Tafuta

Francisko: Maadhimisho ya Juma kuu yawe ni chemchemi ya imani, mapendo na matumaini. Francisko: Maadhimisho ya Juma kuu yawe ni chemchemi ya imani, mapendo na matumaini.   (Vatican Media)

ALHAMIS KUU: Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na Huduma ya Upendo Katika Unyenyekevu

Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Alhamisi Kuu tarehe 6 Aprili 2023 anatarajiwa kubariki: Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa pamoja na kuweka wakfu Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu. Wakati wa Karamu ya Bwana, Papa Francisko katika Gereza la Watoto Watukutu atawaosha miguu vijana 12. Huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Siku tatu kuu za Pasaka, Mama Kanisa anaadhimisha Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Ni wakati muafaka kwa waamini kuomba fadhila ya: imani, matumaini, mapendo, toba na wongofu wa ndani ili kuweza kuadhimisha Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa na kutakaswa na Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima. Kwa njia ya Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, binadamu ameweza kukombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mateso na kifo cha Kristo Yesu kiwe ni chemchemi ya maisha mapya mintarafu tunu msingi za Kiinjili.  Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Alhamisi Kuu tarehe 6 Aprili 2023 anatarajiwa kubariki: Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa pamoja na kuweka wakfu Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu. Alhamisi kuu ni Siku ya Ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo. Wakristo wanapakwa mafuta na kuwekwa wakfu kwa njia ya Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu baada ya kubatizwa Mtoni Yordani. Kumbe, kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara waamini wanatumwa kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kukuza na kudumisha: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, kwa hakika wao wanashiriki pia: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na chombo cha amani, maridhiano na upatanisho. Hii ni Sikukuu ya Mapadre na fursa ya kurudia tena utii kwa Maaskofu mahalia. Katika miaka ya hivi karibuni, kumezuka kashfa ya matumizi mabaya ya “Mafuta Matakatifu.”

Alhamis Kuu: Daraja Takatifu ya Upadre
Alhamis Kuu: Daraja Takatifu ya Upadre

Ikumbukwe kwamba, mafuta ni alama ya ushirika, furaha, upendo na mshikamano. Kadiri ya Mapokeo ya Kanisa Katoliki, Mafuta Matakatifu ni alama ya imani inayoimarisha vifungo vya upendo kwa njia ya Roho Mtakatifu ili kushuhudia: Ukuu, uzuri na utakatifu wa familia ya Mungu inayowajibikiana. Mama Kanisa anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, kamwe hawatindikiwi na mafuta ya neema ya imani, matumaini na mapendo. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha na kuboresha maisha yao kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Matendo ya adili na ya huruma kwa maskini na wahitaji zaidi. Msalaba uwe ni ufunuo wa huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa binadamu. Na kwa Maadhimisho ya Ibada ya Kuweka wakfu Krisma ya Wokovu, Mama Kanisa anafunga rasmi kipindi cha Kwaresima na kuanza kujiandaa kuzama zaidi katika Mafumbo ya Kanisa. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Alhamisi Kuu: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu
Alhamisi Kuu: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuadhimisha Karamu ya Mwisho kwenye Gereza la Watoto watukutu la "Casal del Marmo" lililoko mjini Roma na kuwaosha miguu vijana 12. Baba Mtakatifu analenga kuragibisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, ili serikali na taasisi zinazohusika zijielekeze zaidi katika mchakato wa maboresho ya maisha ya wafunga na magereza yenyewe. Ibada ya kuwaosha vijana hawa miguu ni kielelezo cha unyenyekevu wa kibinadamu, ushuhuda wa upendo na ujirani mwema kwa kuwakum busha kwamba, wote ni ndugu wamoja, hata katika shida na mahangaiko ya ndani. Kumbe, kuna umuhimu wa kujikita zaidi katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata upya wa maisha. Baba Mtakatifu atawafuta vijana hawa kwa taulo ya huruma ya Mungu na kubusu miguu yao kama alivyofanya Kristo Yesu, kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, tayari kusimama kwa ujasiri na kusonga mbele katika maisha. Hili si busu la usaliti kama ilivyokuwa kwa Yuda Iskariote. Ili kupambana na changamoto za maisha, wachumi, watunga sera na wanasiasa hawana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwa namna ya pekee vijana na changamoto zao, kwa kuwawezesha kupata nyenzo zitakazowazuia kutumbukia katika mtandao wa uhalifu, kiasi hata cha kuwa ni “wahuni na vijana wa ovyo sana” katika jamii. Ni wajibu wa wazazi na walezi kutambua karama na vipaji vya watoto na vijana hawa, tayari kuviendeleza kwa njia ya shule makini, sanaa, muziki na michezo pamoja na kuwapatia fursa za ajira.  

Alhamisi Kuu: Huduma inayosimikwa katika unyenyekevu
Alhamisi Kuu: Huduma inayosimikwa katika unyenyekevu

Kwa mara ya kwanza, Baba Mtakatifu aliadhimisha Sherehe hii gerezani hapo kunako tarehe 29 Machi 2013, kwa kuwatia shime watoto na vijana hawa kusonga mbele kwa imani na matumaini mapya na kamwe wasitoe nafasi kwa mtu yoyote kuwapokonya matumaini walio nayo nyoyoni mwao. Matumaini haya yawasaidie kusonga mbele kwa kujiamini zaidi. Kijana mmoja mwenye ujasiri, alimuuliza Baba Mtakatifu Francisko, kwa nini aliamua kwenda kuwatembelea? Baba Mtakatifu alimjibu kijana yule kwa kusema kwamba, alijisikia kutoka katika undani wa moyo wake kwenda kuwatembelea na kuwafariji, kielelezo cha fadhila ya unyenyekevu na huduma inayopaswa kuoneshwa na Askofu. Baba Mtakatifu alisema wakati mwingine mambo ya maisha ya kiroho hayana maelezo ya kina, kwani huu ni msukumo kutoka katika undani wa mtu mwenyewe. Baba Mtakatifu Francisko aliwaomba vijana hawa ambao wanatumikia adhabu zao gerezani humo, kumwombea katika maisha na utume wake. Huu ndio ujumbe mahususi unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko si tu kwa ajili ya Magereza ya Italia, bali Magereza yote yanapaswa kuwa ni shule inayosaidia mchakato wa kuleta mabadiliko katika maisha ya mtu, ili baada ya kutumikia adhabu yake gerezani arudi na kujiunga tena na jamii akiwa ni mtu mwema. Magereza yasiwe ni mahali pa mateso na mahangaiko ya watu! Utu na heshima ya wafungwa viheshimiwe na kuthaminiwa, licha ya makosa yao, bado wanaendelea kuwa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Uragibisgahi wa maboresho ya maisha ya wafungwa na magereza
Uragibisgahi wa maboresho ya maisha ya wafungwa na magereza

Ni katika maadhimisho ya Alhamisi Kuu, Kristo Yesu akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbukumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai! Kumbe, Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu inayoadhimishwa na Mama Kanisa hadi Kristo Yesu atakaporudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti Pacha na Daraja Takatifu ya Upadre. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, wakitenda kwa nafsi ya Kristo, wakitangaza fumbo lake pamoja na kuyaunganisha maombi ya waamini pamoja na sadaka ya Kristo Msalabani inayoadhimishwa katika Ibada ya Misa Takatifu.

Papa Alhamis Kuu

 

05 April 2023, 15:30