Tafuta

Wanachama wa Chama Cha Kitaifa cha Waendeshaji wa Sanaa za Maonesho ya Kusafiri nchini Italia "Membri dell'Unione Nazionale Attrazionisti Viaggianti", tarehe 20 Machi 2023 wamekutana na Papa Francisko Wanachama wa Chama Cha Kitaifa cha Waendeshaji wa Sanaa za Maonesho ya Kusafiri nchini Italia "Membri dell'Unione Nazionale Attrazionisti Viaggianti", tarehe 20 Machi 2023 wamekutana na Papa Francisko  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko: Tangazeni na Kushuhudia Furaha ya Injili Kwa Watu wa Mataifa

Chama Cha Kitaifa cha Waendeshaji wa Sanaa za Maonesho ya Kusafiri nchini Italia, kwa njia ya utume wake, kimekuwa mstari wa mbele kutangaza furaha ya Injili, mwaliko kwa wasanii hawa kuhakikisha kwamba wanatekeleza utume huu mintarafu maisha ya kiroho, kama fursa ya watu wa Mungu kukutana na Kristo Yesu ambaye yuko katika Kanisa lake na anaendelea kutenda kazi. Huu ni utume unaowaletea watoto faraja na kumbukumbu ya matumaini kwa familia nyingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama Cha Kitaifa cha Waendeshaji wa Sanaa za Maonesho ya Kusafiri nchini Italia “Unione Nazionale Attrazionisti Viaggianti (UNAV). Kwa kifupi “UNAV”, kilianzishwa  kunako mwaka wa 1947. Chama hiki kinaundwa na Makampuni yanayofanya sanaa za maonesho katika bustani za burudani, katika muktadha wa usanikishaji wa vivutio katika bustani za majiji na miji. Chama hiki pia kina miliki mbuga za kitalii nchini Italia pamoja na michezo ya kuteleza nchini Italia. ANESV imekuwa na uhusiano wa karibu sana na Mfuko wa Wakimbizi wa Idara ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, “Fondazione Migrantes” uliowatia matumaini na shime ya imani, na hatimaye, kuweza kuvuka kipindi kile tete na kigumu kwa maisha ya watu wengi duniani. Chama kimekuwa kikitekeleza shughuli zake kwa kuhamahama, lakini kiliathirika sana wakati wa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, lakini kwa sasa kimeanza kucharuka tena kwa maonesho sehemu mbalimbali za Italia. Mwenyezi Mungu katika Maandiko Matakatifu daima amewahakikishia waja wake kwamba, “Naye BWANA, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.” Kum 31:8. Huu ni ujumbe wa faraja kwa watu wa nyakati zote.

Waamini watangaze na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa
Waamini watangaze na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” anasema, furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaoikubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya.” Evangelii gaudium, 1. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 20 Machi 2023 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Chama Cha Kitaifa cha Waendeshaji wa Sanaa za Maonesho ya Kusafiri nchini Italia kwa kifupi “ANESV.” Chama Cha Kitaifa cha Waendeshaji wa Sanaa za Maonesho ya Kusafiri nchini Italia, kwa njia ya utume wake, kimekuwa mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, changamoto na mwaliko kwa wasanii hawa kuhakikisha kwamba wanatekeleza utume huu mintarafu maisha ya kiroho, kama fursa ya watu wa Mungu kukutana na Kristo Yesu ambaye yuko katika Kanisa lake na anaendelea kutenda kazi. Huu ni utume unaowaletea watoto faraja na kumbukumbu ya matumaini kwa familia nyingi.

Sanaa za Maonesho ni chemchemi ya furaha kwa watoto wengi
Sanaa za Maonesho ni chemchemi ya furaha kwa watoto wengi

Furaha hii inapata chimbuko lake kutokana na kipaji cha ubunifu na uchangamfu unaosimikwa katika hali halisi ya maisha na hivyo kuacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi. Baba Mtakatifu anawataka wasanii, kuendeleza utume wao katika uhalisia wa maisha, kinyume kabisa cha kile ambacho watu wanaweza kukiona kwenye simu zao za mikononi au kwenye luninga. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza kutoka huko walikojichimbia ili kukutana na mashabiki wao barabarani, katika utekelezaji wa majukumu yao sanjari na kusherehekea furaha ya maisha, ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye anafurahia kuona watoto wake wakisherehekea kwa pamoja na ndugu zao katika hali ya kawaida. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewakabidhi wasaniii hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Msaada wa Wasafiri, anayewaongoza kumwendea Kristo Yesu, Mtakatifu Yohane Bosco, Msimamizi na mwombezi wao aendelee kuwategemeza kwa sala na maombi yake pamoja na Mtumishi wa Mungu Don Dino Torreggianti, Mtume wa wasanii.

Papa Sanaa Maonesho

 

20 March 2023, 14:46