Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Dominika ya Matawi kwa mwaka 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Dominika ya Matawi kwa mwaka 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko Kuongoza Mwanzo wa Maadhimisho ya Mafumbo Makuu

Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Dominika ya Matawii, tarehe 2 Aprili 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwanzo wa kipindi cha Maadhimisho ya Juma kuu linalofumbata Mafumbo makuu ya wokovu wa mwanadamu, yaani: mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu. Hii inatokana na afya ya Baba Mtakatifu kuendelea kuimarika zaidi na Jumamosi, tarehe 01 Aprili 2023 anarudi tena Vatican. Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makatekista kutoka Tanzania wamtumia Papa Francisko salam na matashi mema. "Ninaitwa Padre Aurelian Mwinuka toka Jimbo Katoliki Njombe, nchini Tanzania, Afrika Mashariki. Nahudumu kama Mkuu wa Chuo cha Katekesi Madunda." Anasema, “Tumepokea Kwa mshituko habari za kudhoofika Kwa afya ya Baba Mtakatifu wetu Francisko kwa siku za hivi karibuni. Tunamwombea matashi mema kwa afya yake ili aendelee kuimarika na kuendelea kutuimarisha katika: imani na maadili sisi ndugu zake katika Kristo Yesu. Wanajumuiya ya Chuo cha Katekesi Madunda, Jimbo Katoliki la Njombe, tunamkabidhi Baba Mtakatifu Kwa maombezi matukufu ya Mama Bikira Maria aliye afya ya Wagonjwa ili Mungu Mwenyezi, mwingi wa huruma na mapendo amponye.” Hizi ni salam na matashi mema kutoka kwa Jumuiya ya Chuo cha Katekesi, Jimbo Katoliki Njombe kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye tangu Jumatano Alasiri, tarehe 29 Machi 2023 alipelekwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma kufanyiwa uchunguzi na kubainika kwamba, alikuwa anakabiliwa na changamoto katika mfumo wa hewa na kwamba, huu si Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Madaktari wakalazimika kumlaza Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya uchunguzi wa kiafya na matibabu zaidi, zoezi lililohitaji siku kadhaa na muda wa mapumziko na kwamba, Jumamosi, tarehe Mosi Aprili 2023 anatarajiwa kuruhusiwa na kurejea mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake kama kawaida, matendo makuu ya Mungu.

Hali ya afya ya Papa Francisko inaendelea kuimarika zaidi na zaidi.
Hali ya afya ya Papa Francisko inaendelea kuimarika zaidi na zaidi.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, Cnbb, linaungana na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, ili kwa maombezi ya Bikira Maria wa Aparecida, Mwenyezi Mungu aweze kumwiimarishia afya, ili aendelee kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Nalo Baraza la Maaskofu Katoliki Cyprus, linamtakia heri na baraka tele Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kupona haraka, ili aendeleze utume wake bila kuchoka kwa ajili ya watu wa Mungu. Taarifa kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, Ijumaa tarehe 31 Machi 2023 inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na madaktari tangu alipolazwa, unaonesha kwamba, afya yake inaendelea kuimarika zaidi. Kama hakutakuwa na mabadiliko mengine, Baba Mtakatifu anatarajiwa Jumamosi, tarehe Mosi Aprili 2023 kuruhusiwa kutoka Hospitalini kurejea kwenye makao yake, Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican Baba Mtakatifu ameendelea kula vizuri, huku akishirikiana na madaktari, wauguzi na walinzi wake, kama alama ya shukrani kwa Mungu. Anaendelea kusali, kutafakari, kujisomea na kufanya kazi kwa utulivu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Dominika ya Matawi kwa mwaka 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwanzo wa kipindi cha Maadhimisho ya Juma kuu linalofumbata Mafumbo makuu ya wokovu wa mwanadamu, yaani: mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu.

Papa Francisko Kuongoza Ibada Dominika ya Matawi 2023
Papa Francisko Kuongoza Ibada Dominika ya Matawi 2023

