Tafuta

Tarehe 11 Februari 2023 inabeba matukio mazito katika maisha na utume wa Kanisa: Mkataba wa Lateran Miaka 94; Uhuru wa Vatican na Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani 2023. Tarehe 11 Februari 2023 inabeba matukio mazito katika maisha na utume wa Kanisa: Mkataba wa Lateran Miaka 94; Uhuru wa Vatican na Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani 2023.  (Vatican Media)

Miaka 94 ya Mkataba wa Lateran: 1929-2023: Uhuru, Wagonjwa & Papa Benedikto XVI

Tarehe 11 Februari 2023: Kumbukizi ya Miaka 94 ya Mkataba wa Lateran. Kumbukumbu ya B. Maria wa Lourdes sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Dunianii. Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipotangaza kung’atuka kutoka madarakani kutokana na hali yake ya afya kuanza kudhorota, akafariki dunia tarehe 31 Desemba 2022.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 11 Februari 2023 inabeba matukio mazito katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni Siku ya Kumbukizi ya Mkataba wa Lateran “Patti Lateranensi: Lateran Treaty” uliotenganisha Kanisa na Serikali ya Italia na hivyo kuondoa kinzani na mwingiliano wa majukumu kati ya Taasisi hizi mbili zenye dhamana na majukumu tofauti, lakini zote zikiwa ni kwa ajili ya huduma kwa mwanadamu. Tangu wakati huo Mama Kanisa akajikita zaidi katika masuala ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu. Ni uinjilishaji unaojielekeza zaidi katika ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili.  Pili ni kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye maadhimisho haya anakazia umuhimu wa kutenda kadiri ya mtindo wa Mungu; kwa kufuata mfano wa Msamaria mwema, ili kuondokana na upweke hasi na hali ya kutelekezwa. Kanisa liwe ni hospitali katika uwanja wa mapambano, kwa kujielekeza zaidi katika ushirikiano na udugu wa kibinadamu katika huduma kwa wagonjwa. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wafanyakazi katika sekta ya afya kwa huduma na tafiti zao.

Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2023
Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2023

Huu ni mwaliko kwa jumuiya za Kikristo kujipambanua katika huduma kwa wagonjwa. Siku ya Wagonjwa Duniani ni nafasi ya kutafakari kanuni maadili na utu wema; sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa na wazee, tayari kusoma alama za nyakati kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wagonjwa na wale wanaoteseka. Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Kanisa Katoliki ni siku maalum kwa ajili ya kukoleza uragibishaji na maadhimisho yanayokusudia kuwasaidia waamini kusali na kushiriki mateso ya wagonjwa; na kwa wagonjwa wenyewe kutolea mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu na hatimaye, kuwaonjesha wagonjwa kuwa ni sura na ufunuo wa Kristo Yesu, anayeteseka kati pamoja nao. Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipotangaza kung’atuka kutoka madarakani kutokana na hali yake ya afya kuanza kudhorota. Walimwengu wakapigwa bumbuwazi. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akafariki dunia tarehe 31 Desemba 2023. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 5 Januari 2023, akaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Hayati Benedikto XVI kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani “Ultima Commendatio & Valedictio” na mazishi kufanyika kwenye Makaburi yaliyoko chini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican “Grotte Vaticane.”

Papa Benedikto XVI: Imani, Matumaini na Mapendo
Papa Benedikto XVI: Imani, Matumaini na Mapendo

Mwili wa Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ulitolewa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican saa 2:45 asubuhi kwa saa za Ulaya na kuwekwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tayari kwa Ibada ya Misa Takatifu, wakati wote huo, waamini wakasali Rozari Takatifu, huku wakimsindikiza Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika usingizi wa amani. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake alikazia umuhimu wa kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma na kuendelea kupata faraja kutoka kwa Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia uzuri na furaha ya Injili, Sheria ya shughuli za kichungaji. “Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho.” Lk. 23:46. Vatican ni kati ya nchi ndogo kabisa duniani, tarehe 11 Februari, 2023 inatimiza miaka 94 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana saini Mkataba na Serikali ya Italia “Inter Sanctam Sedem e Italiae Regnum Conventiones” kwa kifupi “Patti Lateranensi” yaani “Mkataba wa Lateran” unaoratibiwa na kusimamiwa na Sheria za Kimataifa na hivyo kuhitimisha kile kilichojulikana “Masuala ya Roma, Questione Roman.” Hii ni Italia iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha shughuli za Kanisa na Serikali ya Italia.

