Katika Misukosuko ya Maisha, Mkristo Anasaidiwa na Nguvu ya Upendo Mwaminifu wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Askofu mkuu Rolandas Makrickas, Kamishna Maalum wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Santa Maria Maggiore, anamtakia afya njema na baraka tele katika maisha na utumishi wake, akiongozwa na hekima na busara ya kichungaji kuangalia kile kinachopaswa kufanywa au kutofanywa; kubadilishwa au kuachwa jinsi kilivyo, lengo ni kuhakikisha kwamba, Mama Kanisa anajitahidi kumwilisha sheria ya Kristo Yesu ikusukumwa kwa namna ya pekee na upendo wa Kristo Yesu na jirani. Ajitahidi kuwa ni mpatanishi wa nafsi za watu pamoja na kuwahimiza kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anatambua na kuthamini majiundo yake kama Daktari wa Historia ya Kanisa aliyefunzwa na kurithishwa vyema roho ya imani, upendo na huruma sanjari na kupambwa na sifa njema katika maisha na utume wake katika shughuli mbalimbali alizokabidhiwa na Mama Kanisa katika diplomasia ya Kanisa huko nchini Giorgia, Sweden, Marekani, Gabon pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican. Bidii ya kazi na weledi ni mambo ambayo yamemtambulisha katika maisha na utume wake wakati wote huo.
Baba Mtakatifu Francisko anapenda kumhakikishia Askofu mkuu mpya Rolandas Makrickas, Kamishna Maalum wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu ushirikiano, upendo wenye subira na wema kwa ajili ya maslahi mapana ya Kanisa la Mungu; wanyenyekevu, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wote hawa watendewe na kuoneshwa wema mintarafu Sheria ya Kikristo: Yaani kukanya kwa roho ya upole, kwa kujiangalia nafsini, ili asije akajaribiwa mwenyewe kwani kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe, kumbe kutenda wema ni wajibu wa Kikristo. Rej. Gal 6, 1.4.10). Baba Mtakatifu amehitimisha salam zake za uteuzi kwa Askofu mkuu Rolandas Makrickas, Kamishna Maalum wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, kwa kumweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Maria Salus Populi Romani.” Kauli mbiu yake ya Kiaskofu ni: “Deus fidelis manet.” Huu ni mwaliko wa kukumbuka Fumbo la Pasaka: “Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.” 2 Tim 2:11-13. “Katika misukosuko ya maisha, na patashika nguo kuchanika” Mkristo anasaidiwa na nguvu ya upendo mwaminifu na usio na masharti wa Mwenyezi Mungu katika Yesu Kristo.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amekazia kuhusu: Moyo wazi, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu, huduma inayosimikwa katika umoja, ushiriki, utume wa Kanisa na upendo, kama mchungaji mwema, tayari kuwalinda waamini ambao ni dhaifu kwa imani. Awe ni kiongozi mwenye moyo wa ukarimu na uaminifu utakaomwezesha kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu, tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha “Amana ya Imani: “Fidei Depositum” inayohifadhiwa na Mama Kanisa, chachu ya utakatifu wa watu wa Mungu. Karama ya huruma itamwezesha Askofu mkuu mpya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuadhimisha Sakramenti za Kanisa chemchemi ya neema, baraka na utakatifu wa maisha, daima Kristo Yesu mchungaji mwema, akiwa mbele yake kama mfano bora wa kuigwa, aliyewatafuta kondoo “waliotokomea gizani”, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa wote hawa anapaswa kuwa ni: Kiongozi, Mchungaji mwema, Baba na Mwalimu wa watu wa Mungu. Kardinali Parolin amemkumbusha umuhimu wa kusimama imara katika misingi ya imani anapofundisha, ongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Awe mwaminifu na mdumifu katika misingi ya Injili ya Kristo. Amepakwa mafuta ya Krisma ya wokovu, amepewa pete ya kiaskofu kama alama ya uaminifu kwa Mungu, kielelezo cha ukamilifu wa imani, usafi wa maisha na ulinzi wa Kanisa, Mchumba mwaminifu wa Kristo Yesu. Kofia ya Kiaskofu, “MITRA” ni alama ya mng’ao wa utakatifu wa maisha, kielelezo cha Ufalme na shughuli za kichungaji.
Askofu mkuu Rolandas Makrickas katika salam zake za shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu pamoja na watu wa Mungu katika ujumla wao kwa zawadi ya uhai na Daraja Takatifu ya Upadre ambayo kwake imefikia utimilifu wake kwa kumweka wakfu kuwa Askofu mkuu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuwa mwaminifu katika ahadi zake na chemchemi ya neema na baraka katika maisha na utume wake na kwamba, anapenda kuendelea kuwa mwaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kumwimbia utenzi wa sifa na shukrani na utukufu, kwa baraka na neema zake zinazookoa! Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Rolandas Makrickas, Kamishna maalum wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, “Basilica di Santa Maria Maggiore, Saint Mary Major Basilica” alizaliwa tarehe 31 Januari 1972 huko Biržai, nchini Lithuania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 20 Julai 1996 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Panevėžys, lililoko nchini Lithuania. Tarehe 15 Desemba 2021 akateuliwa kuwa Afisa mwandamizi Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 11 Februari 2023 akamteuwa kuwa Askofu mkuu na Kamishna maalum wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma na kuwekwa wakfu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mkesha wa Sherehe ya Huruma ya Mungu, tarehe 15 Aprili 2023.