Tafuta

Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha.   (Vatican Media)

Papa Francisko: Umuhimu wa Michezo Katika Maboresho ya Maisha: Kimwili na Kiroho

Papa Francisko amekazia: Umuhimu wa michezo katika kupyaisha na kurahisisha maisha pamoja na kukuza mchakato wa mshikamano wa upendo kwa kuwajali na kuwasaidia watoto wanaohudumiwa kwenye Hospitali ya Bambino Gesù.” Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ni kwa mara ya kwanza anakutana na kuzungumza na wanamichezo wa mchezo wa “Pentathlon ya Kisasa”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika Waraka wake wa “Dare il Meglio di Se” yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” linakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika medani mbalimbali za maisha ili kufikia lengo linalotarajiwa. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: Ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha kwa kuhakikisha kwamba, kila mtu anajitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaobomolea mbali kuta za tabia ya ubinafsi, uchoyo na ubaguzi na hivyo kuwakirimia watu wateule wa Mungu ile furaha ya moyoni! Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Michezo isaidie maboresho ya mwili, roho na akili
Michezo isaidie maboresho ya mwili, roho na akili

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 10 Februari 2023 kwa mara ya kwanza katika maisha na utume wake, amekutana na kuzungumza na Maafisa na Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Italia ya “Pentathlon ya Kisasa”: “Dirigenti della Federazione Italiana Pentathlon Moderno e atleti della squadra nazionale.” Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa michezo katika kupyaisha na kurahisisha maisha pamoja na kukuza mchakato wa mshikamano wa upendo kwa kuwajali na kuwasaidia watoto wanaohudumiwa kwenye Hospitali ya Bambino Gesù.” Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ni kwa mara ya kwanza anakutana na kuzungumza na wanamichezo wa mchezo wa “Pentathlon ya Kisasa” unajumuisha michezo ya: Uzio, kuogolea, kuendesha Farasi, kulenga shabaha na riadha. Hii ni michezo ya zamani sana, lakini imepyaishwa, ili kumwezesha mwanamichezo walau kufahamu vizuri zaidi michezo mitano ambayo inahitaji: ujuzi na mazoezi tofauti vinavyomsaidia mwanaridhiana kujiendeleza kimwili, kiakili na kiroho. Ni mchezo unaoonesha umuhimu wa elimu ya michezo inayotekelezwa kwa uaminifu mkubwa, kwa kutumia vipimo mbalimbali ili kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii katika michezo, kwa kuweka uwiano mzuri katika michezo yote ili kupata mafanikio yanayo kusudiwa.

Michezo ni furaha, nidhamu na mshikamano
Michezo ni furaha, nidhamu na mshikamano

Hapa utu na heshima ya mwanadamu inaonekana katika medani mbalimbali za maisha; umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii; uwezo wa kubadilika na hivyo kusonga mbele katika hali ya utulivu na uhodari. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wanamichezo hawa kwa mfano na ushuhuda wao unaowafundisha watu wateule wa Mungu kujikita katika: Uvumilivu, mazoezi, ubunifu na ukakamavu, ili kuboresha maisha na hatimaye kufikia malengo yanayokusudiwa, licha ya magumu na changamoto zinazogeuzwa kuwa ni fursa za maendeleo. Ni katika muktadha huu, maisha ya kiroho yanapewa umuhimu wa pekee, ili kuweza kujenga mahusiano bora na kuishi na wengine katika hali ya amani, upendo na ukarimu. Hii ni changamoto ya kujenga moyo wa upendo na ukarimu; moyo unaofahamu kupokea na kutoa kwa ukarimu. Baba Mtakatifu anawashukuru wanamichezo kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa wanaohudumiwa kwenye Hospitali ya “Bambino Gesù” inayoendeshwa na kusimamiwa na Vatican. Wanamichezo watambue kwamba, thawabu yao ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu amewapatia heri na baraka katika mashindano ya ujenzi wa mshikamano wa huduma ya upendo.

Papa Michezo 2023

 

10 February 2023, 15:38