Mkataba wa Lateran 11 Februari 1929
Mkataba wa Lateran 11 Februari 1929

Kardinali Pietro Gasparri, Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati huo kwa niaba ya Kanisa pamoja na Bwana Benito Mussolini, Waziri Mkuu wa Italia kwa niaba ya Serikali ya Italia, walitiliana saini Mkataba wa Lateran maarufu kama “Patti Lateranensi.” Mkataba huu ulikuwa na sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuhitimisha kinzani na mpasuko uliokuwa umejitokeza baada ya Serikali ya Italia kuvamia mji wa Roma kunako mwaka 1870. Mkataba huu ulitoa uhuru kwa Kanisa Katoliki nchini Italia kuweza kujiamria mambo yake bila kuingiliwa na Serikali. Huu ni msingi wa uhuru wa kuabudu. Vatican ikapewa mamlaka kamili ya kujisimamia yenyewe katika shughuli zake na Serikali ya Italia, tangu wakati huo ikatambua uhuru na mamlaka ya mji wa Vatican hata katika udogo wake. Mkataba huu, uliiwezesha Vatican “Kiti Kitakatifu-Holy See” kuwa na uhuru kamili kuhusiana na masuala ya dini na imani. Sehemu ya Pili ya Mkataba huu, uliitaka Serikali ya Italia kulipa fidia kwa Vatican kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na Serikali wakati wa kuvamia mji wa Roma ambao ulikuwa ni ngome ya Kanisa Katoliki, kunako mwaka 1870. Serikali ikailipa Vatican fidia. Sehemu ya tatu ya Mkataba huu ni kuhusu “Makubaliano ya Kifedha” “Convenzionale Finanzarie.”

Makubaliano ya Kifedha
Makubaliano ya Kifedha

Huu ni utaratibu na kanuni zinazoratibu mchakato wa mahusiano ya ndani kati ya Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki nchini Italia. Katika sehemu hii, Maaskofu walipaswa kula kiapo cha utii kwa Serikali. Na Serikali kwa upande wake, ikalipatia Kanisa upendeleo wa kufundisha dini na kumwilisha Mafundisho tanzu ya Kanisa katika maisha ya hadhara.Serikali ya Italia ikatambua Sakramenti ya Ndoa na utenguzi wake kufanyika kwenye Mahakama za Kanisa. Mkataba wa Lateran uliifanya Vatican kutambuliwa rasmi kama nchi huru yenye uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe katika medani za kimataifa bila kuingiliwa na Serikali ya Italia.Papa Pio XI alilitaka Kanisa kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia: kiroho na kimwili; kwa kutumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kitamaduni na kisanaa; mambo yanayofumbatwa katika Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihakikishia Italia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili kweli nchi ya Italia, iendelee kuwa aminifu kwa Mapokeo pamoja kupyaisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu ambao umeipambanua Italia kwa miaka mingi. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni katika hotuba yake elekezi kwenye Kongamano la kitaifa lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko Roma na kuongozwa na mada “Umuhimu wa Vatican katika muktadha wa Jumuiya ya Kimataifa 1929 – 2019”, alikazia: uhuru wa kuabudu, uhuru wa kidini, utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Amesema, hizi ni changamoto ambazo zimepewa kipaumbele cha pekee na Vatican katika kipindi cha zaidi ya miaka 90 ya uwepo na utume wake.

Diplomasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Diplomasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za binadamu

Vatican imekazia umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu dhamiri nyofu za watu, mahali patakatifu sana katika maisha ya mwanadamu! Ikumbukwe kwamba, Haki msingi za binadamu zinazozungumziwa hapa ni zile zinazofafanuliwa katika Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na wala si ukoloni wa kiitikadi unaotaka kupenyezwa kwa mataifa maskini duniani! Kardinali Parolin, alitumia fursa ya mkutano huu, kufafanua vipengele mbali mbali vilivyomo kwenye Mkataba wa Lateran kwa kusema, kwamba, Mkataba huu, umekuwa ni ngome na ulinzi thabiti kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kuweza kutekeleza dhamana na utume wake kwa uhuru zaidi, bila kuingiliwa na chombo chochote kile! Dhamana na wito wa Vatican katika diplomasia, unafumbatwa katika utume wake wa maisha ya kiroho, kimaadili na utu wema kwa ajili ya familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Vatican haipendi kuingilia mambo ya ndani ya nchi, bali inapenda kusikilizwa kwa makini, kama chombo cha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, dhamana inayotekelezwa kwa unyoofu na unyenyekevu mkuu!

Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo

Itakumbukwa kwamba, Mkataba wa Lateran, ulifanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuendana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican. Ushirikiano kati ya Serikali ya Italia na Vatican unaolenga kulinda, kudumisha na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mkataba unaojipambanua kwa kukazia uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Nchi ya Vatican inapaswa kuendelea kuwepo, ikiwa huru katika kujiamria mambo yake yenyewe, ili kutekeleza utume wake katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote. Mifumo ya kisiasa na sera mbali mbali zinazogusa utu, heshima na maisha ya mwanadamu na hata wakati mwingine kuzama katika undani wake. Vatican imekuwa mstari wa mbele kukemea uhuru usiokuwa na mipaka wala uwajibikaji; imekazia majadiliano katika ukweli na uwazi na mshikamano wa kidugu. Vatican ni kati ya nchi ambazo ziko mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu, kama mtu mmoja mmoja au taifa. Zote hizi ni kati ya sababu ambazo zinahalalisha uwepo wa Nchi ya Vatican ili iweze kutekeleza majukumu yake katika misingi ya ukweli, haki na uwazi.

Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru mwingine wote.
Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru mwingine wote.

Vatican kutokana na ushiriki wake kwenye Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kutoa mchango mkubwa unaofumbata maendeleo fungamani binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, uhuru wa kuabudu na ule wa kidini unazingatiwa na kuheshimiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Mama Kanisa anapenda kutekeleza wajibu na utume wake akiwa huru kabisa, ili kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uhuru wa kidini ni haki ya kila dini au dhehebu lolote lile kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za nchi husika. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamekazia umuhimu wa Kanisa na Serikali kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu: kiroho na kimwili. Uhusiano kati ya Kanisa na Serikali unategemea kwa kiasi kikubwa: hali ya kitamaduni, kijamii, kisiasa na kihistoria kwa nchi husika. Mahali ambapo utawala wa sheria unaheshimiwa, Kanisa limekuwa likitekeleza wajibu kwa ajili ya maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Lakini, katika baadhi ya nchi, Kanisa limekuwa likikumbana na madhulumu na sera za kibaguzi zinazolibeza Kanisa kwa kudhani kwamba, linaingilia mambo yake. Kanuni ya mpe Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu inapaswa kuwaongoza wanasiasa wenye misimamo mikali ya maisha. Kanisa, daima limeendelea kusoma alama za nyakati na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapaswa kutekeleza dhamana na utume wake katika mazingira huru kabisa. Kamwe, Khalifa wa Mtakatifu Petro, hatasita kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki msingi za wakimbizi na wahamiaji pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Biashara haramu ya silaha duniani, biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyavalia njuga katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Mkataba wa Laterano

 

10 February 2023, 16:19