Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji yananogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki.” Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji yananogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki.”   (AFP or licensors)

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi Na Wahamiaji kwa Mwaka 2023

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki.” Kauli mbiu hii inapania pamoja na mambo mengine kukuza tafakari na ufahamu mpya kuhusu haki ya kuhama au kubaki nyumbani na katika nchi yako mwenyewe. Kuna sababu nyingi zinazowalazimisha watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao: Vita, Majanga asilia nk.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. LG 1. Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni kutokana na: mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na madhara makubwa ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu. Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kwa dhati kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha.

Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohatarisha sana maisha.
Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohatarisha sana maisha.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tangu mwaka 1952, Siku hii ilikuwa ikiadhimishwa Dominika baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Lakini kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko baada ya kusikiliza maoni na kuridhia maombi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia akaamua kwamba, Siku hii iadhimishwe Dominika ya mwisho ya Mwezi Septemba na kwa mwaka huu, inaadhimishwa tarehe 24 Septemba 2023.

Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji ziko hatarini
Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji ziko hatarini

Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki.” Kauli mbiu hii inapania pamoja na mambo mengine kukuza tafakari na ufahamu mpya kuhusu haki ya kuhama au kubaki nyumbani na katika nchi yako mwenyewe. Kuna sababu nyingi ambazo zinapelekea watu kulazimika kuyahama makazi nan chi zao, ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Haki ya kubaki nchini mwako ina mizizi yake katika maisha ya mwanadamu, kwani hii ni haki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni haki inayomwezesha mtu kuishi kwa kuzingatia utu, heshima na haki zake msingi na hivyo kujipatia pia maendeleo fungamani. Haki inapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji yananogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki” iwe ni fursa ya maandalizi ya kina kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani.

Wahamiaji 106

 

25 March 2023, 16:02