Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.”  

Ujumbe wa Papa Francisko Kipindi cha Kwaresima 2023: Toba na Mchakato wa Sinodi

Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2023: Kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ni ujumbe unaochota utajiri wake kutoka katika tukio la Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Kwaresima “Quadragesĭma” kinaanza rasmi kwa Jumatano ya Majivu 22 Februari hadi tarehe 5 Aprili 2023. Kwaresima ni kipindi cha safari ya Siku 40 katika jangwa la maisha ya kiroho, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani tayari kuadhimisha kiini cha Fumbo la Wokovu wa mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu yaani Fumbo la Pasaka. Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ni ujumbe unaochota amana na utajiri wake kutoka katika tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro, kiasi cha kuambiwa na Kristo Yesu, alikuwa ni Shetani, kikwazo kwake kwani alikuwa hawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu. Rej Mt 16:23.

Kwaresima ni kipindi cha Kupanda Mlimani Tabor na Yesu.
Kwaresima ni kipindi cha Kupanda Mlimani Tabor na Yesu.

Kipindi hiki cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho, ili kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kisinodi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wanapaswa kuondokana na maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa mazoea, na hivyo anawaalika kupanda juu mlimani, ili kumsindikiza Kristo Yesu na hivyo kupata mang’amuzi ya ndani kabisa ya nidhamu ya maisha ya kiroho, kama watu watakatifu wa Mungu. Toba ya Kwaresima kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi inaimarishwa kwa neema ili kuondokana na utepetevu wa imani na kashfa ya kutokubali kumfuasa Kristo Yesu katika Njia yake ya Msalaba, kama Mtakatifu Petro na wenzake, walivyotaka kufanya!

Kwaresima ni kipindi cha Tafakari ya kina ya Maandiko Matakatifu
Kwaresima ni kipindi cha Tafakari ya kina ya Maandiko Matakatifu

Huu ni muda muafaka wa ukombozi, unaomwezesha mwamini kuzama na kukumbatia Fumbo la Wokovu linalosimikwa katika sadaka binafsi inayoongozwa na upendo, kwa kujiondoa katika anasa na mambo yasiyo na msingi. Huu ni wakati wa kukwea kwenda mlimani, jambo linalohitaji: nguvu, sadaka, majitoleo na umakini na hivyo kupata fursa ya kuweza kutafakari uhusiano uliopo kati ya toba ya Kwaresima na mang’amuzi ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Aliwa juu mlimani, Kristo Yesu anawateuwa Mitume wake watatu ili waweze kuwa ni mashuhuda amini wa tukio maarufu katika maisha na utume wake, tayari kukabiliana uso kwa uso na Fumbo la Msalaba. Kristo Yesu alipenda kuhakikisha kuwashirikisha wafuasi neema ya tukio lake la kugeuka sura kama jumuiya kwani hata imani ni mang’amuzi ambayo waamini wanashirikishana kwa pamoja. Kama waamini, wanapaswa kutembea bega kwa bega na waamini wenzao, kuelekea kwenye Mlima Tabor, ndiyo maana Kwaresima ya Mwaka 2023 ni sehemu ya mchakato wa Sinodi, wakiwa wameambatana na Kristo Yesu, Mwalimu wao, ambaye kimsingi ni: Njia, Ukweli na Uzima. Kumbe, hija hii ya Kiliturujia ni sehemu muhimu sana ya Kanisa inayopania kuzama katika Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani
Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani

Kilele cha hija ya Kristo Yesu pamoja na Mitume wake pale juu mlimani ni kugeuka sura na kuonesha mng’ao wa utukufu wake. Wakati wa mchakato wa maadhimisho ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, safari hii inaweza kuonekana kuwa ni ngumu na inayokatisha tamaa, lakini ni jambo la msingi kuendelea na safari ili kutambua vyema mapenzi ya Mungu na utume wa waamini katika huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Safari hii, ilirutubishwa kwa uwepo wa Yesu, Musa na Eliya, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii. Kristo Yesu anatimiza yote haya kwa kuweka Agano Jipya na la milele. Hivi ndivyo ilivyo pia katika maadhimisho ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, unaojikita katika Mapokeo ya Kanisa na hivyo pia kuwa tayari kupokea mambo mapya yanayojitokeza kwa kusoma alama za nyakati na hivyo kuepukana na kishawishi cha kutenda kwa mazoea. Malengo ya Hija ya Toba ya Kwaresima na mchakato wa Sinodi ni kwa ajili ya mwamini binafsi na Kanisa katika ujumla wake na yote haya yanapatikana kwa neema ya Fumbo la Pasaka, huku wote wakiwa wanaambatana na Kristo Yesu. Hatua ya kwanza kabisa ni: Kumsikiliza Kristo Yesu anapozungumza nao kwa njia ya Neno la Mungu linalotolewa na Mama Kanisa wakati wa maadhimisho ya Liturujia Takatifu, katika Ibada ya Misa Takatifu.

Kwaresima ni wakati wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu
Kwaresima ni wakati wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu

Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu hata kwa njia ya msaada wa vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na waja wake kwa njia ya maskini na wale wote wanateseka kwa sababu mbalimbali za maisha. Mchakato wa maadhimisho ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, hauna budi kusimikwa katika utamaduni wa: majadiliano na kusikilizana, kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi. Pili, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukabiliana na hali mbalimbali za maisha yao kwa ujasiri, ari na moyo mkuuu bila kutaka kutafuta njia ya mkato, kwani mng’ao wa utukufu wa Kristo Yesu, ni ishara ya ushiriki wao katika utukufu wa Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Safari ya Kipindi cha Kwaresima inawawezesha waamini kusherehekea Ufufuko wa Kristo Yesu. Hii ni fursa kwa waamini kujiandaa kikamilifu kuadhimisha Fumbo la Pasaka kwa kushiriki katika Njia ya Msalaba kwa imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, kusherehekea Ufufuko uletao wokovu.

Ni wakati wa kushiriki Njia ya Msalaba pamoja na Yesu
Ni wakati wa kushiriki Njia ya Msalaba pamoja na Yesu

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2023 anakaza kusema, mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, waamini wanapokirimiwa neema, wanapata nguvu na mang’amuzi ya ujenzi wa ushirika, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Huu ni wakati wa kujizatiti na kusonga mbele ili mang’amuzi ya kipindi hiki yawawezeshe waamini kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa mchakato wa Sinodi katika uhalisia wa maisha ya kawaida. Roho Mtakatifu mleta uzima, awaongoze na kuwasimamia waamini katika kipindi hiki cha Kwaresima, ili waweze kukwaa kwenda juu mlimani huku wakiwa wameandamana na Kristo Yesu, ili kupata mang’amuzi ya ukuu na utukufu wake, ili hatimaye, aweze kuwaimarisha katika imani, na kuwajalia uvumilivu wa kusonga mbele pamoja na Kristo Yesu kwa ajili ya utukufu wa watu wake na mwanga kwa Mataifa.

Papa Ujumbe wa Kwaresima 2023

 

22 February 2023, 16:53