Tafuta

Parokia ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini tayari kuinjilishwa na kuinjilisha. Parokia ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini tayari kuinjilishwa na kuinjilisha.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Parokia ni Kitovu cha Uinjilishaji wa Kina: Kiroho na Kimwili! Maparoko Kaeni Chonjo!

Papa amekazia: Umuhimu wa kuimarisha vyama mbalimbali vya kitume, ili kusaidia malezi, makuzi na majiundo ya watu wa Mungu kutoka katika medani mbalimbali za maisha. Parokia zijitahidi kuandaa Misa Maalum kwa ajili ya watoto, kama sehemu muhimu ya Katekesi kwa watoto kadiri ya hali na mazingira yao. Mapadre katika utume wao, wajenge moyo wa upendo, ari na ukarimu kwa watu wa Mungu na kamwe wasiwe kama watu wa mshahara, saa mkononi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania pamoja na mambo mengine, kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa na umuhimu wa Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, sehemu muhimu ya uinjilishaji wa Kanisa kwa ajili ya Kanisa linaloinjilisha. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni msanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia.” Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa.

Parokia: Sakramenti, Neno, Ushuhuda, Umoja na Upendo
Parokia: Sakramenti, Neno, Ushuhuda, Umoja na Upendo

Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji! Parokia ni mahali muafaka pa waamini wanajisikia kupenda na kupendwa; mahali pa kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara yaani wa kuwa ni: Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, wanapewa malezi na makuzi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Parokia ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha na utume wake.

Paroko ni kiungo muhimu katika maisha na utume wa Kanisa
Paroko ni kiungo muhimu katika maisha na utume wa Kanisa

Watu wote wa Mungu wanaitwa, wanatumwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika ari na mwamko mpya wa kimisionari. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 25 Machi 2023 amewapongeza wanaparokia kutoka katika Parokia ya “San Giovanni Battista” na “Sant’ Ambrogio ad Nemus in Passirana, huko Rho kutoka Jimbo kuu la Milano, Italia. Hizi ni Parokia ambazo kwa hakika ni mifano bora ya kuigwa kutokana na Paroko wao Monsinyo Michele Di Tolve, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, tangu hata bado akiwa ni Padre Gambera wa Seminari. Amekuwa ni mfano bora katika malezi na makuzi ya majandokasisi na waamini katika ujumla wao. Amekuwa ni mfano bora wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, linalowashirikisha waamini kila mtu kadiri ya nafasi, wito na dhamana yake, katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaofumbatwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa. Hii ni hija ya watu wa Mungu katika ujumla wao, wanaotembea kwa pamoja, hatua kwa hatua, kama kielelezo cha ushuhuda wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; imani na upendo thabiti ili kuvunjilia mbali upweke hasi unaowaandama watu wengi, hasa wale wanaoishi mijini.

Vyama na mashirika ya kitume yawe ni chachu ya uinjilishaji.
Vyama na mashirika ya kitume yawe ni chachu ya uinjilishaji.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujenga, kudumisha na kuimarisha vyama mbalimbali vya kitume, ili kusaidia malezi, makuzi na majiundo ya watu wa Mungu kutoka katika medani mbalimbali za maisha. Parokia zijitahidi kuandaa Misa Maalum kwa ajili ya watoto, kama sehemu muhimu ya Mapadre kutoa Katekesi kwa watoto kadiri ya hali na mazingira yao. Mapadre katika maisha na utume wao, wajenge moyo wa upendo, ari na ukarimu kwa watu wa Mungu na kamwe wasiwe kama watu wa mshahara, wanaopima utume wao kwa kuangalia saa mkononi! Waamini wajenge pia moyo wa ukarimu na upendo kwa jirani zao ambao ni wahitaji zaidi: kiroho, kimwili na kiutu. Adui mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Parokia ni: Ukosefu wa uaminifu kwa mali ya Kanisa, umbea na majungu yanayohatarisha mahusiano na mafungamano ya maisha ya familia, jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na Parokia katika ujumla wake. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewataka waamini Maparokiani, kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao katika ushuhuda wa mshikamano wa umoja, udugu na upendo. Kwa kuzingatia amani na ushiriki wa waamini wote katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Vijana na wazee wajenge utamaduni wa kukutana na kushirikishana amana na utajiri wao. Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, wawaombee ili hatimaye, waweze kuimarika katika imani, matumaini na mapendo thabiti.

Parokia na Uinjilishaji
27 March 2023, 15:17