Tafuta

Sakramenti ya upatanisho inaundwa na matendo makuu matatu: Kutubu, Kuungama na Kutimiza Malipizi. Kimsingi, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho yamefumbata kiini halisi cha Ukristo na Kanisa. Sakramenti ya upatanisho inaundwa na matendo makuu matatu: Kutubu, Kuungama na Kutimiza Malipizi. Kimsingi, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho yamefumbata kiini halisi cha Ukristo na Kanisa.  (Vatican Media)

Rehema Katika Mafundisho Tanzu, Maisha na Utume wa Kanisa!

Kimsingi, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho yamefumbata kiini halisi cha Ukristo na Kanisa: Mwana wa Mungu alijifanya mtu ili kutuokoa na aliamua kulihusisha Kanisa kama "chombo cha lazima" katika kazi hii ya wokovu, na ndani yake, wale aliowachagua, akawaita na kuwaweka wawe wahudumu wake. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume anafafanua maana ya Rehema katika: historia, mafundisho tanzu, maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja: Upendo, huruma na msamaha wa Mungu usiokuwa na mipaka, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya: imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima na kwa mwaka huu umeadhimishwa tarehe 17-18 Machi 2023. Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena, anapenda kuwakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo vya upatanisho, huruma na upendo wa Mungu, wajitahidi wao wenyewe kwanza kuwa waungamaji wazuri, ili hatimaye, waweze kuwa ni waungamishaji bora zaidi na kamwe, si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa upole na kwa umakini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina, kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake mintarafu Mahakama ya huruma ya Mungu. Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana”, ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu uliozinduliwa tarehe 8 Desemba 2015 na kuhitimishwa rasmi tarehe 20 Novemba 2016. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma ya Baba wa milele.

Rehema katika maisha, historia na mafundisho tanzu ya Kanisa
Rehema katika maisha, historia na mafundisho tanzu ya Kanisa

Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani. Ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu ambao ni kiini cha Injili; huruma ambayo kimsingi inapaswa kupenya na kugota katika nyoyo na akili za binadamu. Kanisa linapaswa kuwaendea wote pasi na ubaguzi kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni ushuhuda unaofumbata huruma ya Mungu, mwanga na njia inayowaelekeza watu kwa Baba wa milele! Huruma ya Mungu ni sehemu ya mpango wa maisha unaoleta furaha na amani ya ndani! Mapadre wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayoadhimishwa kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Upatanisho! Msamaha ni chombo kilichowekwa kwenye mikono dhaifu, ili kumwezesha mwamini kuachilia mbali hasira, ghadhabu, ukatili na kisasi ili kuishi kwa furaha, amani na utulivu wa ndani. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika zaidi ili watoto wake waweze kuwa na afya bora zaidi. Wakati umewadia kwa Mama Kanisa kuitikia kwa mara nyingine tena wito huu wa furaha na msamaha. Ni wakati wa kurejea kwenye msingi wa imani na kubeba madhaifu na mahangaiko ya jirani.

Msamaha wa kweli upate chimbuko lake katika akili na moyo wa mtu, ili kujenga amani
Msamaha wa kweli upate chimbuko lake katika akili na moyo wa mtu, ili kujenga amani

Huruma ya Mungu ni msukumo unaowaamsha waamini kwa maisha mapya na hivyo kuwatia ujasiri wa kuyaangalia ya mbeleni kwa imani, matumaini na mapendo. Msamaha wa dhambi zilizotendwa baada ya Ubatizo huondolewa kwa Sakramenti ya pekee iitwayo: Sakramenti ya uongofu, ungamo, kitubio na upatanisho. Sakramenti hii inaundwa na matendo makuu matatu: Kutubu, Kuungama na Kutimiza Malipizi. Kimsingi, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho yamefumbata kiini halisi cha Ukristo na Kanisa: Mwana wa Mungu alijifanya mtu ili kutuokoa na aliamua kulihusisha Kanisa kama "chombo cha lazima" katika kazi hii ya wokovu, na ndani yake, wale aliowachagua, akawaita na kuwaweka wawe wahudumu wake. Ni katika muktadha huu, Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume anasema, kuanzia tarehe 21-24 Machi 2023, Idara ya Toba ya Kitume inaendesha mafunzo ya ndani kwa ajili ya Majandokasisi na Mapadre wapya kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Zawadi ya Rehema Katika Moyo wa Fumbo la Ukombozi”: “Il dono dell’indulgenza: nel cuore del mistero della Redenzione.” Kozi hii maalum ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1990, ili kujibu changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Sakramenti ya Upatanisho na wahudumu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Kozi hii kwa sasa imeingia katika awamu yake ya thelathini na tatu, 33. Katika hotuba yake elekezi, Kardinali Mauro Piacenza, amefafanua maana ya “Rehema” mintarafu: Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Chimbuko na umuhimu wake kihistoria, katika maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji zinazoendeshwa na Mama Kanisa kwa ajili ya wokovu wa roho za watu na maisha ya uzima wa milele.

Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha na amani
Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha na amani

Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema Kamili. Rehema ni matunda ya kazi ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka. Mama Kanisa ndiye mhudumu na mlinzi mkuu wa Sakramenti ya Upatanisho. Kimsingi Kanisa ni Jumuiya ya watakatifu na wa dhambi wanaojitahidi kutubu na kumwongokea Mungu.

Mama Kanisa ndiye Mhudumu na mlinzi mkuu wa Sakramenti ya Kitubio
Mama Kanisa ndiye Mhudumu na mlinzi mkuu wa Sakramenti ya Kitubio

Utakatifu ni matokeo ya huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu, anayetakatifuza kwa kuwapenda waja wake na hivyo kuwakomboa kutoka katika udhaifu wao wa kibinadamu. Kwa njia ya Kristo Yesu, wote wanafanyika kuwa ni sehemu ya viungo vyake. Kumbe, furaha, mateso na mahangaiko ya mwanajumuiya mmmoja ni mahangaiko na mateso ya Kanisa zima. Ushirika wa watakatifu ni kiungo cha nguvu kiasi kwamba, hata kifo hakiwezi kuwatenganisha. Ushirika wa watakatifu ni muungano wa Kanisa la Mbinguni na Duniani. Ushirika wa watakatifu unawawezesha waamini kujisikia kwamba, wanao walinzi na waombezi mbinguni, wanaoweza kuzungumza nao mubashara. Watakatifu ni mifano bora ya maisha na tunu msingi za Kikristo, ndiyo maana waamini wanakimbilia, kuomba ulinzi na maombezi yao.

Rehema Katika Kanisa
21 March 2023, 14:42