Papa Francisko:Yesu anaendelea kubisha hodi katika Kanisa,lakini halitoki nje kufungua
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Mungu yuko anaonesha Kanisa njia ya umoja, ya kutembea pamoja, ambayo ni mwaliko wa kushinda njia zinazofanana lakini ambazo hazikutani kamwe. Amesema hayo Baba Mtakatifu alipokutana Jumamosi tarehe 18 Februari 2023, katika Ukumbi mpya wa Sinodi, mjini Vatican marais na wawakilishi wa Tume za Walei wa Mabaraza ya Maaskofu ulimwenguni ambao wameshiriki Kongamano la Kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Likiongozwa na tema: “Wachungaji na Waamini walei walioitwa kutembea pamoja”, “Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa hiyo amebainisha kuwa ili kufanya hivyo, kuna haja ya kuwathamini walei ambao haitegemei mambo mapya ya kitaalimungu bali inategemea maono sahihi ya Kanisa, yale ya Kanisa kama Watu wa Mungu, ambalo walei ni sehemu kamili ya sifa pamoja na wahudumu waliowekwa wakfu. Kwa upande wa Baba Mtakatifu ametoa, mwaliko kwa washiriki takriban mia mbili walioshiriki ili kurejesha umuhimu wa kikanisa ambalo inaweka msisitizo juu ya umoja na sio utengano, ambapo mlei sio asiye na dini, bali aliyebatizwa, na neno la mwanafunzi, ndugu, kama linavyotumika katika Agano Jipya kwa wote, wahudumu waamini na waliowekwa wakfu.
Kushinda njia za kutenda kwa kujitegemea
Baba Mtakatifu Fransisko kwa maana hiyo amewakumbusha wale waliohudhuria kongamano hilo kwamba bado kuna mchakato wa njia ndefu ya Kanisa ili liweze kuishi kama mwili, kama watu wa kweli, lakini ni Mungu anayeonesha njia ya kufuata mbele, ile ya kuishi kwa bidii zaidi na kwa uthabiti zaidi katika umoja. Kwa maana hiyo Askofu wa Roma alizungumza juu ya njia nyingi zinazofanana ambazo hazijakutana kamwe na ambazo tumeitwa kuzishinda. Njia hizo ni Makasisi waliojitenga na walei, watawa waliotengana na makleri na waamini, imani ya kiakili kwa baadhi ya wasomi waliojitenga na ibada za imani za watu wengi, Curia Romana iliyojitenga na Makanisa mahalia, maaskofu waliojitenga na mapadre, vijana waliojitenga na wazee, wanandoa na familia kushiriki kidogo katika maisha ya Jumuiya, harakati za kikarismatiki zilizotengana na parokia na mengine mengi. Hilo ndilo jaribu zito zaidi kwa sasa, Papa Francisko amesisitiza.
Watu walioungana katika utume huamsha shauku ya kutembea pamoja
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake alisisitiza jinsi gani Watu wote wa Mungu wameunganishwa na imani moja, kwa hiyo wao sio aina ya vyama vya watu au vya wasomi, lakini ni watu waamini Watakatifu wa Mungu ambao wanahuishwa na utakaso sawa na mwelekeo ili kuelekea utume uleule wa kutangaza upendo wa huruma ya Mungu Baba. Kipengele hicho cha mwisho, cha kuunganishwa katika utume, ndicho chenye maamuzi stahiki, ambapo Sinodi inapata chimbuko na dhamira yake kuu katika utume . Hapo unazaliwa utume na kuelekezwa katika utume. Kwa hakika, kushirikisha utume Baba Mtatifu amesisitiza kuwa, hunawaleta karibu wachungaji na walei zaidi, huzaliwa muungano wa nia, hudhihirisha ukamilishano wa karama mbalimbali na kwa hiyo huamsha kwa kila mtu shauku ya kutembea pamoja.
Mifano haikukosekana kuanzia na ya Kristo hadi kufikia ya Mtakatifu Paulo na tena katika wakati mkuu uzinduzi wa kimisionari wa Kanisa, Baba Mtakatifu amesma kuwa tunaiona kwa Yesu mwenyewe, ambaye alizungukwa, tangu mwanzo, na kundi la wanafunzi, wanaume kwa wanawake, na kuishi huduma yake ya hadharani pamoja nao. Kamwe hakuwa peke yake. Na alipowatuma wale Thenashara kutangaza Ufalme wa Mungu, aliwatuma wawili wawili. Kwa hiyo amesema tunaona jambo lile lile kwa Mtakatifu Paulo, ambaye alihubiri daima pamoja na washirika wake, hata walei na wanandoa. Yeye hakuwa peke yake. Na ndivyo ilivyokuwa katika nyakati za upyaisho na ari ya kimisionari katika historia ya Kanisa, kwani walikuwa pamoja na wachungaji na waamini walei pamoja. Hawakuwa wamejitenga binafsi, bali walikuwa watu wanaoinjilisha! Watu Watakatifu wa Mungu.
