Papa Francisko Mbele ya Mateso na Kifo Kazini: Kimya Kikuu na Huruma Vinatawala Zaidi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kunako tarehe 20 na 23 Aprili 2022 kulitokea ajali kwenye machimbo ya makaa ya mawe nchini Poland. Watu 5 walifariki dunia na wengine 17 walipotea katika mazingira ya kutatanisha. Familia za waathirika wa wafanyakazi hawa, Ijumaa, tarehe 24 Machi 2023 zimekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Amewashukuru kwa kumtembelea na kwamba, katika masikitiko na majonzi makubwa kiasi hiki kwa kuwapoteza wenzi wao wa maisha, ndugu na jamaa zao, anaishiwa nguvu na kukosa maneno ya kusema. Katika hali na mazingira kama haya busara inadai kimya kikuu kinachofumbatwa na kumwilishwa katika huruma. Kuwapoteza wapendwa katika mazingira ya kazi kama haya ni jambo la kusikitisha na huzuni kubwa.
Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwaonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili waweze kuupokea ukweli huu mchungu katika historia ya maisha yao. Katika majonzi makubwa kiasi hiki, kama mtu hana imani thabiti, anaweza kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu “ameziba masikio na kamwe hawezi kuwasikiliza.” Baba Mtakatifu amewatia moyo na kuwaambia kwamba, hata katika muktadha huu, hasira yao inageuka kuwa ni sala na tafakari ya kina juu ya Fumbo la kifo. Hata katika uvuli wa giza na mauti, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na waja wake. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake fupi kwa kuwahakikishia kwamba, anaendelea kuwakumbuka katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka yake.