Tafuta

Takriban watu zaidi ya 5, 000 wamefariki dunia nchini Uturuki na Siria kutokana na tetemeko la ardhi lililozikumba nchi hizi mbili Jumatatu tarehe 6 Februari 2023. Takriban watu zaidi ya 5, 000 wamefariki dunia nchini Uturuki na Siria kutokana na tetemeko la ardhi lililozikumba nchi hizi mbili Jumatatu tarehe 6 Februari 2023.  (AFP or licensors)

Tetemeko la Ardhi Uturuki na Siria: Masikitiko Na Sala ya Papa Francisko Kwa Wahanga

Takriban watu zaidi ya 5, 000 wamefariki dunia nchini Uturuki na Siria kutokana na tetemeko la ardhi; kuna zaidi ya watu 24,000 wanaohusika na jitihada za uokoaji, Inakadiriwa kwamba, kuna watu zaidi 4, 300 ambao hawajulikani mahali walipo. Majumba 5,775 yameporomoka na WHO inakadiria kwamba, zaidi ya watu milioni 23, wakiwemo watoto zaidi ya milioni moja wameathirika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taarifa zinaonesha kwamba, takriban watu zaidi ya 5, 000 wamefariki dunia nchini Uturuki na Siria kutokana na tetemeko la ardhi lililozikumba nchi hizi mbili hadi kufikia Jumanne tarehe 7 Februari 2023 mchana. Katika kipindi cha saa 24 zilizopita Uturuki imekumbwa na matetemeko mengine madogo zaidi ya 81. Taarifa inaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 24,000 wanaohusika na jitihada za uokoaji, ingawa kadiri muda unavyozidi kuyoyoma, matumaini ya kupata watu wakiwa hai yanafifia. Inakadiriwa kwamba, kuna watu zaidi 4, 300 ambao hawajulikani mahali walipo na jitihada za kutaka kuokoa maisha yao zinaendelea. Majumba 5,775 yameporomoka na Shirika la Afya Duniani linakadiria kwamba, zaidi ya watu milioni 23, wakiwemo watoto zaidi ya milioni moja wameathirika kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu tarehe 6 Februari 2023 kati ya Uturuki na Siria. Makali yake yamesikika pia nchini Lebanon na Israeli.

Mshikamano wa Papa Francisko na waathirika wa tetemeko la ardhi.
Mshikamano wa Papa Francisko na waathirika wa tetemeko la ardhi.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Marek Solczyński, Balozi wa Vatican nchini Uturuki na kwa Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria, anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Uturuki na Siria uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake kwa wale wote walioathirika kwa tetemeko hilo ambalo limesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Anawaombea marehemu wote waweze kupata huruma ya Mungu na wapumzike kwenye usingizi wa amani. Salam za rambirambi ziwafikie wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Wagonjwa na majeruhi wapate tiba, wapone na kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Jitihada za kuokoa maisha zinaendelea kwa matumaini kidogo
Jitihada za kuokoa maisha zinaendelea kwa matumaini kidogo

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea watu ambao wamejisadaka kwa ajili ya kuwaokoa wale waliofukiwa na kufunikwa na kifusi cha majengo, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo awafanyie wepesi katika shughuli zao, kwa kuwakirimia nguvu, udumifu na amani katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha yao. Wakati huo huo, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Mashirika mbalimbali ya Misaada ya Kanisa Katoliki yameanza kupeleka msaada wa fedha na mahitaji muhimu kwa waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Siria. Lengo ni kujenga mtandao wa mshikamano wa udugu katika huduma kwa waathirika wa tetemeko hilo la ardhi ambalo kadiri ya takwimu linaonekana kuwa na madhara makubwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Tetemeko ardhi 2023

 

07 February 2023, 14:41