Papa Francisko Asikitishwa na Maafa ya Tetemeko la Ardhi Nchini Ecuador na Peru
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Takwimu zinaonesha kwamba, watu 15 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 500 wamejeruhiwa kufuatia tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.8 katika kipimo cha Richter lililojikoteza nchini Ecuador na Perù, Jumamosi tarehe 18 Machi 2023. Tetemeko hili limesababisha madhara makubwa kwenye miundo mbinu; watu na mali zao hasa eneo la Kusini mwa mji wa Guayaquil. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika, tarehe 19 Machi 2023 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa tetemeko hili. Majeruhi waweze kupona haraka na hivyo kurejea tena kwenye shughuli zao za ujenzi wa Taifa. Marehemu wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa amani.
Rais Guillermo Lasso Mendoza, anawaalika wananchi wa Perù kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu katika historia ya maisha yao. Zaidi ya shule 80 pamoja na hospitali, vituo vya afya na zahanati zaidi ya 30 zimeharibiwa vibaya kutokana na tetemeko hilo kiasi cha kusababisha ugumu katika huduma kwa waathirika. Taarifa zinaonesha kwamba, hata Jumba la Makumbusho ya Taifa la Puerto Bolìvar limeharibiwa na tetemeko. Itakumbukwa kwamba, tarehe 16 Aprili 2016, takribani miaka saba iliyopita, Perù ilikumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha watu 670 kupoteza maisha yao!