Tafuta

Kauli mbiu inayonogesha Mkutano huu ni “Uongozi wa Watu Asilia Kuhusu Masuala ya Tabianchi: Suluhisho la Kijamii ili Kuimarisha Ustahimivu na Bioanuai.” Kauli mbiu inayonogesha Mkutano huu ni “Uongozi wa Watu Asilia Kuhusu Masuala ya Tabianchi: Suluhisho la Kijamii ili Kuimarisha Ustahimivu na Bioanuai.”  (ANSA)

Papa Francisko: IFAD: Mchango wa Watu Asilia Katika Utunzaji Bora wa Mazingira

Kauli mbiu inayonogesha Mkutano huu ni “Uongozi wa Watu Asilia Kuhusu Masuala ya Tabianchi: Suluhisho la Kijamii ili Kuimarisha Ustahimivu na Bioanuai.” Hii ni fursa makini ya kutambua na kuthamini umuhimu wa watu asilia katika kutunza mazingira nyumba ya wote na kupata suluhu kwa changamoto za kimataifa, zinazoendelea kuleta madhara makubwa kwa binadamu kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Jukwaa la Watu Asilia unaofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, “International Fund for Agricultural Development; IFAD), unapania kuragibisha mapambano dhidi ya umaskini na baa la njaa duniani, kwa kuwekeza katika sekta ya kilimo vijijini katika Nchi zinazoendelea. Mkutano huu umefunguliwa rasmi tarehe 9 Februari na unahitimishwa tarehe 13 Februari 2023. Kauli mbiu inayonogesha Mkutano huu ni “Uongozi wa Watu Asilia Kuhusu Masuala ya Tabianchi: Suluhisho la Kijamii ili Kuimarisha Ustahimivu na Bioanuai.” Hii ni fursa makini ya kutambua na kuthamini umuhimu wa watu asilia katika muktadha wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, mintarafu hekima na busara zinazowaongoza kupata suluhu kwa changamoto za kimataifa, zinazoendelea kuleta madhara makubwa kwa binadamu kila kukicha! Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 10 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Jukwaa la Watu Asilia unaofadhiliwa na Mfuko wa IFAD. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: mchango wa watu asilia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia, Ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kuondokana na ubaguzi na mifumo mbalimbali ya ukoloni mamboleo pamoja na mchango wa IFAD katika kuragibisha mshikamano na haki jamii.

Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Jukwaa la Watu Asilia 2023
Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Jukwaa la Watu Asilia 2023

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa inashuhudia kwa kiasi kikubwa athari za mabadiliko ya tabianchi, changamoto kubwa kwa sasa ni kusimama kidete, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kufanya wongofu katika mtindo wa maisha, miundo ya uzalishaji na ulaji. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza wazawa na hivyo kujifunza kutokana na mfumo wao wa maisha, utunzaji bora wa mazingira pamoja na kuheshimiana. Kumbe, mchango wa watu asilia ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Leo hii kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya maisha ya binadamu, kuna idadi kubwa ya watu wanaodai mabadiliko katika miundo mbinu ya madaraka inayosimamiwa na Mifumo ya Nchi za Magharibi sanjari na kubadili mahusiano na mafungamano ya kihistoria unaainishwa na ukolon na ubaguzi; mambo yanayohitaji kupyaishwa na kuboreshwa zaidi. Kuna haja ya kujikita katika umoja, ushirikiano na mshikamano wa kidugu, ili kukabiliana kikamilifu na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa sababu watu wote katika ujumla wao wanaathirika.

Watu asilia katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira
Watu asilia katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira

Baba Mtakatifu Francisko anawaomba wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwatambua na kuwaheshimu watu asilia, kuthamini na kuenzi: tamaduni, lugha, mila na desturi njema: kiroho na kimwili; Kwa kuthamini na kuheshimu: utu, heshima na haki zao msingi, kwa kutambua kwamba, utajiri wa familia kubwa ya binadamu, kwa kiasi kikubwa unafumbatwa katika utofauti. Kuwapuuza na kushindwa kuwathamani watu asilia katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ni kosa na dhuluma kubwa mbele yao. Na kwa upande mwingine, utu, amana na urithi wao wa kitamaduni utasaidia kuanzisha njia bora za utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu mwishoni, ameiupongeza Mfuko wa IFAD kwa kusaidia jamii asilia katika mchakato wa kujipatia maendeleo makubwa ya uhuru jamii. Juhudi hizi hazina budi kuongezwa, kwa kuzingatia ukweli na uwazi, ili kufikia mabadiliko ya haki. Baba Mtakatifu Francisko kwa njia hii amependa kuwaonesha ukaribu wake na anaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ifad 2023
10 February 2023, 16:01