Tafuta

Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu.   (Vatican Media)

Kwaresima Ni Kipindi cha Toba na Wongofu wa Ndani: Lengo Kuu ni Ushuhuda wa Utakatifu

Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwa wanaitwa kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Kwaresima ni fursa ya kuamsha na kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea wainjilishaji wote, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kile wanacho amini, kufundisha na kuadhimisha. Iwe ni fursa ya kugundua na kutambua kwamba, wao kama waamini ni Mitume wa Yesu, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha. Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji.

Kwaresima ya Kisinodi, kutembea na kusikilizana
Kwaresima ya Kisinodi, kutembea na kusikilizana

Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao. Mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Katekesi yake, Jumatano 29 Machi 2023.

Hiki ni kipindi cha kuambata na kushuhudia utakatifu
Hiki ni kipindi cha kuambata na kushuhudia utakatifu

Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ni ujumbe unaochota amana na utajiri wake kutoka katika tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro, kiasi cha kuambiwa na Kristo Yesu, alikuwa ni Shetani, kikwazo kwake kwani alikuwa hawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu. Rej. Mt 16:23. Kipindi hiki cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani Tabor ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho na kiutu, ili kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Kipindi cha Kwaresima
29 March 2023, 14:30