Tafuta

Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya “Santa Maria huko Montevergine”  tarehe 28 Mei 2023 Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya “Santa Maria huko Montevergine” tarehe 28 Mei 2023  (Vatican Media)

Uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 900 ya Abasia ya S.Maria Montevergine, Italia: Ushuhuda wa Imani

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya “Santa Maria huko Montevergine” Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ili kuwa mwakilishi wake mkuu katika maadhimisho ya kufungua Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya “S. Maria huko Montevergine” Dominika tarehe 28 Mei 2023, Sherehe ya Pentekoste. Lengo ni kupyaisha ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kunako Karne ya 12, Enzi za Kati za Kikristo, Mtakatifu Guglielmo anayejulikana na wengi kama Mtume na hujaji alibahatika kuwa na utambuzi wa hali ya juu kabisa na ujasiri, kiasi hata cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kwa hakika, alikuwa ni kiungo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Nyakati za Kati. Aliongoza na kuratibu mageuzi kwenye Shirika la Wabenediktin, kwa kuwarejesha tena kwenye Mapokeo hai ya Mama Kanisa. Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Guglielmo anafananishwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyezamisha maisha yake kwa ajili ya huduma kwa maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ingawa alizaliwa miaka arobaini tu baada ya kifo cha muasisi wa Abasia ya Montevergine. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa ari kuu, imani na matumaini zaidi.

Jubilei ya Miaka 900 ya Abasia ya S. Maria, Montevergine.
Jubilei ya Miaka 900 ya Abasia ya S. Maria, Montevergine.

Katika hali na mazingira haya ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya “Santa Maria huko Montevergine” Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ili kuwa mwakilishi wake mkuu katika maadhimisho ya kufungua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya “Santa Maria huko Montevergine” Dominika tarehe 28 Mei 2023, Sherehe ya Pentekoste. Hili ni adhimisho linalohitimisha kipindi cha Pasaka ya Kristo Yesu kwa kummimina Roho Mtakatifu, Bwana na mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabududiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana, aliyenena kwa vinywa vya manabii; ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni siku ya kutafakari juu ya uwepo wa Roho Mtakatìfu katika Kanisa, maisha ya waamini na ni siku ya waamini kumwomba Roho Mtakatifu kuwaimarisha kwa mapaji yake saba na kuwajaza kwa matunda yake tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ndani na nje ya Italia. Hii ni siku ambayo Manispaa ya Mji wa Mercogliano, itatoa uraia wa heshima kwa Kardinali Pietro Parolin, kama ishara ya mwanzo wa maadhimisho haya yanayolenga kupyaisha ari na mwamko wa maisha na utume wa wamonaki hawa katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Parolin 900
27 March 2023, 14:35