Papa ametoa wito kusitisha matukio ya vurugu kwa Nchi Takatifu na Burkina Faso
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, kwa waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican Dominika tarehe 26 Februari 2023, ameelezea uchungu wake kutokana na matukio mabaya ya ulimwengu. Kwanza kabisa alisema: "Habari za uchungu bado zinafika kutoka Nchi Takatifu: watu wengi waliuawa, ikiwa ni pamoja na watoto ... Je, tunawezaje kukomesha wimbi hili la vurugu? Ninarudia kutoa ombi langu la kufanya majadiliano ili kuweza kushinda chuki na kulipiza kisasi, na ninamwomba Mungu kwa ajili ya Wapalestina na Waisraeli, ili wapate njia ya udugu na amani, kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa".
Majanga ya kigaidi nchini Burkina Faso
Baba Mtakatifu akiendelea ameonesha pia wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya nchi ya Burkina Faso, ambako mashambulizi ya kigaidi yanaendelea. kwa njia hiyo ametoa: "mwaliko wa kuwaombea wakazi wa nchi hiyo pendwa, ili vurugu walizopata zisiwafanye wapoteze imani katika njia ya demokrasia, haki na amani".