Papa Francisko: Majadiliano ya Kiekumene Yasimikwe Katika Upendo na Umoja
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anakazia uekumene wa: Damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha adili na matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia ni mambo yanayowaunganisha wote bila ubaguzi hata kidogo. Damu ya Wakristo, itaendelea kuwa ni mbegu ya Ukristo na mchakato wa umoja wa Wakristo. Wakristo wote wanateseka na kudhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kumbe, uekumene wa damu una nguvu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 23 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na Mapadre vijana pamoja na watawa kutoka Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu: Kipindi cha Kwaresima, umuhimu wa majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika upendo pamoja na shauku ya dhati ya kuwa na umoja. Baba Mtakatifu anasema, Jumatano ya Majivu inafungua maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima, sehemu muhimu sana ya maandalizi ya maadhimiho ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Katika Maandiko Matakatifu Mwinjili Luka anaonesha jinsi ambavyo Yesu Mfufuka alivyowatokea wafuasi wa Emau, akaandamana nao, akajadiliana na kuwafafanulia Maandiko Matakatifu juu yake na hatimaye, wakamtambua katika kuumega Mkate. Hivi ndivyo ilivyo pia katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili wakristo wote kwa pamoja waweze kumtambua Kristo Yesu anayeambatana nao, ili mwishowe aweze kuwaunganisha, hii ndiyo hija ya ushirika inayofumbatwa katika majadiliano ya upendo, ukweli na maisha; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mwongozo wa Majadiliano ya Kiekumene ulioandaliwa na Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Kuhamasisha Umoja wa Wakristo.
Majadiliano ya mahujaji wa Emau na Kristo Yesu ni fursa ya kukutana na Kristo Mfufuka anayeamua kufanya hija pamoja nao kwa kuwafafanulia Maandiko Matakatifu, kielelezo kwamba, majadiliano ya kiekumene yanasimikwa katika Maandiko Matakatifu yanayofafanuliwa na Kristo Yesu kwa msaada wa mwanga wa Roho wake Mtakatifu. Yesu hawalazimishi wafuasi wake kutambua uwepo wake angavu, lakini wakimkaribisha, kwa hakika macho yao yanafumbuliwa na hivyo kumtambua katika kuumega mkate. Kumbe, kuna haja ya kuweka nia ya dhati kabisa kwa jili ya kupata umoja wa Wakristo, nia mbayo inamwilishwa katika maisha ya sala; kwa moyo wote na nguvu zote bila ya kuchoka wala kukata tamaa. Kwa kujadiliana na kutembea kwa pamoja kutawasaidia kuwa na nguvu ya kumkaribisha, kumpokea na kumega Mkate kwa pamoja. Nia thabiti ya kuumega mkate pamoja na Kristo Yesu inakosekana katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo.
Umoja wa Kanisa upewe kipaumbele cha kwanza kuliko mafao mengine yote! Kwa njia hii, Wakristo wataweza kujenga na kudumisha ushirika na Kristo Yesu pamoja na Wakristo wenzao kwa kuumega na kushiriki Fumbo la Ekaristi, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kama ilivyokuwa kwa mahujaji wa Emau walivyoamua kurejea tena Yerusalemu ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, “ili ulimwengu upate kusadiki.” Yn 17:21. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa hotuba yake amewataka Mapadre vijana pamoja na watawa kutoka Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili na Kristo Yesu Mfufuka. Wakuze na kukoleza majadiliano ya kidugu, ili kupyaisha na kunogesha moto wa ushirika. Baba Mtakatifu amewataka mahujaji hawa kumfikishia salam zake za rambirambi kwa wote walioguswa na kutikiswa na tetemeko la ardhi lilijitokeza nchini Uturuki na Siria. Jumuiya ya Kimataifa iamue na kutenda kwa hekima na busara, ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vya kiuchumi ili misaada iweze kupelekwa na kuwafikia walengwa.