Misa ya Papa katika kumbukumbu ya miaka yake ya upapa.Heri kutoka CEI
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Habari za jioni ambayo Papa Fransisko alijiwasilisha kwa Kanisa na kwa ulimwengu mzima, miaka kumi iliyopita ilikuwa mwanzo wa mazungumzo na ambayo kwa wakati huu, yamesaidia kuelewa jinsi gani Injili inavyovutia, yenye ushawishi, yenye uwezo wa kujibu maswali mengi ya historia na kusikiliza maswali yanayojitokeza katika safu za uwepo wa mwanadamu. Haya ni maneno ya Kardinali Matteo Maria Zuppi, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Bologna na Rais wa Baraza la Maaskofu (CEI,) aliyoyatoa katika ujumbe kwa njia ya video kwa niaba ya maaskofu wote wa Italia kwa ajili ya kumpongeza kwa kuadhimisha miaka ya Upapa wake. Salamu za kheri na baraka za Uaskofu wa Italia, lakini ni pamoja na wengine wengi, zilizomfikia Papa Francisko, ambaye asubuhi tarehe 13 Machi 2023, kwa mujibu wa msemaji wa vyombo vya habari ametoa taarifa kuwa Papa aliongoza maadhimisho ya Ekaristi Takatifu katika Kanisa la Mtakatifu Marta, Vatican pamoja na Makardinali waliopo Roma.
Kwa hiyo tangu salamu hiyo ya jioni ya tarehe 13 Machi 2013, kwa mujibu wa Kardinali Zuppi, “yamekuwa maneno na ishara za Papa ambazo zimeendelea kugusa moyo, kwa mshangao, wa kuongea na watu wote. Papa Francisko, ametufundisha kutoka ndani na kwenda nje, kukaa katikati ya barabara na zaidi ya yote kwenda kwenye mitaa ili kuelewa sisi ni akina nani." Rais wa Cei ameongeza kusema: "Tunaweza kujijua wenyewe tu kwa kuangalia kutoka nje, kwenda katika mitaa kwanza ambayo ni masikini.” Kardinali Zuppi amebainisha kuwa: "Papa alituhimiza kukutana nao, kuwaona, kuwagusa, kuwafanya kuwa kaka na dada zetu wadogo zaidi, kwa sababu, kama Papa alivyokumbuka mara kwa mara, kuwa "imani yetu sio imani ya maabara, bali ni mchakato wa safari kupitia historia ambayo inafanyika kwa pamoja.”
Maaskofu wa Italia pia wamesisitiza shukrani zao kwa kukubali urithi wa Benedikto XVI na kwa kuwasindikiza, kuanzia Mwaka wa Imani na kuwatia moyo ili kuishi kama Wakristo katika migogoro mingi, changamoto na milipuko ya majanga ya ulimwengu huu. Ahadi iliyothibitishwa tena na Maaskofu ni “kufuatilia njia za amani kwa pamoja, kwa sababu ni amani tu itokayo kwa upendo wa kidugu na usio na ubinafsi inaweza kutusaidia kushinda migogoro ya kibinafsi, kijamii na kimataifa”.