Rais wa Malawi ametangaza siku 14 za Maombolezo ya Kitaifa kufuatia maafa makubwa yaliyosababishwa na kimbunga cha Freddy. Rais wa Malawi ametangaza siku 14 za Maombolezo ya Kitaifa kufuatia maafa makubwa yaliyosababishwa na kimbunga cha Freddy.   (ANSA)

Papa Francisko Asikitishwa na Maafa Makubwa ya Kimbunga cha Freddy Malawi na Msumbiji

Baba Mtakatifu Francisko anasali kwa ajili ya wale wote waliopoteza maisha, ili waonje huruma ya Mungu. Majeruhi waweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli zao za kila siku na wale wasiokuwa na makazi ya kudumu, wapate hifadhi na faraja katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko makubwa. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuziombea familia na jumuiya zilizoathirika kutokana na kimbunga hiki cha Freddy! Siku 14 za Maombolezo ya Kitaifa, Malawi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 15 Machi 2023 ameonesha ukaribu wake kwa njia ya sala na sadaka yake kwa watu wa Mungu nchini Malawi na Msumbiji waliopoteza maisha baada ya kukumbukwa na kimbunga cha kitropikali kijulikanacho kama Freddy. Baba Mtakatifu anasali kwa ajili ya wale wote waliopoteza maisha, ili waonje huruma ya Mungu. Majeruhi waweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli zao za kila siku na wale wasiokuwa na makazi ya kudumu, wapate hifadhi na faraja katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko makubwa. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuziombea familia na jumuiya zilizoathirika kutokana na kimbunga hiki cha Freddy!

Kimbunga cha Freddy kimesababisha maafa makubwa sana Malawi
Kimbunga cha Freddy kimesababisha maafa makubwa sana Malawi

Kwa upande wake, Rais Lazarus Chakwera wa Malawi, Jumatano, tarehe 15 Machi 2023 ametangaza siku 14 za Maombolezo ya Kitaifa kufuatia maafa makubwa yaliyosababishwa na kimbunga cha Freddy. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 15 Machi 2023 zaidi ya watu 225 walikuwa wamefariki dunia, watu 41 hawajulikani mahali walipo. Kimsingi nchini Malawi watu zaidi ya 59, 000 wameathirika vibaya sana na kwamba, wananchi 19, 000 hawana makazi maalum. Mafuriko yaliyoambatana na maporomoko ya udongo yamefukia na kuharibu makazi ya watu. Kiasi cha dola milioni 1.5 zimetolewa na Serikali ya Malawi, ili kuwasaidia wahanga wa janga hili la kitaifa. Serikali ya Malawi inaomba msaada wa dharura kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa kwa watu walioathirika na kimbunga na Freddy. Taarifa kutoka nchini Msumbiji zinaonesha kwamba, watu zaidi ya 20 wamefariki dunia nchini Msumbiji na kwamba, kuna majeruhi zaidi ya 24.

Papa Francisko asikitishwa na maafa makubwa Malawi na Msumbiji
Papa Francisko asikitishwa na maafa makubwa Malawi na Msumbiji

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na wadau wake wake wanaendelea kutoa misaada nchini Msumbiji na Malawi. Ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema, wakati mvua kubwa ikitarajiwa kuendelea kunyesha katika nchi hizo mbili kwa siku kadhaa zijazo, kuna hatari ya kutokea kwa mafuriko na maporomoko zaidi ya udongo ambayo yataathiri watu wengi zaidi na kutatiza shughuli za utoaji wa misaada. OCHA imesema msaada wa chakula, matibabu na vifaa mbalimbali vinavyohitajika, umesafirishwa kwenye vituo vya muda vya wahanga nchini Msumbiji na Malawi.

Papa Maafa Malawi
16 March 2023, 14:47