Kushinda tabaka za kisosholojia yaani kijamii kwa sababu sisi ni wanafunzi
Mara baada ya kukumbuka umuhimu wa malezi ya walei, Baba Mtakatifu Francisko amesisitizia umuhimu kwa uwajibikaji wa kuishi mradi tu sio wa kisomi, kikomo cha mawazo ya kinadharia, lakini kwa njia ya matendo pia. Kwa njia hiyo ametoa mwaliko wa kila mtu kurejesha maana ya umuhimu wa kikanisa, kama ilivyokuwa katika karne za kwanza, ambamo kila kitu kiliunganishwa kuwa mali ya Kristo, na hivyo kuweza kushinda maono ya kisosholojia ambayo hutofautisha tabaka za kijamii na safu za kijamii na ambayo hatimaye hutegemea nguvu iliyopewa kila tabaka . Mkazo huo lazima uwekwe kwenye umoja na sio utengano. Mlei, kwa kuwa siyo mwenye wakfu wa daraja na wala kuwa mtazamo lakini anapaswa kuchukuliwa kama mtu aliyebatizwa, kama mshiriki wa watu watakatifu wa Mungu, ni sakramenti inayofungua milango yote. Katika Agano Jipya neno mlei halionekani, lakini kuna mazungumzo ya waamini, wanafunzi, ndugu, watakatifu, ambayo ni maneno yanayotumika kwa kila mtu kwamba “Walei waamini na wahudumu waliowekwa wakfu wa daraja.” Mawazo ya Baba Mtakatifu akiendelea na hotuba yake aligeukia, Waraka kwa Kanisa la Laodikia, wakati “Yesu aliposema “tazama niko mlangoni na ninabisha”. Lakini akasema: “leo hii kuna mchezo wa kushangaza wa Kanisa kwamba Yesu anaendelea kubisha mlango, lakini kwa nini hatutoki ndani na kuwacha atoke nje! Mara nyingi Kanisa linafungwa, haliwezi kumtoa Bwana.
Bwana alikuja kwa ajili ya utume na anataka sisi tuwe wamisionari”. Inahitajika ushirikiano mkubwa zaidi, ambapo Baba Mtakatifu Francisko amesema jukumu hilo la ushirikiano lililofanywa na uzoefu kati ya wachungaji na walei litaruhusu kushinda migawanyiko, hofu na tofauti zinazofanana. Kwa Upande wa Baba Mtakatifu Francisko amebainisha kwamba sasa ni wakati wa wachungaji na walei kutembea pamoja, katika kila eneo la Kanisa na kila sehemu ya ulimwengu. Kwa hiyo wito wa kuthamini zaidi walei, kwa wazo maalum kwa ajili ya wanawake ambapo amesema Waamini walei sio wageni katika Kanisa, kwa sababu wako nyumbani, kwa hivyo wameitwa kutunza nyumba zao wenyewe. Walei, zaidi ya wanawake wote, wathaminiwe zaidi katika ujuzi wao na karama zao za kibinadamu na kiroho kwa maisha ya parokia na majimbo. Wanaweza kuleta utangazaji wa Injili kwa lugha yao ya kila siku, wakijihusisha na aina mbalimbali za mahubiri.
Wanaweza kushirikiana na mapadre kufunda watoto na vijana, kusaidia wachumba kujiandaa kwa ajili ya ndoa na kuwasindikiza wanandoa katika maisha ya ndoa na familia. Wanapaswa kushauriwa kila wakati wakati wa kuandaa mipango mipya ya kichungaji katika kila ngazi, kikanda, kitaifa na ulimwengu mzima. Ni lazima wapewe sauti katika mabaraza ya kichungaji ya Makanisa mahalia. Ni lazima wawepo katika ofisi za majimbo. Wanaweza kusaidia katika usindikizaji wa kiroho wa walei wengine na pia kutoa mchango wao katika malezi ya waseminari na wa watawa.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekumbuka swali ambalo aliulizwa, yaani, ikiwa Mlei anaweza kuwa kiongozi wa kiroho. Jibu lake ni kwamba ni karama ya walei, sio ya kikuhani, inategemea kama Bwana atakuwa amempatia uwezo wa kufanya. Hivyo umuhimu wa wajibu wa walei pia katika mazingira ya kilimwengu. Kwa hiyo Papa amesisitiza kuwa pamoja na wachungaji, lazima watoe ushuhuda wa Kikristo katika mazingira wanamoishi ya ulimwengu kwa mfano ulimwengu wa kazi, utamaduni, siasa, sanaa, mawasiliano ya kijamii. Na hatimaye, onyo kutoka kwa Baba Mtakatifu ni lile na kuwaomba walei wasiingilie hali za ukasisi. Walei walioadhimishwa wakati mwingine wanaweza kuwa hata wabaya katika Kanisa. Kwa njia hiyo amewaomba kila mmoja katika nafasi na wajibu wake, bila kuingiliana bali kushirikiana na kushaurina kwa ajili ya wema wa kuinjilisha katika watu wa Mungu.