Taarifa ya kitabibu iliyotolewa Alhamisi tarehe 30 Machi 2023 inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alipata wasaa wa kulala vyema usiku na hali yake inaendelea kuimarika polepole. Baada ya kifungua kinywa na sala ya asubuhi, amejipatia nafasi ya kusoma baadhi ya magazeti na kuanza shughuli zake, akiwa hospitalini hapo. Kabla ya chakula cha mchana, amejitenga kwa sala binafsi na baadaye akapokea Ekaristi Takatifu. Katika siku za hivi karibuni, Baba Mtakatifu alianza kuhisi maumivu kwenye mfumo wa hewa na hii ikawa ni sababu muhimu ya kwenda kumfanyia uchunguzi wa kina, Jumatano tarehe 29 Machi 2023. Hadi wakati huu, uchunguzi na taarifa za madaktari zinasema kwamba, Baba Mtakatifu anaendelea vyema na wala hakuna sababu za msingi za kuhofia afya yake na kwa sasa anahudumiwa katika Idara ya Sayansi ya Magonjwa ya Moyo kwa kushirikiana na Idara nyingine kwa ajili ya uchunguzi wa kina, ili kuhakikisha kwamba, afya ya Baba Mtakatifu Francisko inatengamaa na hivyo kurejea tena katika maisha na utume wake. Itakumbukwa kwamba, Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 29 Machi 2023 imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu inayoonesha kiri ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayethibitisha kuhusu wito wake akisema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Huu ndio ushuhuda wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, akionesha shauku ya uinjilishaji na bidii ya kitume, baada ya kutubu na kumwongokea Kristo Yesu. Kutoka katika Torati akaikumbatia Injili; Yeye ambaye ambapo mwanzo alitaka kulidhulumu na kulibomoa Kanisa, sasa anakuwa ni shuhuda wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa, kiasi kwamba, sasa anataka kujisadaka kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.

Papa Francisko kuongoza Maadhimisho ya Mafumbo makuu ya Kanisa
Papa Francisko kuongoza Maadhimisho ya Mafumbo makuu ya Kanisa

Wakati wote wa Katekesi, Baba Mtakatifu alionekana kuwa mchangamfu isipokuwa pale aliponyanyuliwa ili kuketishwa kwenye kiti cha wagonjwa, alionekana kuhisi maumivu makali. Baadaye alipelekwa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, kwa gari la wagonjwa na kulazwa kwenye ghorofa yak umi, ambako kwa sasa macho na vyombo vya mawasiliano ya jamii vimejielekeza zaidi. Ni katika muktadha huu, shughuli zote za Baba Mtakatifu Francisko zilizokuwa zimepangwa zimefutwa hadi pale taarifa nyingine itakapotolewa. Uchunguzi uliofanywa na madaktari hadi sasa unaonesha kwamba, moyo wake unaendelea kufanya kazi vyema na kiasi cha oksijeni kwenye mzunguko wa damu kiko vyema. Madaktari walijielekeza zaidi kuangalia changamoto ya mfumo wa hewa pamoja na moyo. Matokeo yanaridhisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, limemtumia salam Baba Mtakatifu Francisko na kumhakikishia kwamba, watu wa Mungu nchini Italia, wanamwombea na kwamba, wanapenda kumzamisha kwenye huruma ya Mungu ili juhudi za madaktari na wauguzi ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kwake binafsi pamoja na wagonjwa wengine wote. Wakati huo huo, familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma, inapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye amelazwa na hivyo kumwombea neema, baraka na huruma ya Mungu ili aweze kumponyesha haraka, na kuwajalia pia nafuu na hatimaye uponywaji wagonjwa wote wanaoteseka hospitalini na majumbani, sehemu mbalimbali za dunia.

Salam na matashi mema kutoka kwa watu wa Mungu Brazili
Salam na matashi mema kutoka kwa watu wa Mungu Brazili

Wakati huo huo, Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican yapatayo 183, katika salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu anasema kwa niaba yake na wanadiplomasia wote wa Vatican, wanamtakia uponywaji wa haraka. Ni matumaini ya wanadiplomasia kwamba, Mwenyezi Mungu ataweza kumjalia afya njema na hatimaye, kurejea tena mjini Vatican, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na uzuri wa imani. Taarifa ya kuugua na hatimaye, kulazwa kwa Baba Mtakatifu Francisko zimeenea kwa haraka sana sehemu mbalimbali za dunia. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 majira ya jioni alilazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma kwa ajili ya kufanyia operesheni kubwa kwenye utumbo mpana. Operesheni hiyo ilifanywa na Prof. Sergio Alfieri. Kabla ya kwenda kufanyiwa operesheni kubwa, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili alisali na kutafakari na waamini pamoja na mahujaji waliofika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuhusu “Kashfa ya Fumbo la Umwilisho.” Kwa sasa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kumkumbuka na kumwombea, ili kazi hii ya madaktari ipate kibali na hitimisho lake kwa baraka za Mwenyezi Mungu! Radio Vatican itaendelea kukujuza hali ya Baba Mtakatifu Francisko kadiri taarifa zitakavyokuwa zinatolewa na Hospitali ya Gemelli. Historia inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko na Mtakatifu Yohane Paulo II ndio viongozi wakuu wa Kanisa katika miaka ya hivi karibuni kulazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, kiasi kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, Hospitali ya Gemelli kwake ni Ikulu Ndogo ya Tatu, ya Pili kwa wakati ule ilikuwa ni Castel Gandolfo ambayo kwa sasa imegeuzwa kuwa ni eneo la kitalii.

Papa Gemelli
31 March 2023, 17:52