Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amebariki: Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa pamoja na kuweka wakfu Krisma ya Wokovu; Baba Mtakatifu Francisko amebariki: Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa pamoja na kuweka wakfu Krisma ya Wokovu;   (Vatican Media)

Alhamisi Kuu: Mmepakwa Mafuta Kumtangaza na Kumshuhudia Kristo Yesu

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake Alhamisi kuu 6 Aprili 2023 amekazia kuhusu uwepo wa Roho Mtakatifu anatenda kazi katika maisha na utume wa Kristo Yesu; Roho Mtakatifu aliyewashukia Mitume Siku ile ya Pentekoste wakapata ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Huyu ndiye Roho wa Imani, Ukweli, Faraja na Amani, changamoto na mwaliko kwa Mapadre kuwa ni mashuhuda wa wema na ukarimu wa Mungu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Alhamisi kuu tarehe 6 Aprili 2023 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amebariki: Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa pamoja na kuweka wakfu Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu. Hii ni Siku ya Ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo. Wakristo wanapakwa mafuta na kuwekwa wakfu kwa njia ya Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu baada ya kubatizwa Mtoni Yordani. Kumbe, kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara waamini wanatumwa kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kukuza na kudumisha: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, kwa hakika wao wanashiriki pia: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na chombo cha amani, maridhiano na upatanisho. Hii ni Sikukuu ya Mapadre na ni fursa ya kurudia tena ahadi za utii kwa Maaskofu mahalia. Kutokana na sababu za kichungaji, Majimbo mengi duniani, yaliadhimisha Sikukuu hii siku kadhaa zilizopita! Mama Kanisa anakiri na kufundisha kwamba, Roho Mtakatifu ni moja ya Nafsi za Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwenye uwamo mmoja na Baba na Mwana, “anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana.” Tangu mwanzo anaendelea kushiriki katika mpango wa wokovu wa mwanadamu hadi utimilifu wa nyakati au nyakati za mwisho zilizozinduliwa kwa njia ya Fumbo la Umwilisho; anayefunuliwa na kutolewa; kutambuliwa na kupokewa kama Nafsi. Mpango wa wokovu umetimilizwa kwa njia ya Kristo Yesu na kwa njia ya kummimina Roho Mtakatifu: Kanisa, ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili, na uzima wa milele.

Alhamisi Kuu: Mafuta ya Wakatekumeni, Wagonjwa na Krisma
Alhamisi Kuu: Mafuta ya Wakatekumeni, Wagonjwa na Krisma

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake kwa neno “Asante kwa Mapadre wote” kutokana na ushuhuda na huduma yao kwa watu wa Mungu; kwa kazi njema wanazotenda pasi na makuu wala kutaka kujimwambafai mbele ya watu; shukrani kwa wito, maisha na utume wa Kipadre wanaoutekeleza hata wakati mwingine kwa shida na magumu mengi, bila hata kutambuliwa wala kupewa shukrani. Katika mahubiri ya Alhamisi kuu kwa Mwaka 2023, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu uwepo wa Roho Mtakatifu anayetenda kazi katika maisha na utume wa Kristo Yesu; Roho Mtakatifu aliyewashukia Mitume Siku ile ya Pentekoste wakapata ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Huyu ndiye Roho wa Imani, Ukweli, Faraja na Amani, changamoto na mwaliko kwa Mapadre kuwa ni mashuhuda wa wema na ukarimu wa Mungu kwa waja wake. Baba Mtakatifu anasema Roho Mtakatifu ndiye Mhimili mkuu katika mchakato mzima wa Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Roho Mtakatifu ndiye mleta uzima na kwamba, miili yao ni hekalu la Roho Mtakatifu na kwamba, Roho Mtakatifu anaishi ndani ya Kanisa. Mapadre wamewekwa wakfu na Roho Mtakatifu, ili waweze kuwafundisha, kuwatakasa na kuwaongoza watu watakatifu wa Mungu. Roho Mtakatifu amekuwepo na amekua akitenda kazi katika maisha na utume wa Kristo Yesu, tangu alipotungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akabatizwa mtoni Yordani na kushuhudiwa na Roho Mtakatifu; na katika kuwahubiria na kuwaponya watu, nguvu za Roho Mtakatifu zilijionesha wazi. Ni katika muktadha huu, Mapadre walioteuliwa kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wamepakwa mafuta. Kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, walioacha yote na kuamua kumfuasa Kristo Yesu; wakaonesha udhaifu wao wa kibinadamu kama ilivyokuwa kwa Mtume Petro aliyethubutu kumkana Kristo Yesu mara tatu.

