na Ibada ya Komunio Takatifu. Katika hali ya kimya kikuu, Baba Mtakatifu ameanza maadhimisho ya Ijumaa Kuu kwa kulala kifudifudi, alama ya anguko la Adamu na Eva na sababu ya mwanadamu kuendelea kuteleza na kuanguka dhambini kila wakati, kwa sababu alipoteza ile neema ya utakaso.

Ijumaa kuu: Mateso na Kifo cha Kristo Msalabani
Ijumaa kuu: Mateso na Kifo cha Kristo Msalabani

Kulala kifudifudi ni alama ya fedheha ya mwanadamu aliyoipata baada ya kuanguka dhambini na hatimaye, hiki ni kielelezo cha huzuni na mateso ya Mama Kanisa juu ya dhambi zinazoendelea kumsulubisha Kristo Yesu hata kwa nyakati hizi. Kimsingi hiki ni kielelezo cha mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Msalaba wa Kristo Yesu ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu, ni mahali ambapo wokovu wa binadamu umetundikwa juu yake, yaani Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha ufunuo wa huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa binadamu unaoweza kuonekana kana kwamba ni upuuzi mtupu kwa wasio amini. Kila mara mwamini anapoutazama Msalaba, anagundua upendo na huruma ya Mungu iliyotundikwa Msalabani. Msalaba ni Kitabu kikuu kinachosimulia huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wa nyakati zote. Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo Yesu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, uchoyo, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kulitafakari Fumbo la Msalaba linaloonesha sadaka na majitoleo ya Kristo Yesu hadi kifo cha aibu! Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia undani wa Fumbo la Msalaba. Ibada kwa Madonda Mtakatifu ya Yesu, iwawezeshe waamini kuzama katika Moyo wake Mtakatifu, ili kujifunza na hatimaye, kutambua Fumbo la maisha na utume wa Kristo Yesu; Ukuu na Hekima ya Msalaba, kitabu cha maisha kinachoendelea kuwaashangaza wengi.

Msalaba ni kitabu cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha
Msalaba ni kitabu cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha

Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa katika mahubiri yake wakati wa Liturujia ya Neno la Mungu amesema, Kanisa katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, baada ya mageuzo linatangaza: Kifo na Kuutukuza Ufufuko wa Kristo Yesu mpaka atakapokuja tena.” Ni katika muktadha huu, baadhi ya wanataalimungu waliona ugumu kudadavua “taalimungu ya kifo cha Mungu, baada ya wanafalsafa kama Nietzsche kuibuka na kutangaza kuhusu “Kifo cha Mungu.” Mama Kanisa kwa ujasiri na moyo mkuu kabisa, Ijumaa kuu anatangaza na kukiri kifo cha Kristo Yesu kiletacho wokovu na maisha ya uzima wa milele: “Ecce-homo”: “Tazameni Mtu.” Fumbo la Pasaka la Msalaba na Ufufuko wa Kristo Yesu ni kiini cha Habari Njema ya wokovu, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Ni katika Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, Mama Kanisa kwa ushupavu mkubwa anatangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kukiri pamoja na Kristo Yesu wakati anasulubiwa kwa kusema “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Lk 23:34. Huu ni ujumbe makini kwa watu wa vizazi vyote na wala si tu kwa wale waliokuwepo pale Mlimani Kalvari, ni maneno ya faraja kwa binadamu wa nyakati zote anasema Kardinali Raniero Cantalamessa, ni wakati wa kusimama kidete ili kutangaza na kushuhudia mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu toka kwa wafu, chemchemi ya neema, baraka, utakaso na maondoleo ya dhambi.

Msalaba ni Mti wa Ujumbe wa Matumaini
Msalaba ni Mti wa Ujumbe wa Matumaini

Binadamu anapaswa kutambua kwamba, kuna dhambi na ubaya wa moyo na wala wasikubali kudanganywa kama ilivyokuwa kwa Adamu na Eva “Nyoka akamwambia mwanamke, “Hamtakufa! Mungu alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Mwa 3:5. Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anataka kuhalalisha kila jambo na wala kwake dhambi na ubaya wa moyo ni mambo ya kufikirika! Hiki ni kiburi na majivuno ya mwanadamu! Kristo Yesu kwa njia ya mateso na kifo chake amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba.” Flp 2:6-8. Dhambi za binadamu ndizo zilizopelekea mateso na kifo cha Msalaba na kwamba, ufufuko wake kwa wafu ni chemchemi ya maisha mapya, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, unaowawezesha waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, tayari kutangaza “Kifo na Kuutukuza Ufufuko wa Kristo Yesu mpaka atakapokuja tena.”

Ijumaa kuu: Fumbo la Msalaba

 

 

07 April 2023, 17:44