Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani tarehe 11 Februari 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.” Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani tarehe 11 Februari 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.”   (Vatican Media)

Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Roma: Injili ya Msamaria Mwema: Kilio cha Wagonjwa

Papa Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani, 11 Feb. 2023 amekutana na wahudumu wa shughuli za kichungaji kwa wagonjwa kutoka Jimbo kuu la Roma na kuwataka kujihusisha zaidi na wagonjwa, kwa kujenga ujirani mwema, kuwapatia sauti, ili waweze kusikilizwa na kwamba, huduma kwa wagonjwa ni ushirika katika Injili ya upendo kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, kwa Mpako Mtakatifu wa wagonjwa na sala za Makuhani, Mama Kanisa huwakabidhi wagonjwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa na kutukuzwa ili awainue na kuwaokoa. Mama Kanisa anawaalika wagonjwa na wazee kujiunga kwa hiari na mateso na kifo cha Kristo Yesu, ili kutoa mchango wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Rej. KKK. 1499. Mpako wa wagonjwa hutimiliza kufananishwa kwa waamini kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kama Sakramenti ya Ubatizo inavyoanza. Siku ya Wagonjwa Duniani, ni wakati wa kusali na kuwaombea wagonjwa na familia zao; kwa kuwaenzi wahudumu katika sekta ya afya pamoja na watu wanaojitolea usiku na mchana, kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na wazee sehemu mbalimbali za dunia. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wito wa huduma ya afya, ili kuweza kuwasindikiza wagonjwa na wanaoteseka katika shida na mahangaiko yao. Ni fursa kwa Kanisa kupyaisha tena na tena huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni siku ya Sala, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Sakramenti ya Mpako kwa wagonjwa na wazee. Itakumbukwa kwamba, Siku ya Wagonjwa Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 13 Mei 1992 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes nchini Ufaransa kunako tarehe 11 Februari 1993.

Maadhimisho ya Siku ya 31 Mjini Roma
Maadhimisho ya Siku ya 31 Mjini Roma

Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023 inaadhimishwa Jumamosi tarehe 11 Februari 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.” Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!  Kanisa linaweka mbele ya macho ya waamini Mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema.

Injili ya Msamaria mwema ni huruma ya upendo wa Mungu
Injili ya Msamaria mwema ni huruma ya upendo wa Mungu

“Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Lk 10: 25-37. Ni katika mkutadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 9 Februari 2023 kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023 amekutana na kuzungumza na wahudumu wa shughuli za kichungaji kwa wagonjwa kutoka Jimbo kuu la Roma na kuwataka kujihusisha zaidi na wagonjwa, kwa kujenga ujirani mwema, kuwapatia sauti, ili waweze kusikilizwa na kwamba, huduma kwa wagonjwa ni ushirika katika Injili ya upendo. Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi na wahudumu katika sekta ya afya kutengeneza ujirani mwema, kwa kuwasikiliza kwa makini, kwa kuwapenda na kuwakarimia. Wajifunze kuona na kuonja mateso na mahangaiko ya wagonjwa, tayari kuwahudumia kwa huruma na mapendo, mchakato unaowahusisha wadau wote yaani wahudumu pamoja na wagonjwa wenyewe. Kwa kutembea huku wakiwa wameshikamana kama dhana ya Sinodi inavyoelekeza ni kuwa na mang’amuzi thabiti ya maana ya maisha na upendo wa kweli.

Mshikamano na wagonjwa ni muhimu sana
Mshikamano na wagonjwa ni muhimu sana

Baba Mtakatifu anawataka wawe ni sauti ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kuzungumza na kujitetea. Hawa ni wale maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kukosa nguvu za kiuchumi na kimaadili na matokeo yake ni kupoteza pia imani, hasa kwa wagonjwa wanaoteseka kwa magonjwa ya muda mrefu. Huu ni mwaliko wa kujenga mtandao wa huduma inayookoa, inayowawezesha watu kufanya kazi katika umoja na ushirika; watu wanaoshikamana katika huduma na upendo unaoboreshwa kwa maisha ya sala na ujasiri wa kuwaunganisha wahudumu wa sekta ya afya, wagonjwa na watu wa kujitolea kwa kutambua kwamba, viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. Rej. 2Kor 12: 12-27. Kila mtu apokelewe kwa upendo na ukarimu kama kielelezo cha baraka ya Mungu. Kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa. Wanapokutana kutana na vikwazo, iwe ni fursa kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, kielelezo cha Injili ya huruma na upendo kwa wagonjwa na wahitaji. Baba Mtakatifu anawataka wagonjwa kuishi mateso na mahangaiko yao ya ndani kwa imani, matumaini na mapendo. Watambue kwamba, wao wanao upendeleo mkubwa mbele ya Mungu. Waendelee kujikita katika sala na kujenga ujirani mwema pamoja na wagonjwa wenzao, ili kilio cha wagonjwa kiweze kusikilizwa na kupewa majibu muafaka. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume, tayari kuadhimisha vyema Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023.

Injili ya Msamaria Mwema
09 February 2023, 15:24