Alhamisi Kuu: Daraja Takatifu ya Upadre
Alhamisi Kuu: Daraja Takatifu ya Upadre

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, pengine, Mtume Petro alitarajia kuona mambo makubwa yakitendwa na Kristo Yesu na badala yake, mbele ya macho yake akakumbana na kashfa ya Msalaba, mateso na kifo cha Kristo, kiletacho wokovu na uzima wa milele. Sherehe ya Pentekoste, kwa Petro pamoja na Mitume wengine, ilikuwa ni mwanzo wa kuzaliwa upya katika maisha na utume wao! Wakatoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mitume Petro, Yohane na Yakobo wakayamimina maisha yao kama ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ndio mfano bora ambao Mapadre wanapaswa kuuiga na kuutolea ushuhuda. Wito wao wa kwanza unapaswa kuimarishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, ili kuvuka vipindi vya giza na mtikisiko wa imani kutokana: na kuishiwa nguvu, mchoko wa kazi na utume; mazoea pamoja na kukosa uaminifu na udumifu katika maisha, wito na utume wa Kipadre. Hiki ni kipindi ambacho Mapadre wote wanakipitia katika maisha na utume wao, anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hapa kuna kishawishi kikubwa cha Mapadre kujisahau na hatimaye, kujikuta wakiwa kama ni watu wa mshahara na hivyo kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kama Mapadre waliowekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa watu wateule wa Mungu.

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake Azizi
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake Azizi

Awamu ya pili katika maisha, wito na utume wa Mapadre, ni pale wanapojivika fadhila ya unyenyekevu na kukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu sanjari na kuupokea mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, tayari kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kumpokea na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu anataka kuwaambia nini, hasa pale anapogusa, kuganga na kuponya madonda ya udhaifu wao wa kibinadamu, mchoko na umaskini wa hali na kipato. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mbele ya macho yake, anayo idadi ya Mapadre wanaopambana changamoto katika maisha, wito na utume wa Kipadre, kiasi cha kujikatia tamaa ya kusonga mbele! Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Mapadre kama hawa ni kujivika ujasiri, tayari kusimama na kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo thabiti, tayari kujiaminisha chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu. Ni wakati wa kusimamia ukweli katika udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu na kuuweka mbele ya Roho Mtakatifu, Roho wa kweli anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika: wito, maisha na utume wa Kipadre na hivyo kumruhusu kuzamisha mizizi yake katika maisha yao. Ni Roho wa ukweli atakayewawezesha kulinda na kutunza wakfu wao na hivyo kuganga na kuwaponya dhidi ya ukosefu wa uaminifu wao, ili kusimama katika ukweli na haki. Mapadre wajifunze kumwachia nafasi Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili hatimaye, kuwakirimia amani na utulivu wa ndani katika maisha, wito na huduma yao kwa watu watakatifu wa Mungu. Amani na utulivu wa ndani vinasimikwa katika umoja kama lilivyo Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa umoja, ushiriki na utume wa Kanisa; mambo yanayosimikwa katika heshima, utu wema na unyenyekevu. Huu ni mwaliko kwa Mapadre wote kujizatiti katika ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa kwa kukazia utu wema, ili kwa njia ya Mapadre, watu waweze kumwona Kristo Yesu ndani ya maisha yao. Umoja na ushirika wa watu wa Mungu ni kielelezo cha uwepo wa Mungu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kuwashukuru Mapadre wote kwa wito, maisha na utume wao kwa watu wateule wa Mungu.

Papa Roho Mtakatifu
06 April 2023, 15:58